SHINA LA UHAI: Hofu ya makali ya virusi vipya vya corona

SHINA LA UHAI: Hofu ya makali ya virusi vipya vya corona

Na LEONARD ONYANGO

WANASAYANSI wanaendelea na uchunguzi ili kubaini madhara ya aina mpya ya virusi vya corona vilivyogunduliwa humu nchini wiki iliyopita kwa watoto na vijana.

Hii ni baada ya tafiti zilizofanywa katika mataifa mbalimbali duniani kugundua kuwa virusi hivyo vipya vinasambaa kwa kasi ya juu miongoni mwa watu wa umri mdogo. Lakini madhara ya virusi hivyo kwa watoto na vijana yangali hayajulikani.

Kaimu Mkurugenzi wa Wizara ya Afya Patrick Amoth wiki iliyopita, alisema kuwa wanaume wawili – raia wa kigeni waliozuru Kenya – walipatikana na virusi vipya vya corona, vinavyojulikana kama 501Y.V2, sawa na vile vilivyogunduliwa nchini Afrika Kusini.

Dkt Amoth alisema kuwa wawili hao ambao hawakuonyesha dalili zozote za kuwa na corona tayari wamejea makawao.

Aidha alisema kuwa kuna uwezekano kwamba hawakuambukiza Wakenya.

“Ikiwa wangekuwa wameambukiza Wakenya virusi hivyo vya 501Y.V2, tungekuwa tumeanza kushuhudia idadi ya maambukizi ikiongezeka kwa kasi humu nchini,” Dkt Amoth aliambia jarida la Afya na Jamii.

Lakini baadhi ya wataalamu wa afya wanashikilia kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba wanaume hao waliambukiza Wakenya virusi hivyo kwani walitangamana na watu kabla ya kuondoka humu nchini.

Dkt Amoth alifichua hayo siku chache baada ya wanasayansi 10 wa Taasisi ya Kutafiti Matibabu (Kemri) kugundua aina nyingine ya virusi vya corona katika Kaunti ya Taita Taveta.

Kulingana na wanasayansi hao wa Kemri, aina mpya ya virusi vya corona vilivyopatikana katika Taita Taveta, ni tofauti na virusi vya 501Y.V2 (vilivyogunduliwa Afrika Kusini) na B.1.1.7 (vilivyopatikana Uingereza).

Dkt Charles Agoti aliyeongoza watafiti hao anasema virusi hivyo vipya vilivyopatikana katika Taita Taveta huenda vikasababisha idadi ya maambukizi ya corona kuongezeka kwa kasi humu nchini.

Kati ya Juni na Oktoba 2020 watafiti wa Kemri wamebaini aina 16 za virusi vya corona katika maeneo ya Pwani. Lakini Dkt Agoti anasema kuwa aina hizo 16 ni hafifu na havina madhara kwa afya. Hiyo inamaanisha kuwa hata mtu akipata maambukizi ya virusi hivyo, hawezi kuugua au kuonyesha dalili zozote.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa aina hizo mpya zinazoendelea kugunduliwa kote ulimwenguni ni tishio.

Mwakilishi wa WHO humu nchini Rudi Eggers anasema kuwa kuibuka kwa aina mpya za virusi vya corona kote duniani ni jambo la kuogofya.

“Kuibuka kwa aina mpya za virusi vya corona kunamaanisha kuwa chanjo ambazo tayari zinatumiwa kukabiliana na maambukizi huenda zikakosa kufanya kazi. Utafiti zaidi unahitajika ili hatua za haraka zichukuliwe,” anasema.

Aina ya 501Y.V2

Virusi aina ya 501Y.V2 viligunduliwa Afrika Kusini na watafiti wa Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal baada ya visa vya maambukizi kuongezeka kwa kasi katika mkoa wa Eastern Cape.

Matokeo ya awali ya tafiti zilizofanywa na taasisi ya Africa Health Research Institute na Chuo Kikuu cha Witwatersrand Afrika Kusini, na kuchapishwa Alhamisi iliyopita katika jarida la Nature, yalibaini kuwa aina ya 501Y.V2 vina uwezo wa ‘kukwepa’ kinga za mwili hivyo kuwafanya baadhi ya waathiriwa kulemewa na ugonjwa huo.

Watafiti hao walisema kuwa virusi hivyo vinaweza kuwaambukiza tena watu waliopona baada ya kuugua aina ya kwanza ambayo imeenea kote duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ripoti yake ya kila wiki iliyotolewa Jumatano iliyopita, lilisema kuwa virusi vipya vya B.1.1.7 ambavyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza Uingereza, sasa vimesambaa katika nchi 60 kote duniani.

Mataifa 23, ikiwemo Kenya, yameripoti kupata virusi aina ya 501Y.V2 ambavyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza Afrika Kusini.

Brazili imegundua aina mpya inayojulikana kama P.1 baada ya raia wawili kupimwa katika uwanja wa ndege wa Haneda, nchini Japan.

Kulingana na Kituo cha Kudhibiti Maradhi (CDC), virusi vya P.1 vina uwezo mkubwa wa kukwepa kinga za mwili. Hiyo inamaanisha kuwa kinga za mwili hushindwa kuvitambua vinapoingia mwilini.

Virusi vipya vilivyogunduliwa Afrika Kusini vinasambaa kwa asilimia 50 zaidi kuliko vya kawaida. Kasi ya kuenea kwa virusi vipya vilivyopatikana Uingereza ni kati ya asilimia 56 -70 zaidi ikilinganishwa na vya kawaida.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Imperial College London, ulibaini kuwa aina mpya ya vilivyopatikana Uingereza vinaathiri zaidi watoto na vijana wa chini ya umri wa miaka 20.

Virusi vya kawaida vinaathiri zaidi watu wazima kuliko watoto. Kulingana na wanasayansi, hilo linasababishwa na ukweli kwamba seli za watoto zina ‘milango’ michache ambayo virusi vya corona hutumia kuingia ndani ya seli.

Wanasayansi wanahofia kwamba huenda kuna uwezekano aina mpya inaingia ndani ya seli bila kizuizi.

Lakini Hospitali ya watoto ya Royal College of Paediatrics and Child Health (RCPCH) ya Uingereza iliondoa wasiwasi kwa kusema kuwa haijapokea watoto walio hali mahututi kutokana na corona, kulingana na shirika la BBC.

Afisa Mkuu wa hospitali hiyo Laura Duffel alikiri kuwa idadi ya watoto wanaopatikana na corona hawaonyeshi dalili zozote za maradhi hayo.

Hospitali hiyo pia iliambia BBC kuwa, idadi ya vijana wa kati ya miaka 18 na 30 wanaopatikana na corona pia imeongezeka japo wengi wao hawaonyeshi dalili.

Ingawaje watoto na vijana hawalemewi sana na corona ikilinganishwa na watu wa umri wa juu, tafiti zinaonyesha wao ni miongoni mwa walioathiriwa pakubwa kiakili na janga la hili nchini.

Kulingana na Nancy Karwitha, mtaalamu wa saikolojia ya watoto, visa ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa nchini hivi karibuni ambapo watoto wanashambulia wenzao na walimu shuleni vyaweza kuwa matokeo ya matatizo ya kiakili yaliyosababishwa na janga la virusi vya corona.

Wataalamu sasa wanasema kuwa chanjo inayoendelea kutolewa katika mataifa mbalimbali duniani huenda ikasaidia kupunguza kasi ya kuibuka kwa aina mpya za virusi vya corona.

Japo kuna hofu kwamba huenda virusi vipya vikasababisha chanjo zinazotumika sasa kukosa makali, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Rockefeller ulibaini kuwa chanjo zilizotengenezwa na kampuni za Moderna na Pfizer/BioNTech zina uwezo wa kusambaratisha virusi hivyo vipya.

Watafiti hao walichukua damu kutoka kwa watu ambao wamedungwa chanjo za Moderna na Pfizer/BioNTech na kisha kuweka virusi vipya vilivyopatikana Uingereza na Afrika Kusini.Walipopima baadaye waligundua kuwa virusi hivyo vililemewa na chanjo hizo.

Kulingana na CDC, watu milioni 2.4 tayari wamedungwa chanjo ya kuzuia corona nchini Amerika.

Dkt Agoti wa Kemri anasema kuwa aina mpya ya virusi vilivyogunduliwa katika Kaunti ya Taita Taveta ni hafifu na vinaweza kusambaratishwa na chanjo kwa urahisi.

Kulingana na waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, Kenya inatarajiwa kupokea shehena ya kwanza ya chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya AstraZeneca kwa ushirikiano Oxford mwishoni mwa mwezi ujao. Kenya inatarajia kupokea dozi milioni 47 za chanjo ya corona.

Aidha Serikali imeagiza dozi milioni 24 kupitia mradi wa Gavi ambao unalenga kupatia chanjo nafuu mataifa maskini. Kenya pia itapokea dozi milioni 11 kupitia Umoja wa Afrika (AU) na dozi milioni 12 kutoka vyanzo vinginevyo, kulingana na Waziri Kagwe.

You can share this post!

Bobi Wine akerwa na kimya cha viongozi wa bara Afrika

PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda kwenye ulimi balaa beluwa,...