Makala

SHINA LA UHAI: Hatari ya sumu ipo kila twendako sio kwenye chakula pekee

November 26th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

UNAJUA kwamba sumu inaweza kuingia katika mwili wako kupitia pumzi na miale hatari?

Wataalamu wanasema sio lazima mtu apate sumu mwilini kwa kuimeza pekee mbali inaweza kuingia mwilini kupitia njia mbali mbali.

Sumu ni kitu chochote kinachoweza kusababisha kifo au majeraha kupitia kemikali iliyoko ndani. Wataalamu wanasema kwamba ingawa sumu inaingia mwilini kupitia mdomoni mtu anaweza kuipata kupitia hewa, ngozi, sindano, miale au kuumwa na wanyama kama vile nyoka na wadudu.

“Watu wengi wanafahamu kwamba wanaweza kuathiriwa na sumu wanapoimeza au kupitia chakula. Ukweli ni kwamba mtu anaweza kupata sumu mwilini kupitia hewa au hata ngozi,” asema Dkt David Mwangi wa hospitali ya Bristol Park, Nairobi.

Anasema sumu ikiingia kwa mwili, inaweza kuua mtu iwapo hatua hazitachukuliwa haraka. Baadhi ya dalili za mtu anayeathiriwa na sumu ni:

  1. Kukumbwa na kichefuchefu
  2. Kutapika na kutokwa na povu mdomoni
  3. Maumivu hasa tumboni
  4. Matatizo ya kupumua
  5. Kuchanganyikiwa
  6. Kubadilika kwa rangi ya ngozi

Wataalamu wanasema kwamba mtu akinywa sumu hatari na akose kupatwa na dalili hizi, anapaswa kukimbizwa hospitali achunguzwe na madaktari.

“Sumu inaweza kuwa kemikali hatari ambazo hazifai kumezwa au kuguswa na binadamu zikiwemo rangi na sabuni. Hata hivyo, aina nyingi ya sumu huwa ni bidhaa zinazotumiwa na binadamu vikiwemo vyakula na dawa,” asema Dkt Mwangi.

Uyoga na maji

Kulingana tovuti ya www.emedicinehealth.com kuna aina za uyoga ambazo ni sumu, maji yanayochanganyika na kemikali zinazotumiwa kwa kilimo au viwandani pia huwa ni sumu.

Chakula

Aidha, wataalamu wanasema chakula kikikosa kupikwa vizuri au kushughulikiwa ipasavyo katika mazingira safi kinaweza kuwa sumu kwa mwili.

Dawa

Dawa zinazotumiwa kutibu maradhi tofauti zinaweza kuwa sumu zikitumiwa kwa njia isiyofaa kama kuzidisha kipimo ambacho mtu hushauriwa na daktari au kutumia dawa bila ushauri wa daktari.

Wataalamu wanasema kuwa dawa zikitumiwa visivyo (kuongea au kupunguza kipimo) zinaweza kusababisha maradhi ya moyo, hini na figo na kusababisha kifo.

Mbali na dalili zilizotajwa hapo juu, matabibu wanasema mtu anaweza kupata matatizo ya kuona, kupata kizunguzungu, midomo na ngozi kukauka, moyo kupiga kwa kasi au kasi ya mpigo wa moyo kupungua.

“Huwa ni rahisi kwa matabibu kuhudumia mgonjwa iwapo inajulikana aina ya sumu inayomsumbua. Ikiwa haijulikani, daktari hutumia dalili alizo nazo mgonjwa ili kufahamu matibabu ya kumpatia,” aeleza Dkt Cidy Wanja wa hospitali ya Scion jijini Nairobi.

Anasema mtu anaweza kumeza sumu hasa kupitia chakula na achukue muda wa saa, siku na hata miezi kabla ya dalili kutokea.

“Sumu za aina hii huwa hatari sana kwa sababu mtu anapoenda kupata matibabu, sumu huwa imeathiri viungo vingi vya mwili,” asema.

Wataalamu wanasema kuna baadhi ya magonjwa ambayo dalili zake zinafanana na za mtu aliyeathiriwa na sumu.

“Kwa mfano, kichefuchefu na kutapika ni dalili za mtu aliyeathiriwa na sumu. Hizi pia ni dalili za maradhi mengine ambayo hayasababishwi na sumu kama vile kiharusi, vidonda vya utumbo na matatizo ya nyongo miongoni mwa mengine,” asema Dkt Wanja.

Wataalamu wanaonya watu dhidi ya kununua dawa moja kwa moja bila ushauri wa daktari wanapohisi dalili za maradhi.

Dawa za kununua dukani, asema Dkt Wanja zinaweza kuwa sumu.

Kulingana daktari, mtu anayeshukiwa kuathiriwa na sumu anapaswa:

1. Kupelekwa hospitali akionekana kuwa mgonjwa kama vile kuwa mdhaifu na kuchanganyikiwa.

2. Mtoto akimeza sumu hata kama haonyeshi dalili za kudhurika.

3. Yeyote anayemeza chochote kwa lengo la kujidhuru hata kama anachomeza kinajulikana sio hatari.

Anashauri watu kubeba aina ya sumu au chupa yake iwe ni dawa, rangi, sabuni au hata dawa za kienyeji wanapompeleka muathiriwa hospitali.

Dkt Mwangi anasema hii itamsaidia daktari kuelezwa aina ya sumu na matibabu yanayoweza kumfaa mgonjwa.

Ikiwa aina ya sumu haijulikani, madaktari humpima kwanza kabla ya kuanza kumtibu.

Mtu wa familia au rafiki wa mwathiriwa wa sumu anaweza kumsaidia daktari kwa kumpatia maelezo yafuatayo.

1. Alichokula au kunywa mwathiriwa

2. Aina ya dawa ambazo alikuwa akitumia

3. Aina ya kemikali sehemu ya kazi au nyumbani

4. Kama kuna watu wengine wa familia au kazini walioathiriwa

5. Iwapo mwathiriwa ana historia ya matatizo yoyote ya kiakili yanayoweza kumfanya anywe sumu kwa lengo la kujitoa uhai.

Wataalamu wanaonya watu dhidi ya kuwatibu wanaoathiriwa na sumu nyumbani.

“Sumu ikiingia katika mwili wa binadamu inahitaji kushughulikiwa kitaalamu na matabibu na haiwezi kutibiwa nyumbani na mtu ambaye ana mafunzo ya udaktari.

Ili mgonjwa aweze kupona ni lazima apelekwe hospitali ili kuokoa maisha yake.

Kama huduma ya kwanza, wataalamu wanapendekeza yafuatayo:

1. Ondoa sumu iliyobaki mdomoni mwa mwathiriwa kama ipo. Soma maelezo katika kibandiko na ufuate maagizo kuhusu athari za aina ya sumu aliyomeza

2. Ikiwa ni ngozi iliyoathiria, ondoa mavazi yaliyoathiriwa ukiwa umevalia glavu. Safisha ngozi kwa dakika 15 hadi 20 kwa kutumia maji safi.

3. Sumu machoni; Osha macho kwa maji ya vuguvugu kwa dakika 15 hadi msaada upatikane.

4. Mtu akivuta hewa yenye sumu: Mtoe nje kwenye hewa safi haraka iwezekanavyo. Akitapika, mpindue kichwa alale kwa upande mmoja ili asisakamwe.

Wataalamu wanasema sumu inayotokana na chakula hutibiwa kutokana na hali ya mgonjwa japo kwa baadhi ya watu inaweza kuisha bila hata kupewa dawa.

Hata hivyo, madaktari wanasisitiza kuwa ni lazima mtu aende hospitali akiwa na dalili za kuathiriwa na sumu.

Kwa sababu ya kuhara na kutapika, inapendekezwa mgonjwa apatiwe maji kwa wingi na madini kama sodium, potassium na Calcium ambayo yanasaidia mwili kudumisha kiwango cha maji.

“Patia mgonjwa maji kwa wingi ikiwa anatapika na kuhara ili asiishiwe na maji mwilini hadi afike hospitali. Usinunue dawa dukani umpe mgonjwa bila ushauri wa daktari,” asema Dkt Wanja.