Makala

SHINA LA UHAI: Baridi ilivyo hatari kwa watoto

November 12th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

CHUNGA mtoto wako asiathiriwe na baridi kali iwapo unataka akue vyema.

Wataalamu wa afya bora wanasema kuwa watoto wanafaa kukingwa na baridi kali kwa sababu ni hatari sana kwa afya yao.

Wanasema kwamba baridi inaathiri afya ya watoto na kufanya miili yao kuwa dhaifu.

Kulingana na Dkt Tessy Kamau, mtaalamu wa afya ya watoto katika kituo cha afya cha Mother Ippolita, Nairobi, baridi inasababishia watoto matatizo ya kiafya.

Anasema wazazi wanafaa kuhakikisha kwamba watoto hawapigwi na baridi hasa wakati wa asubuhi wanapoenda shule na jioni.

“Baridi inaweza kufanya kinga ya mwili wa mtoto kupungua. Kinga ikipungua, mwili huwa hauna nguvu ya kukabiliana na maradhi. Hivyo, ni muhimu kwa wazazi kulinda watoto wao na baridi kali,” asema.

Dkt Kamau asema ili kuepuka hali hii, wazazi wanafaa kuwaandaa watoto wao ipasavyo kila asubuhi kulingana na hali ya hewa.

“Wazazi wanafaa kuwaandaa watoto wao ipasavyo ili wasisumbuliwe na maradhi yanayowavamia msimu wa baridi.

Anataja maradhi yafuatayo kama yanayoathiri watoto msimu wa baridi:

1. Watoto wanaweza kuugua niumonia. Ugonjwa huu ni hatari na unaweza kuwaua watoto.

2. Mzio unaosababisha mafua na homa kali.

3. Baridi pia huathiri ngozi na kusababisha maumivu.

4.Baridi inapunguza kinga ya mfumo wa mwili na kuufanya uvamiwe na viini vinavyosababisha maradhi.

5.Maumivu ya kifuani miongoni kwa matatizo mengine.

6.Baridi kali inaweza kusababisha mtoto kutokwa na damu puani.

7. Hypothermia: Hii ni hali ambayo hutokea kiwango cha joto mwilini kinaposhuka zaidi ya kile cha kawaida kwa sababu ya baridi kali mtoto akicheza nje bila kuvalia mavazi yanayofaa.

Dalili za hypothermia ni kutetemeka na kugugumiza.

Wataalamu wa afya wanashauri wazazi kuwakimbiza watoto wao hospitalini wakiwa na dalili hizi.

8.Jadili (Frostbite): Hali hii hutokea ngozi na tishiu za nje za mwili zinapoganda. Wataalamu wanasema hali hii inaathiri hasa vidole, masikio na pua. Mtoto anaweza kulalamika kuwa ngozi yake inawasha au kuganda akipatwa na hali hii.

Wataalamu wanaonya wazazi dhidi ya kusugua sehemu ya mwili wa mtoto iliyoathiriwa na jadili. “ Baada ya dakika chache, mkaushe mtoto kisha mfunike kwa nguo au blanketi apate joto. Unaweza kumpatia kinywaji chenye joto pia,” asema Dkt Kamau.

9. Flu: Msimu wa baridi watoto wanaweza kuambukizwa flu

10: Msimu wa baridi, watoto wanaweza kupata matatizo ya kupumua

Sehemu iliyoathirika ikiendelea kuganda kwa zaidi ya dakika tano, wataalamu wanashauri mtoto apelekwe kwa daktari.

Ingawa wazazi wengi huamini kwamba wanaweza kukinga watoto wao na baridi kwa kuwavalisha mavazi ya kuongeza joto pekee, wataalamu wa afya wanasisitiza kwamba watoto wanafaa kupatiwa lishe bora.

Wanasema hii itahakikisha kwamba kinga ya miili yao ni dhabiti. Wanasema mwili ulio na afya unaweza kuhimili maradhi yanayosababishwa na baridi sawa na yanayosababishwa na viini.

“Japo kumvalisha mtoto mavazi yaliyo na joto kunaweza kumkinga dhidi ya madhara ya baridi kali ni vyema mzazi kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata vyakula vinavyoongeza joto mwilini.

Ni vigumu kwa mwili ulio na afya kukabiliwa na maradhi na unahimili baridi,” asema Dkt Kamau.

Baadhi ya vyakula ambavyo wazazi wanafaa kuwalisha watoto wao ni vilivyo na vitamini na madini. Wataalamu wanaorodhesha matunda na vyakula kama Mayai, Karoti, Viazi vitamu na Nyanya kama vinavyoongeza joto katika mwili.

Ili kumkinga mtoto na baridi wazazi wanashauriwa kuhakikisha yafuatayo:

1. Watoto hawachezi hadharani wakati wa baridi kali. Dkt Kamau asema walimu wamefunzwa jinsi ya kuwakinga watoto na baridi wakiwa shule na wazazi wanafaa kuwalinda wakiwa nyumbani.

2. Watoto hawaogi na maji baridi. Wataalamu wanasema kufanya hivi ni kuhatarisha maisha ya watoto.

3. Watoto wavalishwe mavazi na glovu zilizo na joto. Wataalamu wanasema kichwa na mikono huathiriwa na baridi kama viungo vingine na watoto wanafaa kuvalishwa kofia msimu wa baridi.

4. Watoto wasicheze maeneo yaliyo na unyevunyevu.

Tafiti za kiafya zinaonyesha kuwa miili ya watoto huwa inapoteza kati ya asilimia 50 na 60 ya joto kupitia kichwa na mikono viungo ambavyo wazazi hupuuza wanapowanunulia watoto wao mavazi ya kujikinga na baridi.

Dkt Kamau anaeleza kwamba nyakati za jioni na usiku ambazo huwa na baridi baada ya jua kutua ni hatari kwa watoto.

“Mzazi anafaa kumwandaa mtoto wake vilivyo nyakati za jioni na usiku kwa kumvalisha mavazi yaliyo na joto,” asema na kuongeza kuwa maradhi mengi yanayowapata watoto kutokana na baridi yanaweza kuepukwa.

Wataalamu wanasema baridi kali inaweza kuathiri macho ya mtoto hasa baridi hiyo ikiandamana na upepo.

Mavazi yasiwe ya kuwabana watoto

Wanasema mavazi ya kuwakinga watoto msimu wa baridi hayafai kuwabana kama wanavyoamini baadhi ya wazazi. Wanasema mavazi yaliyobana mwili wa mtoto humtatiza anapotembea.

Wakati wa mvua ni hatari sana kwa watoto na wataalamu wa afya wanasema wazazi wanapaswa kuwavalisha watoto wao mavazi yasiyopenyeza maji.

“Hakikisha ya kwamba mavazi wanayovalia watoto msimu wa mvua hayapenyezi maji na kwamba wanayavua wakifika nyumbani ikiwa wamenyeshewa wakiwa njiani kutoka shule. Ubaridi katika mavazi pia ni hatari kwa mwili wa mtoto,” aeleza Bi Wanjku.

Mavazi ya kuvalia msimu wa baridi pia yanafaa kushonwa kwa vitambaa vinavyohifadhi joto.

Kulingana na tovuti ya www.kidsource.com mbali na kichwa, mikono na uso, shingo ya mtoto inafaa kukingwa dhidi ya baridi. Tovuti hiyo inasema kwamba wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao wanapocheza msimu wa baridi ili kuhakikisha usalama wao.

Wataalamu wanasema wazazi wanafaa kujiandaa mapema ili kusitiri watoto wao na baridi wakati wowote.

Wanashauri wazazi waweke vifaa vya kuongeza joto nyumbani na kwamba wahakikishe wanaepuka vifaa vinavyotoa gesi hatari nyumbani msimu wa baridi. Aidha, wanasema ni vyema watoto kufunzwa jinsi ya kujikinga na baridi wanapokua.