Habari MsetoSiasa

'Sheria yalenga kumzima Ruto'

December 15th, 2019 2 min read

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Rais Dkt William Ruto, huenda akapata pigo baada ya serikali kupendekeza sheria inayowapiga marufuku watumishi wa umma kushiriki michango ya harambee.

Kulingana na mswada unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote, watumishi wa umma watakuwa wakishiriki harambee kupitia idhini ya Rais pekee na hii itakuwa kuchanga pesa wakati wa kusaidia waathiriwa wa majanga ya kitaifa.

Idhini ya rais, unapendekeza mswada huo, itakuwa kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali.

Dkt Ruto ameapa kuendelea kuzuru maeneo mbalimbali nchini kuchangia makanisa kufadhili miradi mbalimbali jambo ambalo litawekwa breki iwapo mswada huo utapitishwa kuwa sheria bungeni.

Wakosoaji wake wamekuwa wakimlaumu kwa kushiriki ufisadi kisha kuwafumba macho raia kwa kutoa fedha hizo kwenye michango.

“Afisa anayeshikilia afisi ya umma hataruhusiwa kisheria kushiriki michango ya harambee kwa njia ambayo inazua maswali mengi kuhusu uwazi, uadilifu wake au mwingiliano wa majukumu ya afisi yake,” unasema mswada huo.

Aidha, watumishi wa umma wenye tabia ya kutoa kandarasi za serikali kwa marafiki au jamaa zao wapo hatarini kutimuliwa na kufunguliwa mashtaka iwapo sheria hiyo itapitishwa.

Wakati wa sherehe za Jamhuri Alhamisi, Rais Uhuru Kenyatta alijitosa kwenye mjadala huo baada ya kuwakemea wanasiasa ambao wanaingilia kazi ambazo zinagongana na majukumu yao na kutilia shaka maadili yao ya uongozi.

Matamshi ya kiongozi wa nchi hasa yalilenga wabunge mawakili ambao wamekuwa wakiwakilisha viongozi wanaoshukiwa kwa ufisadi kila mara wanapofikishwa kizimbani kujibu mashtaka ya uporaji.

Rais alionekana kuwalenga Maseneta Mutula Kilonzo Jr (Makueni) na Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) ambao wiki jana walikuwa mawakili wa Gavana wa Nairobi Mike Sonko anayekabiliwa na mashtaka ya kupora Sh357 milioni wakati wa utoaji wa tenda za kaunti.

Aidha, Rais Kenyatta aliwataka wanasiasa kutotumia afisi za serikali kuendeleza masuala yao ya kibinafsi ambayo hayana manufaa kwa raia.

“Hili ni jambo rahisi. Unahitaji kuhudumia umma kwenye wadhifa uliochaguliwa ama uamue kuhudumia umma kama raia wa kawaida. Kama kiongozi hauruhusiwi kushiriki majukumu yanayogongana na afisi unayoshikilia,” akasema Rais Kenyatta.

Kazi sasa ipo mikononi mwa Mwanasheria Mkuu ambaye aliagizwa na Rais kuandaa mapendekezo hayo kama mswada kisha kuyawasilisha kwa baraza la mawaziri ambalo litayatuma kwa bunge.

“Mtumishi wa umma ambaye anachunguzwa kwa kukiuka sheria hii ataondoka afisini baada ya afisi ya Rais kupokea barua kutoka kwa Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi (EACC). Ataondoka afisini kwa muda wa siku 90 ili kupisha uchunguzi,” ikapendekeza mswada huo.

Mapendekezo mengine ya sheria hiyo pia inawaamrisha maafisa wa umma kutopokea zawadi yoyote ambayo huenda ikawashawishi kutoa uamuzi kwa mapendeleo.

Watumishi wa umma nao watatakiwa kueleza kiwango cha mali wanayomiliki na watakaotoa habari za uongo kuhusu hilo kwa EACC wapo kwenye hatari ya kupigwa faini ya Sh5 milioni.

Kila mtumishi wa umma atakuwa akitangaza mali anayonunua akiendelea kuhudumu na kuitangaza akiacha kazi.