Sheria ya watu fisadi kuepuka korti yatua bungeni

Sheria ya watu fisadi kuepuka korti yatua bungeni

Na IBRAHIM ORUKO

WASHUKIWA wanaokabiliwa na ufisadi huenda siku zijazo wakahepa kufungwa gerezani iwapo watakubali kushirikiana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kisha kusalimisha utajiri wao na kukiri kushiriki uhalifu walioutenda.

Senata Mteule Farhiya Ali ameandaa mswada ambao utahakikisha kuwa wafisadi wanasamehewa makosa yao ila kwa masharti hayo makali.

Bi Ali anapigia upato mswada huo kutokana na kucheleweshwa kwa kesi za ufisadi na mwisho washukiwe kuachiliwa huru au kupewa adhabu nyepesi.

“Maelewano na afisi ya DPP hasa kwa wale waliohusika katika uhalifu wa kiuchumi unaohitaji uchunguzi wa ndani ni wanafaa waruhusiwe kuepuka adhabu. Hii ni kwa sababu kesi hizo huchukua muda tena kwa gharama kubwa ilhali mwishowe baadhi ya washukiwa huishia kuponyoka,” akasema Bi Ali kwenye mswada huo unaolenga pia kuipa afisi ya DPP nguvu nyingi.

Mswada huo unapendekeza kwamba kabla ya kesi ya ufisadi kuanza dhidi ya mshukiwa, afisi ya DPP inafaa imwalike mshukiwa huyo ili kumuuliza iwapo ataingia kwenye makubaliano ya kutatua ufisadi huo au iwapo yuko tayari kufuata mkondo wa kisheria mahakamani.

Ingawa hivyo, DPP anafaa akumbatie njia hiyo iwapo ana uhakika kwamba maslahi ya umma yatatiliwa maanani na makubaliano hayo yataheshimiwa na kukamilishwa kwa kipindi kilichokubalika.

Nakala ya mashtaka iliyoandaliwa na DPP kuhusu uhalifu huo, taarifa zenye hoja za kesi, haki ya mshukiwa na upande wa mashtaka pamoja na kukiri kwa mshukiwa kuhusika katika ufisadi huo ni kati ya masuala ambayo yatazingatiwa.

Aidha, mshukiwa atatarajiwa kusalimisha mali aliyonunua akitumia pesa za ufisadi, alipe riba kwenye pesa hizo na pia kulipa afisi ya DPP pesa za ziada kwa kuingia makubaliano hayo ambayo yatalingana faini ambayo korti ingemtoza.

Afisi ya DPP hata hivyo itaingia mkataba na mshukiwa baada ya kumwalika na maaganoo hayo kuidhinishwa na Mahakama Kuu kulingana na mswada huo.

“Jaji Mkuu wa mahakama kuu lazima ashawishike kuwa masharti ya makubaliano hayo ni ya haki na yanazingatia maslahi ya umma huku pia uwazi ukitiliwa maanani,” akasema Bi Ali.

Aidha, mswada huo unapendekeza kuwa kusikizwa kwa pendekezo la mshukiwa kushiriki mkataba huo, kutasikizwa mahakamani “kwa njia ya kamera” lakini uamuzi wake utatangazwa hadharini kortini.

Pia DPP lazima ahakikishe kuwa mshukiwa hana rekodi ya uhalifu na kutathmini kwa undani jinsi ambavyo amekuwa akishirikiana na asasi za uchunguzi kabla ya kumwalika kwa kikao cha kujadili na kuafikiana kuhusu makubaliano ya kuzuia kesi hiyo kuwasilishwa na kuamuliwa kortini jinsi ilivyo kwa sasa.

Wakati ambapo makubaliano hayo yanasimama, mshukiwa lazima ayaheshimu na akikosa kufanya wajibu wake, DPP atarejea katika mahakama kuu kupata amri ya kuyatupilia mbali au mshukiwa alazimishwe kuwajibika.

Hata hivyo, mahakama kuu inaweza kutoa uamuzi ambapo maagano mengine mapya kati ya pande zote mbili yataafikiwa iwapo mshukiwa amelemewa kuwajibika kulingana na masharti ya mwanzo.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ughaibuni si mbinguni, huko pia kuna magumu

Uholanzi kushirikiana na Kenya kuibuka na aina ya viazi...