Habari za Kitaifa

Shilingi moja: Serikali yawapa Wakenya afueni katika bei za hivi punde za mafuta

February 14th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imetoa afueni kidogo kwa Wakenya kwa kushusha bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa Sh1 kwa lita kulingana na bei mpya iliyotangaza Jumatano jioni.

Kulingana na bei hizo zilizotolewa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) petroli, dizeli na mafuta taa zitauzwa kwa Sh206.36, Sh195.47, Sh193.23, mtawalia jijini Nairobi na viunga vyake.

Bei hizo za rejareja zitatumika kuanzia Februari 15, 2024 hadi Machi 14, 2024, kabla ya saa sita za usiku.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Kiptoo alieleza kuwa bei hizo mpya zinajumuisha ushuru wa VAT wa kima cha asilimia 16 kulingana na hitaji la Sheria ya Fedha ya 2023, Sheria ya Ushuru (iliyofanyiwa mabadiliko) ya 2020 na aina viwango vingine vya ushuru.

“Kulingana na Sehemu ya 101 (Y) ya Sheria ya Mafuta ya 2019 na Notisi ya Kisheria Nambari 192 ya 2022, Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) imekadiria bei ya bidhaa hizo ambayo zitatumika kuanzia Februari 15, 2024 hadi Machi 14, 2024,” Dkt Kiptoo akasema kwenye taarifa hiyo.

“Ndani ya kipindi hicho, bei ya petroli, dizeli na mafuta zitapungua kwa Sh1 kwa lita, mtawalia,” akaongeza.

Huu ni mwezi wa tatu mfululizo kwa serikali kupunguza bei ya bidhaa hizo muhimu zaidi kwa uchumi wa nchi.

Mnamo Januari 14, 2024, EPRA ilipunguza bei ya petroli na dizeli kwa Sh5 kwa lita huku ikishusha bei ya mafuta kwa Sh4.82.

Kufuatia punguzo hilo petroli imekuwa ikiuzwa kwa Sh207.36 kwa lita jijini Nairobi, dizeli ikiuzwa kwa Sh196.47 na mafuta taa kwa Sh194.23.

Hata hivyo, mapema mwaka huu, kiongozi wa Azimio Raila Odinga aliitaka serikali kupunguza bei ya mafuta kwa kati ya Sh45 na Sh50 kwa lita kwa misingi ya kupungua “kwa kiwango kikubwa” kwa bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.