Farouk Shikhalo asajiliwa na KMC ya Tanzania

Farouk Shikhalo asajiliwa na KMC ya Tanzania

Na ABDULRAHMAN SHERIFF akiwa DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA golikipa wa Young Africans FC, Farouk Shikhalo amethibitisha kusajiliwa na timu ya Kinondoni Municipal Council (KMC) kwa kipindi cha msimu mmoja lakini ameeleza uwezekano wa kurudi kuichezea Bandari FC ya nchini Kenya.

Akiohojiwa na Taifa Leo, Shikhalo aliyetemwa na Yanga alithibitisha kusajiliwa na klabu nyingine ya Ligi Kuu ya Tanzania ya Vodacom ya KMC kwa msimu mmoja lakini anasema Bandari ni nyumbani kwake anaweza wakati wowote akarudi kuichezea tena.

“Nipo KMC kwa mwaka mmoja ila Bandari ni nyumbani na naamini ipo siku nitarudi,” akasema Shikhalo alipoulizwa uwezekano wa kurudi timu yake hiyo ambayo aliichezea kabla ya kusajiliwa na Yanga.

Alisema amefurahia kufahamu kuwa mashabiki kadhaa wa soka Pwani ya Kenya wamewataka maafisa wa Bandari FC wamsake na kumasajili yeye baada ya kufahamu kuwa alitemwa na Yanga.

“Nafurahi kufahamu mashabiki wa Bandari wangali wanakumbuka nilivyoitumika timu hiyo lakini ni vile tayari msimu huu nimesajiliwa na KMC. Lakini iko siku nitarudi kuichezea tena timu ya nyumbani ya Bandari,” akasema Shikhalo.

Mashabiki hao wa Bandari walisema Shikhalo amekuwa kipa aliyeichezea kwa moyo wake wote na kutokana na ubora alionao hadi wakati huu, wanataka arudi kuihudumia timu hiyo.

“Shikhalo amekuwa kwetu kwa miaka kadhaa na alisajiliwa Yanga baada ya kuonekana akituchezea sisi Bandari. Sasa ni wakati mwafaka kwa maofisa wa Bandari kumrudisha timuni kwani angali ni kipa mzuri sana,” akasema mmoja wa mashabiki wake.

Waliomba Bodi ya Bandari FC warudishwe timuni kwani wanadai aliweza kuisaidia timu kufanya vizuri katika ligi kuu mbali na kuwa miongoni mwa wachezaji walioichezea kwenye dimba la Caf Confederation Cup.

Mashabiki hao wanaamini Bandari kuihitaji kipa mwengine wa tatu na kwa kuwa Shikalo hakuondoka kwa ubaya aliposajiliwa na Yanga, itakuwa vizuri arudishwe timu yake apate kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri zaidi ligi ya msimu ujao.

You can share this post!

Kero ya stima kupotea bila notisi Zimmerman

ONYANGO: Makamishna wa IEBC wasisimamie zaidi ya uchaguzi...