Makala

SHERIA: Ndoa muungano wa hiari ila sharti sheria ifuatwe

March 9th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

JOYCE Adhiambo kutoka Migori, Joseph Kaingu kutoka Kilifi na Harrison Kamau kutoka Kagio, Kirinyaga, wanataka kujua kwa nini watu hufunga ndoa bila kufuata utaratibu wa kisheria ilhali sheria inatoa adhabu kwa wanaoikiuka.

Wanatoa mfano wa ndoa za kitamaduni ambapo watu huanza kwa kuishi kama mume na mke kabla ya kutembelea wazazi kujadili mahari ambayo huchukua muda kabla ya kulipwa.

Kwanza, kitu muhimu kabisa katika ndoa na ambacho ni cha kwanza kutambuliwa kisheria ni kuwa ndoa ni muungano wa hiari kati ya watu wawili wa jinsia tofauti.

Ni lazima watu wakubaliane kuwa mume na mke na ndoa wanayotaka kufanya.

Kuna wanaokubaliana kuishi pamoja wakisubiri kutimiza desturi za ndoa za jamii zao na kuna wanaokubaliana kuwa wakamilishe utaratibu wa kulipa mahari kabla ya kuanza kuishi pamoja kama mume na mke.

Hata hivyo, katika kusajili ndoa yao huwa hakuna njia ya mkato.

Huwa ni lazima masharti yote ya kisheria yatimizwe kikamilifu na hii huwa ni kwa manufaa ya pande zote.

Hili ni muhimu

Ni muhimu kuelewa kwamba hata watu wakikubaliana kuishi pamoja kwa miongo saba bila kusajili ndoa yao, huwa hawajatimiza mahitaji ya kisheria.

Kabla ya msajili kunakili ndoa kuwa imesajiliwa, huwa anathibitisha kwamba ilizingatia mahitaji yote ya kisheria na akiridhika kwamba sheria ilifuatwa kikamilifu, basi ataisajili na kuorodhesha katika sajili ya ndoa.

Mahakama nchini Kenya zimeamua kesi nyingi za watu kuishi pamoja bila kusajili ndoa na kila kesi huwa inaamuliwa kivyake kwa kuzingatia ushahidi na maombi yanayowasilishwa kortini.

Nimekuwa nikisisitiza katika makala haya kwamba kusajili ndoa huwa ni kwa manufaa ya pande zote kwa sababu japo ndoa ni hiari, sheria ni lazima itimizwe.

Hii ni pamoja na kuadhibiwa kwa kuikiuka.