Makala

SHINA LA UHAI: Covid-19 tishio kwa sekta ya afya duniani

May 26th, 2020 5 min read

Na LEONARD ONYANGO

JANE Atieno (si jina lake halisi) wiki iliyopita alizuru kituo kimoja cha afya katika Kaunti ya Homa Bay, baada ya kuhisi maumivu ya kichwa na joto jingi mwilini.

Baada ya kuwaelezea wahudumu wa afya kuwa alihisi maumivu ya kichwa na joto jingi mwilini, walimshauri aende akapimwe virusi vya corona hata kabla ya kumhudumia.

“Walikataa kunitibu labda kutokana na hofu kwamba ningewaambukiza virusi vya corona,” anasema Bi Atieno ambaye ni mama ya watoto wawili.

“Nilirudi nyumbani nikanunua dawa na sasa nimepona. Sijui ikiwa nina virusi vya corona lakini sitaenda kupimwa sababu sitaki kupelekwa karantini na kuwaacha watoto wangu bila mwangalizi,” anasimulia.

Sawa na Bi Atieno, idadi kubwa ya Wakenya ‘wamesusia’ kwenda hosptalini kutokana na hofu ya kuambukizwa virusi vya corona.

Huku wagonjwa wakikwepa kupimwa, wahudumu katika vituo mbalimbali vya afya pia wanahofia kuambukizwa virusi hivyo kutoka kwa wagonjwa.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, alipokuwa akizungumza katika Kaunti ya Machakos Alhamisi iliyopita alikiri kuwa idadi kubwa ya Wakenya sasa hawaendi hospitalini kutokana na hofu ya kupata corona.

“Kuna hospitali spesheli ambazo zimetengwa kwa ajili ya kushughulikia waathiriwa wa virusi vya corona katika kila Kaunti. Huduma za matibabu zinaendelea kama kawaida katika hospitali nyinginezo zilizosalia,” akasema Bw Kagwe.

Miezi miwili iliyopita, waziri Kagwe alidai kuwa kupungua kwa idadi ya watu wanaoenda hospitalini kutafuta huduma za matibabu ilikuwa ishara kwamba magonjwa kama vile kuhara na maradhi mengineyo ambayo husababishwa na uchafu yamepungua kwa sababu ya kuosha mikono mara kwa mara kama njia mojawapo ya kujikinga na Covid-19.

Baadhi ya Wakenya waliozungumza na jarida la Afya Jamii walisema kuwa wanahofia kupelekwa karantini iwapo watapatikana na dalili za corona.

Baadhi ya wagonjwa sasa wananunua dawa madukani na hata kutumia dawa za mitishamba wanapokuwa wagonjwa.

Jane Waithaka, ambaye ni muuzaji wa mboga katika mtaa wa Zimmerman, jijini Nairobi anasema kuwa hajawahi kwenda hospitalini tangu kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipothibitishwa humu nchini miezi mitatu iliyopita.

“Binti yangu wa umri wa miaka sita alikuwa na joto jingi mwilini wiki iliyopita. Nilinunua dawa dukani nikampa na sasa amepata nafuu. Siwezi kumpeleka hospitalini kwani sitaki amepelekwe karantini,” anasema Bi Waithaka.

Naye Philip Kimwere, anayefanya kazi ya ujenzi jijini Nairobi anasema kuwa janga la corona limemsababishia hofu kiasi kwamba anahisi dalili za ugonjwa huo mara kwa mara ila hospitalini hakanyagi ng’o!

“Ninapendelea kununua dawa dukani badala ya kwenda hospitalini. Daktari anayekuhudumia anaweza kuwa na virusi hivi kwani anatibu watu wengi,” anasema Bw Kimwere.

Wahudumu wa afya, hasa katika hospitali nyingi zinazosimamiwa na kaunti wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa na mavazi ya kuwakinga (al-maarufu PPE) dhidi ya kuambukizwa corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt Patrick Amoth, mnamo Mei 13, alisema kuwa wahudumu wa afya 33 tayari wameambukizwa Covid-19.

Hospitali za umma na za kibinafsi kote nchini zimeripoti kupungua kwa idadi ya watu wanaofika kutafuta huduma za matibabu yasiyohusiana na corona.

Chama cha Wamiliki wa Hospitali za Kibinafsi (KAPH) kinasema kuwa watu hawaendi hospitalini kutibiwa kutokana na hofu ya kuambukizwa maradhi haya.

“Idadi ya watu wanaofika hospitalini kutafuta huduma za matibabu imepungua zaidi. Hali hiyo imeathiri mapato ya hospitali. Watu wanaokuja hospitalini ni wale walio wagonjwa zaidi,” anasema Katibu Mkuu wa KAPH Timothy Olweny.

Ripoti ya kura ya maoni iliyofanywa na TIFA katika majiji ya Mombasa na Nairobi, hata hivyo ilisema kuwa ni asilimia 2 pekee ya wakazi wa maeneo hayo wanaoamini kuwa wanaweza kuambukizwa corona wakienda hospitalini.

Kulingana na ripoti ya TIFA, idadi kubwa ya wakazi wa Nairobi na Mombasa wanaamini kuwa wanaweza kuambukizwa wakizuru maeneo yenye msongamano wa watu kama vile masoko na matatu.

Lakini uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Coast General jijini Mombasa, idadi ya watu wanaoenda kutafuta huduma za matibabu imepungua kwa kiasi kikubwa.

Waathiriwa zaidi ya 40 wa corona wanatibiwa katika wadi maalumu hospitalini hapo.

Aidha matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) yaliyotolewa wiki iliyopita yanaonyesha kuwa ni asilimia 12.4 ya familia nchini zilizopeleka jamaa zao hospitalini kwa ajili ya huduma za matibabu yasiyohusiana na corona tangu Februari 2020.

Mwezi uliopita, Gavana wa Isiolo Mohamed Kuti alisema kuwa serikali za kaunti zimeanza juhudi za kutenganisha wadi za waathiriwa wa corona na wagonjwa wa maradhi mengineyo.

Alisema hatua hiyo itawaondolea watu hofu hivyo kujitokeza kutibiwa.

Huduma zilizoathirika hospitalini

• HIV

Miongoni mwa wanaokwepa kwenda hospitalini ni waathiriwa wa HIV ambao hawajakuwa wakijitokeza kuchukua dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo (ARVs).

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa vifo 500,000 zaidi vinavyotokana na Ukimwi huenda vikashuhudiwa kote ulimwenguni kutokana na hatua ya waathiriwa kutoenda hospitalini kuchukua ARVs kwa kuhofia maambukizi ya corona.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 1.1 hufariki kutokana na maradhi yanayohusiana na Ukimwi kote duniani. Hiyo inamaanisha kuwa janga la Covid-19 huenda likasababisha idadi ya vifo vinavyotokana na Ukimwi kufikia milioni 1.6.

Takwimu za Baraza la Kudhibiti Maradhi ya Ukimwi (NACC) zinaonyesha kuwa kati ya watu 15,400 – 39,000 hufariki kila mwaka kutokana na maradhi yanayohusiana na Ukimwi humu nchini.

Kwa kuzingatia makadirio hayo ya WHO, kuna hofu kuwa idadi ya vifo vinavyohusiana na Ukimwi huenda ikaongezeka.

Baraza la NACC linakadiria kuwa jumla ya watu milioni 1.5 humu nchini wanaishi na virusi vya HIV. Kati yao, asilimia 75 wanatumia ARVs zinazopunguza makali ya virusi hivyo.

Takribani watu 52,800 huambukizwa virusi vya HIV kila mwaka.

Lakini shirika la WHO linakadiria kuwa huenda idadi ya maambukizi ya HIV ikaenda juu na maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa mama hadi kwa mtoto yakaongezeka wakati huu wa janga la virusi vya corona.

• Upangaji uzazi

Idadi ya watu wanaoenda hospitalini kutafuta huduma za upangaji uzazi pia imepungua katika hospitali za umma na kibinafsi kote nchini.

Mbali na hofu kwamba huenda wakaambukizwa virusi vya corona, kuna uwezekano kwamba mwongozo wa serikali ambao umesitisha baadhi ya huduma za upangaji uzazi pia umechangia kwa watu wachache kujitokeza.

Kulingana na mwongozo wa Wizara ya Afya uliotolewa mwezi uliopita, njia za kupanga uzazi zinazoshauriwa wakati huu wa janga la corona ni matumizi ya kondomu na tembe zinazotumiwa kwa muda wa miezi mitatu na zaidi.

“Aina nyinginezo za kupanga uzazi haswa zinazohusisha upasuaji zimesitishwa hospitalini hadi pale hali itakapokuwa shwari,” unasema mwongozo huo uliotolewa na Dkt Amoth.

Kulingana na ripoti ya Hali ya Uchumi ya 2020 iliyotolewa na shirika la KNBS, wanawake 1,879,317 walienda hospitalini mwaka 2019 kudungwa sindano yenye homoni za kuzuia ujauzito kwa angalau miezi 12. Wanawake 174,142 waliwekewa kifaa cha IUCD katika mfuko wa uzazi. Kifaa hicho cha IUCD kinaweza kuondolewa na kumwezesha mwanamke kuendelea kupata mimba.

Wanawake 514,213 walipanga uzazi kwa kutumia teknolojia inayojulikana kama Implants Insertion. Kwa kutumia teknolojia hiyo, kifaa kinacholingana na kijiti cha kiberiti huwekwa ndani ya ngozi ya mkono kwa lengo la kuzuia ujauzito.

• Ujauzito

Mwongozo wa Wizara ya Afya pia unasema kuwa wanawake wajawazito wanafaa kwenda kliniki mara tatu tu wakati huu wa janga la corona.

Wataalamu wanahofia kuwa janga hili huenda likaongeza idadi ya visa vya wanawake kujifungulia nyumbani hivyo kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.

Kati ya watoto 1,178,260 waliozaliwa mwaka jana, asilimia 96.7 walizaliwa hospitalini. Ni asilimia 3.3 ya watoto walizaliwa nyumbani.

• Malaria

Shirika la WHO tayari limetabiri kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na malaria vitaongezeka maradufu kutokana na janga la corona.

Visa vya malaria humu nchini viliongezeka kwa asilimia 18.6 hadi milioni 4.7 ikilinganishwa na 2018, kwa mujibu wa ripoti ya KNBS. Takribani watu 23,000 walifariki kutokana na malaria mwaka 2019.

WHO linatabiri kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na malaria humu nchini huenda ikafikia 46,000.

Kulingana nalo, dalili za malaria kama vile joto jingi na maumivu mwilini, zinafanana na zile za corona. Hivyo kuna uwezekano kwamba baadhi ya wagonjwa wa malaria wanaweza kufungiwa karantini wanapopatikana na joto jingi hivyo kukosa tiba na kuhatarisha maisha yao.

Kadhalika linahofia kuwa virusi vya corona huenda vikafanya mataifa yasifikie Malengo ya Maendeleo (SDG) kuhusu afya kufikia 2030.