Habari za Kitaifa

Shida ya Wakenya si njaa tena, utafiti wa TIFA waonyesha

May 2nd, 2024 2 min read

NA STEVE OTIENO

UTAFITI wa Kampuni ya TIFA uliotolewa Alhamisi umeonyesha kuwa Wakenya hawashughulishwi tena na bei ya unga na mafuta.

Masuala yanayowakera zaidi sasa ni ufisadi unaohusishwa na mbolea feki, mvua kubwa inayoendelea kunyesha, mafuriko na ajali nyingi za barabarani pamoja na mgomo wa madaktari ambao umeingia mwezi wa pili.

Kwa mujibu wa utafiti wa Tifa uliofanyika Aprili 27-Aprili 29, asilimia 53 za Wakenya wamemlaumu Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kutokana na sakata ya mauzo ya mbolea feki.

Asilimia 82 ya Wakenya wanafahamu kuhusu mpango wa serikali wa kutoa mbolea ya bei nafuu, japo asilimia 55 wanasema kuwa mpango huo hauendelei vizuri.

Dhana hasi kuhusu mpango wa kuwauzia wakulima mbolea kwa bei nafuu ipo sana miongoni mwa wakazi wa Pwani na Kusini mwa Bonde la Ufa kwa asilimia 70 na 67 mtawalia.

Asilimia 47 na 43 mtawalia wa wakazi wa Kati mwa Bonde la Ufa na maeneo ya Kaskazini nao walisema kuwa mpango huo haufanyi kazi vizuri.

Kampuni ya kutengeneza mbolea KEL Chemicals, Shirika la Ukadiriaji wa Ubora wa Bidhaa, Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao na Wizara ya Kilimo, ndizo zililaumiwa kutokana na mbolea kutokuwa kwenye ubora unaohitajika.

Katika utafiti huo, Wakenya hawashughulishwi tena na bei ya mafuta na unga kutokana na kushuka kwa gharama ya kuzinunua. Wanahisi kuwa mbolea feki itaathiri sekta ya uzalishaji wa chakula na kuleta njaa ndiposa wanamakinikia suala la mbolea feki.

Mgomo wa madaktari pia umewashughulisha Wakenya kutokana na vifo vinavyotokea kwa sababu ya kukosekana kwa huduma za matibabu.

Wakazi wa Magharibi ndio wameathirika sana kutokana na mgomo wa madaktari kwa asilimia 61 huku Nairobi na Nyanza zikifuata kwa asilimia 59. Mashariki imeathrika kwa asilimia 56, Pwani (55), Kati mwa Bonde la Ufa (46) huku Kusini mwa Bonde la Ufa na Kaskazini zikiwa na asilimia 43.

Asilimia 54 za Wakenya hawaungi mkono mgomo wa madaktari, asilimia 23 wakiunga sana huku asilimia 19 wakiunga kidogo.

Upinzani zaidi kwa mgomo wa madaktari upo juu sana Kusini mwa Bonde la Ufa kwa asilimia 64 na asilimia 62 katika Mashariki ya chini.

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ndiye analaumiwa zaidi kwa mgomo wa madaktari kwa asilimia 48, Muungano wa Madaktari kwa asilimia 28, serikali za kaunti asilimia nane, Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma kwa asilimia tano na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei kwa asilimia moja.

Asilimia 78 ya Wakenya wanaamini kuwa kumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani. Nairobi inaongoza kwa asilimia 86 huku Mashariki ya chini kwa asilimia 84.

Ni asilimia 15 ya Wakenya ndio wanaamini ajali zimepungua huku asilimia nne wakiamini mambo yamesalia yale yale.

Kuhusu mafuriko, asilimia 56 ya wakazi wa Nairobi wameathirika, Kaskazini Mashariki (56) na Mashariki ya Chini (53). Kwa jumla asilimia 32 ya Wakenya wameathirika kutokana na mafuriko huku asilimia 32 wakisema hawajaathirika.