SHINA LA UHAI: Corona: Chanjo ya AstraZeneca ni salama?

SHINA LA UHAI: Corona: Chanjo ya AstraZeneca ni salama?

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI huenda ikakosa kuafikia lengo lake la kutoa chanjo kwa watu milioni 1.2 ndani ya miezi miwili ijayo kutokana na idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupewa kinga hiyo.

Wataalamu wanasema kuwa idadi ndogo ya wanaojitokeza kupewa chanjo hiyo humu nchini imechangiwa na kuwepo kwa ripoti za kutilia shaka usalama wake na serikali kukosa kuhamasisha Wakenya.

Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi nchini tawi la Mombasa Peter Maroko, anasema kuwa hajahiari kudungwa chanjo hiyo baada ya usalama wake kutiliwa shaka na mataifa ya Ulaya.

“Baadhi ya nchi zimesitisha utoaji wa chanjo ya AstraZeneca baada ya kuhusishwa na ugandaji wa damu mwilini. Madhara ya chanjo hii hayajabainika vyema na utafiti zaidi unahitajika,” anasema.

Bw Maroko ni miongoni mwa maelfu ya wahudumu wa afya ambao hawajajitokeza kuchanjwa wakitilia shaka usalama wake.

Chini ya wahudumu wa afya 500 walikuwa wamechanjwa katika Kaunti ya Mombasa kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita. Mombasa ilipokea dozi 9,000 kwa ajili ya wahudumu wa afya.

Kati ya wahudumu wa afya 3,000 wanaolengwa katika Kaunti ya Taita Taveta, waliodungwa ni chini ya 200.

Kulingana na katibu mkuu wa wahudumu wa kliniki katika Kaunti hiyo, Reinherd Myeuok, wahudumu wa afya wanajikokota kuchanjwa kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusiana na umuhimu wake.

“Nimedungwa tayari, lakini sijui lolote kuhusiana na chanjo hii. Ikiwa mimi sina ufahamu wa kutosha inawezekanaje kwa Wakenya ambao hawajasomea taaluma ya utabibu kuelewa? Wizara ya Afya imeshindwa kuelimisha Wakenya kuhusu chanjo hii,” anasema.

Takribani mataifa 13 ya Ulaya, yakiwemo Ujerumani, Italia, Ufaransa na Uhispania, yalisitisha kwa muda utoaji wa chanjo ya AstraZeneca baada ya kubainika kuwa baadhi ya watu waliodungwa walipata matatizo ya kuganda kwa damu mwilini.

Kulingana na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa Ulaya-EMA, kufikia Machi 10, 2021, takribani visa 37 vya damu kuganda mwilini miongoni mwa watu milioni 5 waliopewa chanjo hiyo inayotumiwa humu nchini, vilikuwa vimeripotiwa katika mataifa mbalimbali ya Ulaya.

Kati yao, watu tisa wamefariki baada ya damu kuganda kwenye mishipa inayoisafirisha kwenye ubongo na sehemu nyinginezo za mwili. Visa vingi vya damu kuganda vimeripotiwa miongoni mwa wanawake – hali ambayo imezua maswali zaidi.

Visa vya damu kuganda mwilini hutokea kwa mtu mmoja kati ya 1,000 kila mwaka hasa miongoni mwa wazee, wanaougua aina fulani za kansa, wajawazito au kwa wanaotumia muda mrefu wakiwa wameketi bila kutembeatembea.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea wasiwasi wake kuwa hatua hiyo ya mataifa ya Ulaya itasababisha idadi kubwa ya watu humu nchini na nchi nyingine za Afrika kususia chanjo ya AstraZeneca.

Kwa mfano, hatua ya mataifa ya Ulaya kutilia shaka usalama wa chanjo hiyo imesababisha nchi za Cameroon na Demokrasia ya Jamhuri ya Congo (DRC) kusitisha kwa muda utoaji wa chanjo hiyo hata kabla ya kushuhudia kisa chochote cha kuganda kwa damu.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu nchini Dkt Patrick Amoth anasema kuwa Kenya itaendelea kutoa chanjo ya AstraZeneca.

“Shirika la WHO limesema kuwa faida ya chanjo ya AstraZeneca ni kubwa kuliko madhara yake. Hivyo, hatutasitisha shughuli ya utoaji wa chanjo,” anasema.

Kauli ya Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi, aliyotoa Ijumaa wiki iliyopita kwamba chanjo haizuii mtu kuambukizwa virusi vya corona pia imeibua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya Wakenya wakihoji umuhimu wa kudungwa.

Dkt Mwangangi alifafanua kuwa chanjo haifanyi mtu kutoambukizwa corona.

“Chanjo inasaidia kusisimua kingamwili ili ziweze kupigana na virusi vya corona vinapoingia mwilini,” akafafanua Dkt Mwangangi.

Lakini wengi wa Wakenya walionekana kufasili vibaya kauli hiyo huku baadhi yao wakishikilia kuwa hakuna haja ya kudungwa chanjo hiyo.

“Kama hiyo chanjo haizuii virusi vya corona, mbona nivumilie uchungu wa sindano na haina faida kwangu?” akauliza Jared Juma kupitia mtandao wa Twitter.

Naye, Salim Abebe alisema; “mbona tunatumia mabilioni ya fedha kununua chanjo ambayo haizuii virusi vya corona kuingia mwilini? Tutumie hela hizo kujenga hospitali na shule.”

Wataalamu wanasema kuwa maswali kama hayo ni ishara kwamba wizara ya Afya haijahamasisha umma ipasavyo kuhusiana na chanjo ya corona.

Shirika la WHO linaafikiana na Dkt Mwangangi kwamba chanjo haizuii virusi hivyo kuingia mwilini na badala yake, inafunza mwili jinsi ya kutambua na kupigana navyo vinapoingia mwili hivyo kumfanya mtu kutokuwa mgonjwa.

“Mwili wa mtu ambaye hajadungwa chanjo unaweza kulemewa kwa urahisi na makali ya corona. Lakini chanjo itapunguza idadi ya watu wanaolazwa hospitalini au kufariki kutokana na maradhi haya,” linasema WHO.

Kuganda kwa damu

WHO na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa Ulaya (EMA) mnamo Alhamisi iliyopita, zilisema kuwa chanjo ya AstraZeneca ni salama licha ya kuwepo kwa visa vichache vya damu kuganda mwilini.

EMA ilisema kwamba zaidi ya watu milioni 20 wamepewa chanjo ya AstraZeneca ilhali ni visa 37 tu vya damu kuganda mwilini ambavyo vimeripotiwa.

“Hiyo ni ithibati kwamba chanjo ni salama na inafaa kuendelea kutumika,” ikasema mamlaka hiyo.

Nchi za Ujerumani, Uhispania, Ufaransa, na Italia tayari zimetangaza kuwa zitaendelea na shughuli ya kutoa chanjo hiyo kwa raia wake kuanzia Ijumaa baada ya kuhakikishiwa na EMA kuwa ni salama.

Norway ambayo imethibitisha visa vya damu kuganda, akiwemo mmoja aliyefariki, pia imesema kuwa itaanza kuitoa tena.

Wataalamu nchini humo walisema kuwa kuna uwezekano kwamba kingamwili za waathiriwa zilipingana na chanjo hiyo hivyo kusababisha damu kuganda mwilini.

Damu inapoganda kwenye mishipa husababisha oksijeni kukosa kufikia ubongo na sehemu nyinginezo za mwili na mwathiriwa anaweza kufariki.

WHO linasema kuwa kuganda kwa damu mwilini kunaweza kuwa ishara kwamba waathiriwa walikuwa na maradhi mengine mwilini.

“Chanjo dhidi ya virusi vya corona haiondoi maradhi mengine mwilini au kuzuia vifo vinavyotokana na magonjwa mengineyo,” likasema kupitia taarifa yake iliyotolewa Machi 17, 2021.

“Matatizo ya damu kuganda mwilini yamekuwepo kwa muda mrefu. Tatizo hilo ndilo huchangia karibu theluthi moja ya maradhi ya moyo kote duniani. Japo tunaendelea na uchunguzi kubaini kiini cha damu kuganda miongoni mwa watu wachache, ni bayana kwamba faida za AstraZeneca ni kubwa kuliko madhara yake,” likaongezea.

Visa vya kuganda kwa damu kwenye mishipa vimekuwa vikihusishwa na wanawake ambao wamekuwa wakitumia aina fulani ya vidonge vya kuzuia ujauzito.

WHO na EMA zimeanza kutafiti kuthibitisha ikiwa tatizo la damu kuganda lina uhusiano na matumizi ya vikinga mimba.

Mwenyekiti wa Jopokazi la Kusimamia Chanjo nchini Dkt Willis Akhwale, anasema kuwa kati ya Wakenya zaidi ya 30,000 ambao wamedungwa chanjo, wizara ya Afya haijapokea kisa chochote cha damu kuganda.

“Bodi ya Kudhibiti Dawa na Sumu (PPB) imepokea ripoti karibu 50 za watu waliodungwa chanjo kupatwa na matatizo ya kiafya kwa muda mfupi kama vile kuumwa na kichwa na misuli pamoja na kuhisi joto. Hayo ni matatizo ya kawaida na hayahitaji kufanyiwa uchunguzi,” anasema.

“Wakenya ambao wamedungwa chanjo wanafaa kuripoti matatizo yoyote ya kiafya yanayotokea baadaye ili wizara ya Afya iweze kuyafanyia uchunguzi,” asisitiza Dkt Akhwale.

Kwa sasa, uchunguzi uliofanywa nchini Amerika na ripoti yake kutolewa jana Machi 21, 2021, unaonyesha kwamba chanjo ya AstraZeneca ina uwezo wa kuzuia waathiriwa kupatwa na dalili za corona kwa asilimia 79.

Chanjo hiyo inazuia watu wanaoambukizwa virusi vya corona kulazwa hospitalini kwa asilimia 100.

Hiyo inamaanisha kwamba iwapo Wakenya wote watapewa chanjo hiyo, idadi ya watu watakaolazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) kutokana na maradhi ya corona itakuwa sufuri.

Uchunguzi huo uliofanywa na kamati huru ambayo pia ilichunguza visa vya kuganda kwa damu miongoni mwa baadhi ya watu ambao walipewa chanjo hiyo.

Kati ya watu 21, 500 waliohusishwa katika utafiti huo, hakuna hata mmoja aliyepatikana na kisa cha kuganda kwa damu kwenye mishipa ya ubongo au sehemu yoyote ya mwili, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Kamati hiyo iliyiongozwa na Profesa Ann Falsey wa Chuo Kikuu cha Matibabu cha Rochester, Amerika, ilisema kuwa matokeo ya utafiti wao yamedhihirisha kuwa chanjo ya AstraZeneca ni salama na inafaa kutumika katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

Patson Daka: Fowadi matata wa Zambia anayenyima miamba wa...

VISABABISHI: Tatizo la damu kuganda mwilini si jambo geni...