SHINA LA UHAI: Hili eneo, ujauzito ni sawa na kitanzi!

SHINA LA UHAI: Hili eneo, ujauzito ni sawa na kitanzi!

NA PAULINE ONGAJI

MWANAMKE yeyote yule ambaye amewahi kujifungua atakwambia kwamba uchungu wa uzazi ni mkali mno na haumithiliki.

Lakini sasa hebu tafakari kwamba katika hali hii inakubidi usubiri kwa saa kadhaa kabla ya kupata mbinu ya usafiri kwenda hospitalini, au hata ikiwa imepatikana bado hauna uhakika wa kufika hospitalini kwa wakati ufaao kutokana na mawimbi makali baharini.

Sio hayo tu, iwapo utabahatika kufika kwenye ufuo wa bara, huenda usifike hospitalini kwa muda ufaao kwani hakuna gari la kukupeleka hospitalini, au hata ukifika hospitalini, bado hauna uhakika wa kupokea matibabu kutokana na ukosefu wa vifaa.

Pengine miongoni mwa wengi huenda hii ni hadithi, lakini kwa wanawake wajawazito wa visiwa vya Ziwa Victoria, huo ndio uhalisi maisha.

Ni uhalisi ambao familia ya marehemu Letizia Achieng ilikumbana nao Machi baada ya mwanamke huyo kufariki katika harakati za kujifungua.

Marehemu Letizia alikumbana ghafla na mauti alfajiri ya Ijumaa Machi 25 akiwa na umri wa miaka 22 pekee.

Bi Letizia Achieng mkazi wa kisiwa cha Mfangano, katika Ziwa Victoria ambaye alipoteza maisha akisubiri kutibiwa alipoanza kuhisi uchungu wa uzazi. PICHA | HISANI

Masaibu ya marehemu Letizia yalianza Alhamisi ya Machi 24 ambapo alianza kukumbwa na uchungu wa uzazi.

“Wakati huo, mumewe Bw Calvin Okoth alikuwa amesafiri kwenda chuoni anakosomea ualimu,” aeleza binamu yake Bw Calvin, Bw Bernard Ogango.

Kulingana na Bw Ogango ambaye wakati huo alikuwa akiishi na marehemu katika ufuo wa Sena, Kisiwani Mfangano, kufikia saa kumi na mbili jioni walimpeleka Letizia katika kituo cha afya cha Sena.

Hapa ilibainika kwamba marehemu alikumbwa na shinikizo la damu ambapo waliagizwa kumpeleka katika hospitali ya kaunti ndogo ya Mbita, zaidi ya kilomita 100 kutoka kisiwani humo.

Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa boti la kumsafirisha kutoka kisiwani humo kumpelekea bara ya Mbita, walilazimika kusubiri hadi saa tatu na robo usiku kabla ya kuanza safari.

“Kisiwa hiki hakina ambulenzi ya boti, lakini kwa bahati nzuri tulifanikiwa kupata boti linaloendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Ekialo Kiona katika eneo hili, ambapo baada ya kununua mafuta tulianza safari,” aeleza Bw Ogango.

Baada ya kukumbana na mawimbi makali ya baharini, waliwasili kwenye ufuo wa bara saa saba za alfajiri.

“Masaibu yetu hayakukomea hapo kwani hata baada ya kufika, hatukuwa na mbinu ya usafiri kutoka ufuoni hadi hospitali ya kaunti ndogo ya Mbita, umbali wa kilomita mbili. Ilitubidi kumbeba mgonjwa wetu kwenye machela hadi hospitalini,” aeleza.

Baada ya kuwasili, mambo yalizidi kuwa mabaya kwani hospitali hiyo haikuwa na uwezo wa kukabiliana na hali ya marehemu ambaye kufikia wakati huo alikuwa amelemewa na maumivu na nguvu kumuishia.

“Ilibidi tuandikiwe barua ya kwenda katika hospitali ya rufaa ya Homa Bay. Lakini tena kukatokea mvutano kuhusu mbinu ya kumsafirisha mgonjwa ambapo tulikuwa tunalazimishwa kulipa Sh5000 za mafuta ya ambulenzi, pesa ambazo hatukuwa nazo,” aeleza.

Baada ya mvutano huu hatimaye mwendo wa saa kumi na mbili unusu asubuhi, familia hii iliruhusiwa kumuondoa mgonjwa wao pale.

“Tulifika katika Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay saa moja asubuhi na dakika kadhaa na hapa ndipo mgonjwa wetu alipoanza kupokea matibabu. Lakini hii ilikuwa baada ya kununua dawa na glavu zilizohitajika ili madaktari waanze kumshughulikia,” aongeza Bw Ogango.

Japo kufikia wakati huu angalau mgonjwa wao alikuwa mikononi mwa madaktari, nafuu ya familia hii ilifikia kikomo dakika chache baada ya kuanza kupokea matibabu ilipothibitishwa kwamba mama na mtoto walikuwa wamefariki.

Masaibu ya wanawake wajawazito katika visiwa vya Ziwa Victoria sio siri huku vituo vya matibabu na hata hospitali katika sehemu hizi zikiwa hazina uwezo kabisa wa kutekeleza taratibu sahili mwanamke mjamzito anapokumbwa na matatizo ya uzazi.

Kwa mfano, katika Kisiwa cha Remba, ni zahanati moja inayoshughulikia zaidi ya wakazi 3,000.

Kulingana na Dkt Gordon Okomo, Mkurugenzi wa afya wa Kaunti ya Homa Bay, kituo hiki hakina vifaa vya kutosha kushughulikia masuala ya dharura kama vile mama anapohitaji kuongezwa damu.

Kulingana na Dkt Okomo, hata hivyo akina mama wajawazito katika kisiwa hiki huelekezwa katika kituo cha afya cha Sena katika Kisiwa cha Mfangano, ambacho kina uwezo mkubwa wa matibabu.

Hata hivyo, Bw Robinson Okeyo, msimamizi wa zamani wa mipango wa shirika la kijamii la Ekialo Kiona katika kisiwa cha Mfangano, asema hata hapa masaibu ni yale yale.

Kulingana na afisa wa kituo cha afya cha Sena ambaye hakutaka kutajwa, kituo hiki kinaweza tu shughulikia taratibu sahili za maabara kwa akina mama wajawazito, lakini inapowadia katika masuala magumu kama vile upasuaji, basi wagonjwa huelekezwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Mbita.

“Kituo hiki hakina thieta (chumba cha upasuaji) na japo jengo lililonuiwa kuhifadhi kitengo hiki lipo, vifaa vya shughuli hii havipo,” asema.

Bw Okeyo asema mipango ya kuimarisha viwango vya hospitali hii na kuwa hospitali ya rufaa imekuwepo kwa muda ila kufikia sasa hakuna chochote kilichofanyika.

“Kwa hivyo wanawake wajawazito hulazimika kusafiri katika hospitali zabara kama vile Sindo, Soni au Mbita,” aeleza Bw Okeyo.

Kando na hayo, Bw Okeyo asema kwamba ambulenzi ya boti inayoshughulikia jamii ya kisiwa hiki kwa kusafirisha wagonjwa inayoendeshwa na shirika la kijamii la Ekialo Kiona, haina vifaa vya kushughulikia dharura hasa mama anapotaka kujifungua.

“Kuna visiwa kama vile Takawiri ambavyo vina ambulenzi za boti, lakini pia vifaa hivi vya usafiri havina vifaa vya kimatibabu. Wanawake wengine wajawaito hutegemea boti za walinda usalama baharini ambazo pia sio za kutegemewa,” aeleza Bw George Obel, afisa wa usalama wa ziwani katika Kisiwa cha Remba.

Utafiti wa 2015 wa Baraza la Kitaifa la Idadi ya watu na ustawi ulionyesha kwamba Kaunti ya Homa Bay ni mojawapo ya maeneo hatari sana kwa wanawake wajawazito nchini.

Kwa mujibu wa utafiti huo, miongoni mwa wanawake 100,000 wajawazito wanaojifungua katika kaunti hiyo, 583 hufariki katika harakati hizo.

Hii ni idadi kubwa ikilinganishwa na takwimu za kitaifa wakati huo zilizoonyesha kwamba ni wanawake 488 miongoni mwa 100,000 hufariki wakijifungua.

Baadhi ya masuala ambayo yamechangia hali hii, ripoti hii yasema, ni kutofikia huduma ya afya wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua.

Ni asilimia 50 pekee wanaofikia huduma za kujifungua hospitalini kwa wakati ufaao.

  • Tags

You can share this post!

Mbagathi kutoa tiba kidijitali – NMS

TUSIJE TUKASAHAU: Wafanyabiashara jijini Nairobi...

T L