SHINA LA UHAI: Huduma mbovu katika hospitali za Kaunti zinavyoua wajawazito

Na LEONARD ONYANGO

IDADI ya wanawake wanaojifungulia hospitalini imeongezeka kutoka asilimia 44 hadi 72 tangu kuanzishwa kwa huduma za kujifungua bila malipo nchini mnamo 2013.

Lakini huduma duni katika hospitali za umma katika kaunti mbalimbali zinasababisha mamia ya wanawake kurejeshwa nyumbani wakiwa ndani ya majeneza.

Hamido Dakane, 30, ni miongoni mwa waathiriwa wa hivi karibuni waliopoteza maisha wakijifungua hospitalini kutokana na huduma duni.

Mumewe, Abdirahman Abdi, angali amegubikwa na majonzi tangu kumzika Hamido nyumbani katika kijiji cha Umoja, Kaunti ya Tana River, mapema mwezi huu.

Bw Abdi anasema kuwa hajakuwa akipata usingizi tangu alipompoteza mkewe aliyefariki alipoenda kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Hola.

Kulingana na Roble Gamano, mamake Hamido, mwendazake alikimbizwa hospitalini alipokumbwa na utungu saa tatu usiku.

Roble Gamano, mamake mwendazake Hamido Dakane akiwa na wajukuu wake wakati wa mahojiano katika kijiji cha Umoja, Kaunti ya Tana River. Picha/ Stephen Oduor

Walipo wasili, Hamido alilazwa katika chumba cha kujifungua ambapo waliombwa kusubiri ahudumiwe.

“Baadaye muuguzi alitwambia kuwa Hamido alifaa kujifungua kwa njia ya upasuaji na daktari hakuwa karibu.

“Tulingojea kwa zaidi ya saa tatu na hakukuwa na huduma zozote huku Hamido akihangaishwa na maumivu,” anasema.

Muuguzi alifanikiwa kumpata daktari usiku wa manane kwa njia ya simu. Daktari, hata hivyo, alisema kuwa chumba cha kufanyia upasuaji kilikuwa katika hali mbovu na akataka Hamido ahamishiwe katika hospitali nyingine.

“Daktari alisema kuwa hospitali haikuwa na vifaa vya kufanyia upasuaji akatutaka tupeleke binti yangu katika hospitali ya Garissa,” anaeleza.

Familia, hata hivyo, ilishauriwa kutoa taarifa za uongo kuhusu walipotoka ili kupata huduma za haraka katika Kaunti ya Garissa.

“Wahudumu wa afya katika hospitali ya Hola walitwambia tuseme kuwa tumetoka eneo la Charidende lililoko umbali wa kilomita 70 kutoka mjini Hola ilhali tulikuwa katika hospitali ya Hola iliyo umbali wa kilomita 14,” anasema.

Walipokuwa wakijiandaa kuondoka, wahudumu hao waliwambia kwamba madereva wa ambulansi wamezima simu hivyo ilikuwa vigumu kuwafikia.

Ilipofika alfajiri, dereva alipatikana lakini ambulansi haikuwa na mafuta.

“Tuliambiwa tununue lita 70 za mafuta ya gari la ambulansi,” anaelezea.

Huku wakiwa katika harakati za kuchangisha fedha za mafuta kutoka kwa jamaa na marafiki, Hamido, alipumua kwa nguvu na kukata roho.

Walitafuta gari aina ya ‘Probox’ wakasafirisha mwili nyumbani kwa ajili ya mazishi.

Bakari Buya angali analaumu serikali ya Kaunti ya Tana River kwa uzembe tangu alipopoteza mkewe, Sikukuu Guyato, aliyefariki akijifungua mtoto wao wa tatu katika Zahanati ya Pumwani, Kaunti Ndogo ya Galole.

Bakari Buya akiwa na mwanawe aliyeachwa baada ya mkewe kufariki alipokuwa akijifungua katika zahanati ya Pumwani, Kaunti Ndogo ya Galole, Tana River. Picha/ Stephen Oduor

Madaktari wa zahanati hiyo walimhakikishia kuwa wangefaulu kumsaidia mkewe kujifungua na hakukuwa na haja ya kumhamisha hadi hospitali nyingine.

“Wahudumu hao walifanikiwa kumtoa mtoto tumboni kwa njia ya upasuaji na kumuosha. Ghafla mke wangu akaanza kuvuja damu.

“Nilikimbia kuwaita wahudumu ambao baadaye walitafuta gari la ambulansi ili wamhamishe katika hospitali nyingine. Walipiga simu katika hospitali ya Hola iliyoko umbali wa kilomita 30 kuomba gari la ambulansi lakini hakukuwa na madereva,” anasimulia.

Hatimaye, ambulansi ilipatikana saa tano baadaye lakini Sikukuu aliaga dunia akiwa njiani akikimbizwa hospitali ya Hola.

Wanawake wasiopungua 10 wamefariki katika Hospitali ya Hola pekee ndani ya miezi sita iliyopita.

Wanaharakati wa mashirika ya kijamii kama vile Muhuri na Haki Africa sasa wanaitaka serikali ya Kaunti ya Tana River kushtakiwa na familia ambazo zimepoteza wapendwa wao wakati wa kujifungua.

Na katika Kaunti ya Homabay, Maxwel Ochoo kutoka eneo la Ogongo anaishi kwa machungu baada ya kupoteza mtoto wake katika Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay Aprili, mwaka huu.

Bw Ochoo anasema kwamba nusura apoteze mkewe katika hospitali hiyo baada ya wahudumu wa afya kumtaka kwenda kununua vifaa vya kufanyia upasuaji ili wamsaidie mkewe kujifungua.

“Tulianzia katika hospitali ya Ogongo lakini tukaambiwa kitovu kilikuwa na tatizo hivyo tukatumwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay,” anasema.

Walichukua muda wa dakika 10 kutoka Ogongo kufika Hospitali hiyo.

“Tulipofika, tulipokelewa na wahudumu wa afya ambao ninashuku kwamba walikuwa wanafunzi. Mke wangu alipelekwa katika chumba cha kujifungulia.

“Lakini baada ya dakika 20, niliambia kuwa hospitali hiyo haikuwa na maji hivyo nilifaa kutafuta,” anaelezea.

Bw Ochoo anasema kuwa baada ya maji kuletwa kwa kibuyu, aliletewa orodha ya vifaa vya upasuaji alivyofaa kwenda kununua nje.

“Niliabiri pikipiki nikaenda kununua vifaa nilivyoandikiwa. Nilitumia Sh3, 850 kununua vifaa hivyo,” anasema.

Anasema aliketi nje ya chumba cha upasuaji akiomba Mungu mtoto na mkewe wawe salama baada ya upasuaji.

Baada ya kungojea kwa zaidi ya dakika 40 alishikwa na wasiwasi na akaamua kwenda kuchungulia kupitia dirishani.

“Wahudumu hao waliniona wakanifukuza. Lakini baada ya dakika 20 hivi mmoja wao alitoka nje na kuniambia kwamba mtoto aliaga dunia dakika chache baada ya kutolewa tumboni,” akasema.

Mnamo Mei, mwaka huu, madiwani wa Kaunti ya Homa Bay walimtimua waziri wa Afya Prof Richard Muga kutokana na huduma mbovu za afya katika eneo hilo.

Gavana Cyprian Awiti, hata hivyo, wiki iliyopita, alikataa kumfuta kazi Prof Muga akisema kuwa ni miongoni mwa mawaziri wake waaminifu.

Hamido na Sikukuu ni miongoni mwa wanawake 336 ambao hufariki kwa kila akina mama 100,000 wanaojifungua humu nchini.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya akina mama wanaofariki wakijifungua ni wa umri wa kati ya miaka 14 na 47.

Hiyo inamaanisha kuwa Kenya ina kibarua kikubwa kuafikia malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutaka vifo vinavyotokea wakati wa akina mama kujifungua kuisha kufikia 2030.

Idadi kubwa ya vifo vya akina mama wanaofariki wakati wa kujifungua vinaweza kuepukika.

Wizara ya Afya inakiri kuwa vituo vya afya na hospitali nyingi zilizo chini ya usimamizi wa serikali za kaunti hazina vifaa au uwezo wa kushughulikia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura.

Mpango wa Serikali kuhusu Matibabu ya Dharura 2020-2025, uliozinduliwa mapema mwezi huu, unasema kuwa kaunti nyingi zina huduma mbovu za ambulansi.

“Baadhi ya kaunti zimekodisha mashirika ya kibinafsi kutoa huduma za ambulansi. Mara nyingi watu hulazimika kutumia magari ya kibinafsi kukimbiza wagonjwa wao hospitalini.

“Katika maeneo ya vijijini na mitaa ya mabanda mijini, watu hutumia pikipiki, baiskeli, mikokoteni au punda kukimbiza akina mama wajawazito hospitalini.

Kulingana na WHO, gari la ambulansi linafaa kufika ndani ya dakika 20 baada ya kupigiwa simu.

WHO pia inapendekeza ambulansi moja inafaa kuhudumia watu 70,000 kwa kutegemea umbali.

Hiyo inamaanisha kuwa Kaunti ya Tana River inafaa kuwa na zaidi ya ambulansi sita zinazofanya kazi wakati wote.