Makala

SHERIA: Njia za mkato kufunga ndoa zitakutia motoni

September 7th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

IKIWA wewe ni kiongozi wa kidini, unafaa kuwa mwangalifu sana usifungwe jela kwa kusimamia au kufungisha harusi bila mashahidi.

Hii ni kwa sababu imeibuka kuwa kuna wahubiri wanaotumia njia za mkato kutangaza watu kuwa mume na mke bila kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.

Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, ni lazima sherehe ya harusi ishuhudiwe na mashahidi wawili ambao ni watu wazima na ambao wanapaswa kutekeleza jukumu kubwa katika maandalizi ya harusi.

Pasta mwenyewe hawezi kuwa shahidi katika ndoa anayosimamia na kwa hivyo anafaa kuhakikisha mashahidi wapo ili ndoa iwe imekamilika.

Akikosa kufanya hivyo, anavunja sheria na anaweza kuadhibiwa kwa kufungwa jela miezi mitatu, kutozwa faini ya Sh10,000 au adhabu zote mbili.

“Mtu anayesimamia muungano unaochukuliwa kuwa ndoa, ambao mashahidi wanapaswa kuwepo lakini hawepo, huwa anavunja sheria na akipatikana na hatia anaweza kufungwa jela kipindi cha miezi mitatu au kutozwa faini ya Sh10,000 au hukumu zote mbili,” inaeleza sheria ya ndoa ya Kenya.

Kwa hivyo, kuna haja ya viongozi wa kidini kuhakikisha mashahidi wapo kabla ya kuunganisha wanandoa.

Mashahidi katika ndoa na viongozi wa kidini pia wanaweza kujipata wakikwaruzana na sheria wakishuhudia harusi wakijua kwamba mmoja wa wanandoa hajatimiza umri wa miaka 18, ilani ya ndoa haikutolewa siku 21 kabla ya harusi inavyoeleza sheria ya ndoa au ilani hiyo iliwasilishwa na haikushughulikiwa au kuondolewa.

Kifungo jela miezi sita

Mtu akipatikana na hatia ya kupuuza mahitaji haya ya kisheria anaweza kufungwa jela kwa miezi sita, kutozwa faini ya Sh50,000 au kupatiwa adhabu zote mbili.

Adhabu sawa pia huwapata wanaolazimisha watu kuolewa au kuoa bila hiari yao au wanaotumia njia za ulaghai kuwanasa wanawake au wavulana kuwa wake na waume zwao.

Kwa hivyo, kuna adhabu kwa wanaotumia njia za mkato katika masuala yote yanayohusu ndoa na njia ya pekee ya kuepuka ni kufuata sheria kikamilifu.