Habari Mseto

Sheria mpya ya SACCO yaibua tumbojoto Kiambu

November 1st, 2018 1 min read

Na ERIC WAINAINA

MZOZO unanukia kuhusu utekelezaji wa sheria inayodhibiti usimamizi wa Vyama vya Ushirika (SACCO) katika Kaunti ya Kiambu.

Sheria hiyo ikitekelezwa kikamilifu, itabidi wasimamizi wa vyama vyote vya ushirika waliopo waondoke mamlakani kabla miezi sita ikamilike.

Sheria hiyo ambayo ilipitishwa Oktoba 12 baada ya kutiwa sahihi na gavana Ferdinand Waititu, imesababisha uhasama kati ya wadau katika sekta ya vyama vya mashirika, huku wengine wao wakielekea mahakamani kuipinga.

Kinachotia wasiwasi zaidi kuihusu ni kwamba itakuwa hatia kwa afisa kuhudumu kwa zaidi ya hatamu mbili mfululizo, kumaanisha huenda maafisa wengi wanaohudumu sasa waondoke kwani wamekuwa mamlakani kwa zaidi ya kipindi hicho.

Bw Waititu alidai sheria hiyo imenuiwa kuleta usimamizi bora kwa vyama vya ushirika na vitahitajika kurekebisha sheria zao za kiusimamizi ambazo hivi sasa nyingi zinaruhusu maafisa kuhudumu kwa muda mrefu.

“Kipindi cha kuhudumu kwa wanachama (wa kamati) kitawekwa wazi kwenye sheria za usimamizi na kipindi hicho hakitazidi miaka mitatu na afisa hatatumikia kwa zaidi ya vipindi viwili mfululizo,” sehemu ya sheria hiyo inasema.

Sehemu ya 57(5) ya sheria hiyo inahitaji vyama vyote vya ushirika ambavyo viliundwa kabla sheria hiyo ianze kutumiwa, vihakikishe kuna mkutano mkuu maalumu kabla miezi sita ikamilike ili vitimize mahitaji ya sheria mpya.

Hii ni kumaanisha vyama vingi vya ushirika vitahitajika kuandaa mkutano wa kuchagua viongozi wapya kwani wengi waliopo wamehudumu kwa zaidi ya vipindi viwili.

Wadau katika sekta hiyo wamelalamika kwamba sheria mpya ina sehemu nyingi zisizofaa na zinakinzana na sheria nyingine zilizopo za kitaifa zinazosimamia SACCO.