Makala

SHERIA: Tatizo la ulaghai wa wahubiri katika usajili wa ndoa

April 27th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

JAMES Wekesa kutoka Chwele anataka kujua hatua za kisheria ambazo kiongozi wa kidini anafaa kuchukuliwa kwa kupotosha wanandoa wakati wa harusi.

Anasema aligundua kwamba mhubiri aliyeongoza harusi hakusajili ndoa yake inavyopaswa kwa sababu hakuna rekodi katika sajili ya ndoa katika ofisi ya msajili.

Ingawa nimewahi kuangazia suala hili katika makala yaliyotangulia, ningetaka kufafanua ifuatavyo sio tu kwa manufaa ya msomaji huyu peke yake bali kwa wengine ambao wamejipata au wanajua watu waliojipata katika hali sawa.

Mtu anayepotosha wanandoa kwa njia yoyote anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kushtakiwa kortini.

Kwanza kabisa, ni makosa kwa mtu yeyote anayefungisha ndoa kukosa au kukataa kuisajili kisheria.

Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, mtu kama huyo anaweza kutozwa faini ya Sh5,000 au kuhukumiwa kufanya kazi ya umma iwapo atapatikana na hatia.

Pili, sheria inasema mhubiri au yeyote anayefungisha ndoa ni lazima awe ameidhinishwa na msajili wa ndoa, anafaa kuwasilisha nakala ya cheti cha ndoa kwa msajili ndani ya siku 14 baada ya harusi ili ndoa isajiliwe.

Kabla ya msajili kunakili ndoa kuwa imesajiliwa, huwa anathibitisha kwamba ilizingatia mahitaji yote ya kisheria na akiridhika kwamba sheria ilifuatwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuongozwa na mtu aliyeidhinishwa kisheria, basi ataisajili na kuorodhesha katika sajili ya ndoa.

Msajili akigundua kuna mahitaji ambayo hayakutimizwa, hawezi kuorodhesha ndoa katika sajili ya ndoa.

Ushauri

Ni muhimu kwa mtu kutafuta ushauri kutoka kwa msajili wa ndoa ili amweleze sababu ya ndoa kukosekana katika orodha ya zile zilizosajiliwa. Ikiwa makosa ni ya pasta, basi kuna utaratibu wa kisheria wa kufuata ili aadhibiwe.

Ni baada ya kugundua sababu ambapo hatua za kurekebisha dosari zinaweza kuchukuliwa kwa ushauri wa msajili au wakili.

Kile ambacho msomaji huyu hakueleza ni ikiwa ndoa yake imesajiliwa katika sajili ya ndoa ya kanisa alilofanyia harusi. Sajili ya ndoa ya kanisa au eneo la umma la kuabudu inatambuliwa kisheria kama thibitisho la ndoa.

Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba ndoa haifai kusajiliwa rasmi kwa msajili wa ndoa.