SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la visa vya ukoma nchini

SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la visa vya ukoma nchini

LEONARD ONYANGO NA WANGU KANURI

UKOMA ni miongoni mwa magonjwa hatari yaliyotajwa katika Biblia na Koran.

Kwenye Biblia kumerekodiwa visa kadhaa vinavyoonyesha wagonjwa wa ukoma wakibaguliwa na kutengwa.

Katika Kitabu cha Mathayo 8, Yesu Kristo amerekodiwa akimgusa na kumponya mwathiriwa. Kwa ufupi ugonjwa huu umekuwepo tangu jadi.

Lakini ripoti ya wizara ya Afya ya hivi punde inaonyesha kuwa visa vya ugonjwa huu vinazidi kuongezeka kwa kasi nchini badala ya kupungua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka kwa kasi tangu 2016. Kwa mfano, kati ya 2018 na 2019, visa viliongezeka kutoka 110 hadi 154.

Mkuu wa Maradhi ya Kitropiki Yaliyotelekezwa (Neglected Tropical Diseases-NTD) Dkt Edith Ramaita, anasema kuwa ukoma umekita katika kaunti sita za Magharibi mwa Kenya na Pwani.

Kaunti zilizoathiriwa sana ni Siaya, Homa Bay, Busia, Kisumu, Kwale na Kilifi.

Ukoma huenezwa baada ya kushika majimaji yanayotoka kwenye pua au mdomo wa mgonjwa.

“Ugonjwa huu wa kuambukiza husababishwa na bakteria Mycobaterium leprae na huathiri sana ngozi, macho, njia ya kupumua na mishipa. Bakteria hao husababisha mwasho ambao hujeruhi mishipa na kumfanya mtu awe mlemavu. Mishipa huwa hafifu, humfanya mtu kupoteza uwezo wake wa kuhisi na ngozi huwa kavu na baadhi ya sehemu kuwa nyeupe kuliko sehemu nyinginezo,” anasema Dkt Ramaita.

Dalili za ukoma huchukua hadi miaka 20 kabla hazijaanza kuonekana huku wagonjwa wakichelewa kutafuta matibabu hivyo kueneza kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

“Ukoma ni mojawapo ya maradhi yaliyotelekezwa nchini na kote duniani na ukosefu wa fedha kusaidia kuwatafuta wanaougua husababisha kuenea kwa urahisi,” anasema.

Aidha huathiri zaidi watu maskini kwani huishi katika mazingira machafu na huchelewa kupata matibabu.

“Viini vinavyosababisha ukoma vinapatikana katika maeneo yenye joto jingi na yanayokaribiana na vyanzo vya maji. Hiyo ndiyo sababu maradhi haya yanapatikana zaidi katika maeneo ya Nyanza na Pwani,” anaongeza.

Asilimia 11 ya wagonjwa humu nchini ni watoto wa chini ya umri wa miaka 15 na zaidi ya asilimia 30 ni wazee wa zaidi ya miaka 65.

Hata ingawa huathiri jinsia zote mbili, mnamo 2018, Kenya ilirekodi visa 110 huku asilimia 57 ikiwa ni wanaume huku watoto kati ya miaka 0-14 wakichangia kwa asilimia 2.7.

Inakadiriwa kuwa asilimia 95 ya watu ambao hupatwa na bakteria ya Mycobaterium leprae hawapati ukoma, ishara kuwa kingamwili ya mtu huchangia pakubwa katika kuenea na kudhibitiwa kwa ugonjwa huu.

Japo mgonjwa huweza kupona anapoanza kupokea matibabu mapema, wengi hupata ulemavu.

Kulingana na Dkt Waqo Erjesa, Mkuu wa Kitaifa wa Programu ya Kifua Kikuu, Ukoma na Magonjwa ya Mapafu (DNTLD-P), baadhi ya ulemavu unaotokana na ukoma ni pamoja na ulemavu wa macho, vidole vya mkono na miguu.

“Unaweza ukapoteza nyusi na kope, kutoweza kupepesa macho kwa hiari, kutoweza kupumua vizuri, kuvunjika mkono, kutoweza kusongesha kidole kidogo na gumba, jeraha kwa vidole vya miguu na kutoweza kukunja mguu au mkono,” anasema Dkt Erjesa.

Ulemavu huo wa viungo vya mwili husababishwa na maambukizi yanayotatiza kusambaa kwa damu katika baadhi ya maeneo ya mwili, hivyo kumfanya mtu kupoteza hisia,kuwa na vidonda, mpasuko na maambukizi na kutoweza kushika vitu vizuri.

Dalili na matibabu

Wataalamu huweza kujua mtu anaugua ukoma iwapo ana moja kati ya dalili zifuatazo; kutohisi au kuwa na madoadoa mekundu kwenye ngozi. Mshipa iliyo nje ya ubongo na uti wa mgongo kuwa nene na kufanya misuli inayosaidiwa na mishipa hiyo kuwa hafifu na kuwepo na bakteria yenye asidi kwenye ngozi.

“Ukoma hutibiwa kwa kutumia dawa nyingi (MDT) ambazo wagonjwa hupata bure kwa hisani ya Shirika la Afya Duniani (WHO). Kwa hivyo ni wajibu wa mwathiriwa kwenda hospitalini kwa matibabu na wahudumu hufuatilia mgonjwa kwa miezi sita au hadi apatapo afueni,” anasema Dkt Erjesa.

Kulingana na WHO, visa 127,558 vilirekodiwa duniani 2020 na watoto walio chini ya miaka 15 wakichangia kwa 8,629.

Kulikuwa na visa milioni 4.4 miongoni mwa watoto mwaka wa 2020 kote duniani. Kati ya visa hivyo, watoto 7198 walikuwa na ulemavu wa kutoona vizuri na kutoweza kuhesabu vidole vya mkono kwa pengo la mita sita.

Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka huo, wagonjwa 129,389 walikuwa wanapokea matibabu. Aidha janga la Covid-19 lilivuruga mpango wa kuzuia maradhi haya kusambaa. 2019 ikilinganishwa na 2020, WHO ilikuwa imeweza kupunguza kwa asilimia 37 visa vya ukoma.

Mwaka wa 2018, nchi 127 duniani zilirekodi visa 208,619 huku idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa kutoka nchi za Amerika, Afrika na Asia ya Kusini-Mashariki.

You can share this post!

Wamunyinyi taabani vigogo wakilenga kumbandua Agosti

Bodaboda walia polisi jijini bado wanawadhulumu

T L