SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la saratani ya mapafu nchini

SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la saratani ya mapafu nchini

Na PAULINE ONGAJI

MIAKA mitatu iliyopita, Jess*, mkazi wa mtaa wa Kayole jijini Nairobi, aligundulika kuugua saratani ya mapafu ikiwa katika awamu ya tatu.

Kabla ya utambuzi huo, binti huyu ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 28 pekee, aliteseka kwa muda mrefu huku akisaka matibabu kutoka kwa hospitali mbalimbali, bila kupata nafuu.

“Tatizo lilikuwa kwamba kila nilipoenda hospitalini, daktari alitambua maradhi tofauti hivyo kunibadilishia dawa,” aeleza.

Wakati huo asema, alionyesha ishara za maradhi tofauti.

“Nakumbuka kabla ya maradhi haya kugundulika, nilikuwa nakohoa damu na nilikumbwa na maumivu mengi. Aidha, wakati huo pia nilipatikana na Kifua Kikuu-TB, suala lililotatiza juhudi za madaktari kutambua nilichokuwa naugua haswa. Hata hivyo nilitibiwa TB na kukamilisha matibabu,” aeleza.

Lakini ajabu ni kwamba hakujulisha jamaa na marafiki kwamba amepatikana na saratani ya mapafu.

“Nilificha hali yangu kwa sababu wakati huo nilikuwa kiongozi wa vijana kanisani na nilichukulia maradhi haya kuwa ya aibu. Kumbuka kwamba ugonjwa huu mara nyingi huhusishwa na uvutaji sigara. Niliona iwapo ningetangaza hali yangu, basi ningetengwa,” aeleza.

Aidha, alihofia kwamba kutokana na sababu kuwa alikuwa anafanya kazi katika sekta ya utalii, angepoteza ajira.

Hata hivyo, kwa bahati nzuri mwaka wa 2019, alifanyiwa upasuaji ambapo pafu lake moja liliondolewa.

“Aidha, baada ya upasuaji huo, nilifanyiwa awamu sita za tibakemia, taratibu zilizochukua miezi minne kukamilisha. Kwa sasa bado naendelea na uchunguzi wa kimatibabu kuhakikisha kwamba kansa hiyo haitarejea,” aeleza.

Kulingana na ripoti ya utafiti iliyozinduliwa na Wizara ya Afya miezi miwili iliyopita, 39% ya vifo nchini 2020, vilitokana na maradhi yasiyosambaa ikilinganishwa na 27% mwaka wa 2014.

Aidha inatabiriwa kwamba vifo vinavyotokana na maradhi yasiyosambaa vitaongezeka kwa 55% kufikia 2030.

Kulingana na utafiti huo, maradhi yasiyosambaa yameonekana kuendelea kuongezeka nchini na sasa yanasemekana kusababisha 46% ya vifo vyote nchini, huku walio chini ya umri wa miaka 40 wakionekana kuathirika pakubwa.

Ongezeko hili linasemekana limetokana na mitindo duni ya kimaisha ikiwa ni pamoja na matumizi ya tumbaku, kutozingatia lishe bora, kutofanya mazoezi na unywaji pombe kupindukia.

Kwa upande wa kansa ya mapafu, utambuzi wake huwa kwa viwango sawa (11.6%) na vile vya kansa ya matiti.

Hata hivyo, kansa ya mapafu huua watu zaidi kwa mwaka ikilinganishwa na ile ya matiti, utumbo na tezi kibofu kwa jumla.

Kulingana na takwimu zilizochapishwa na Shirika la Afya Dunia – WHO – miaka mitatu iliyopita, vifo vinavyotokana na kansa ya mapafu nchini Kenya, vilifika 481 au 0.19% ya idadi yote ya vifo.

Aidha, viwango vya vifo ni 2.67 kwa kila idadi ya 100,000 ambapo Kenya imeorodheshwa nambari 152 miongoni mwa mataifa yaliyoathirika pakubwa duniani.

Makadirio ya kansa ya mapafu kutoka kwa WHO (GLOBOCAN) 2020, yanaonyesha kwamba mwaka jana, idadi ya wagonjwa wapya wa maradhi haya humu nchini ilikuwa 794.

Aidha, takwimu hizo zinaashiria kwamba wagonjwa 729 walifariki kutokana na maradhi hayaUlimwenguni, idadi ya vifo vinavyotokana na kansa hii, inatabiriwa kufikia milioni 2.45 kufikia mwaka wa 2030, ongezeko la asilimia 39 katika kipindi cha mwongo mmoja tu.

Kulingana na Prof Fredrick Chite Asiriwa, mtaalamu wa maradhi ya kansa na ya damu, japo sababu kuu zinazojulikana kusababisha maradhi haya hapa nchini ni uvutaji sigara na ukosefu wa hewa safi, asilimia kubwa ya wanaougua huwa ni kutokana na sababu zisizojulikana.

“Uvutaji sigara ndio hatari kubwa zaidi inayosababisha kansa ya mapafu huku ikichangia asilimia 80 ya visa vyote. Lakini mazingira na jeni pia huchangia. Kuwa wazi kwa asbesto, kemikali za radon aseniki, beryllium na urani, pia kumehusishwa na kansa ya mapafu,” asema.

Hatari

Aidha, hatari ya kukumbwa na aina hii ya saratani huongezeka ikiwa kuna historia ya kansa katika sehemu nyingine ya mwili, umri, historia ya kifamilia, kufanyiwa utaratibu wa mnururisho (radiation) katika sehemu ya kifua, na maradhi mengine ya mapafu kama vile Chronic Obstructive Pulmonary Disease (COPD).

Anadokeza ishara za kansa ya mapafu ni pamoja na mabadiliko ya kamasi, maumivu ya kifua au mgongo, kukohoa damu na ugumu wa kumeza chochote.

“Baadhi ya mbinu za uchunguzi zinazotumika katika utambuzi wa maradhi haya ni picha za eksirei, uchunguzi wa CT na PET scans, bronchoscopy (utaratibu ambapo njia za hewa mapafuni zinachunguzwa kwa kutumia mrija mwepesi kwa jina bronchoscope), needle biopsies (utaratibu ambapo sindano inatumika kuondoa seli, majimaji na tishu kutoka uvimbe unaoshukiwa kuwa na seli za kansa),” aeleza.

Prof Chite asema ni vigumu kudadisi takwimu kamili za maradhi haya kwani visa vingi vya kansa ya mapafu havitambuliwi kutokana na ukosefu wa uhamasishaji wa kutosha katika jamii na wahudumu wa kiafya.

“Aidha, kuna tatizo la violezi dhaifu vya utambuzi wa maradhi haya, ukosefu wa vifaa maalum vya utambuzi katika vituo vya kiafya nchini, huduma duni wakati na baada ya matibabu,” aongeza.

Kulingana na WHO, barani Afrika, ukosefu wa mbinu za utambuzi wa mapema, vilevile elimu muhimu na matibabu, ndio changamoto kubwa.

Mataifa maskini, Kenya ikiwemo, ambapo uwezekano wa kuishi ni chini ya viwango wastani, hunakili 15% pekee ya uwepo wa matibabu ya maradhi haya katika mifumo ya afya ya umma.

Hii ni tofauti sana ikilinganishwa na mataifa tajiri ambapo uwezekano wa kufikia huduma hizi ni 90%.

Ni udhaifu huu ambao umesababisha wagonjwa wengi wa kansa hii nchini kusaka huduma ng’ambo.

Inakadiriwa kwamba kati ya 25% na 30% ya waathiriwa humu nchini, husaka matibabu katika mataifa ya kigeni. Mara nyingi gharama ya matibabu ni ghali mno.

“Kansa ya mapafu sio ugonjwa mmoja na hutegemea na awamu ya maradhi hayo. Matibabu huhusisha taratibu kadhaa kama vile upasuaji, tibaredio, tibakemia n.k na pia huhusisha kikundi cha wataalamu. Gharama ya matibabu yaweza kuwa kati ya Sh1M na Sh5.5M,” aeleza Prof Chite.

Anasema kwamba wakati huu wa janga la corona, hali imekuwa mbaya hata zaidi kwa wanaougua maradhi haya.

“Hii ni kwa sababu wengi wanachelewa kupokea matibabu. Aidha ishara za Covid- 19 zinafanana na zile za kansa ya mapafu. Kwa mfano kushindwa kupumua, kukohoa na matatizo kifuani. Kuna baadhi ya wagonjwa ambao huenda wamefariki pasipo kusaka matibabu kutokana na marufuku ya usafiri kutoka sehemu moja au nyingine, vilevile hofu ya kushukiwa na jamaa zao kwamba huenda wanaugua corona badala ya maradhi haya,” aongeza.

Hata hivyo anasisitiza kwamba bado ni mapema kutambua iwapo corona imechangia kuongezeka kwa wagonjwa wa aina hii ya saratani.

“Kuna uwezekano kuwa wakati huu wa janga la corona mambo yamekuwa mabaya, lakini bado tunapokea wagonjwa wawili kila wiki sawa na awali. Tungali tunaendelea kudadisi hali ilivyo,” asema.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Ukuvu mdomoni ni ishara ya HIV?

Wakenya ‘wasukuma’ juu bei ya mafuta TZ