SHINA LA UHAI: Je, ni ushirikina, laana au ugonjwa?

SHINA LA UHAI: Je, ni ushirikina, laana au ugonjwa?

KNA Na CHARLES WASONGA

KIJIJINI Ndalani, Yatta, Kaunti ya Machakos, familia ya Rael Mwikali imekuwa ikitafakari kwa zaidi ya miaka 30 bila kupata majibu.

Watoto wake wote wa kiume walipatwa na ulemavu katika hali ya kutatanisha licha ya kuzaliwa wakiwa buheri wa afya.

“Wote walipooza walipotimu umri wa kubaleghe. Wanne kati yao walipooza miguuni wakiwa katika Darasa la Sita,” anasema Bi Mwikali ambaye ni mama ya watoto 12.

Watatu kati yao wanatumia viti vya magurudumu ilhali mmoja wao hupewa usaidizi na mhisani ambaye humbeba hapa na pale, panapotokea haja ya kufanya hivyo.

Wengine wawili walifariki miaka 10 iliyopita wakiwa na umri wa miaka 20 baada ya kuishi na ulemavu na kukumbwa na changamoto nyingine za kiafya.

Bi Mwikali anasema kuwa amekuwa akihangaika na maswali tele kuhusu kiini cha mkosi uliowapata wanawe wa kiume.

Ajabu ni kwamba watoto wake wa kike wote ni buheri wa afya, hali inayoibua maswali kuhusu ni kwa nini ulemavu huo unawakumba wavulana pekee.

Alikuwa akiishi maisha ya furaha na mumewe maradhi ya kiajabu yalipoanza kuizonga familia yake.

Mwanzoni alidhani ilikuwa ni bahati mbaya tu. Lakini kadri miaka ilivyosonga huku akishuhudia wanawe wa kiume wakiendelea kulemaa, aling’amua kuwa tatizo hilo lilikuwa kubwa zaidi.

“Kila wavulana wangu walipotimu miaka 12, niliingiwa na matumaini kuwa wangeingia utu uzima afya yao ikiwa sawa. Lakini walipooza miguu mwaka huo huo, hali iliyowalazimu kuacha shule,” asema.

Stephen Wambua, 26, hawezi hata kutambaa na hutegemea wahisani ambao humbeba hapa na pale.

Mmoja wa wanawe Rael Mwikali ambaye hawezi hata kutambaa akiwa amebebwa na mhisani nyumbani kwao Kwa Ndolo, Ndalani, kaunti ndogo ya Yatta. PICHA | KNA

Naye Jonathan Mutuku, 20, hutumia viti vya magurudumu. Wanawe wengine wawili wamesajiliwa katika shule moja ya kutoa mafunzo maalum, ambako wanatunzwa.

Jambo la kusikikitisha ni kwamba kaka yao mwenye umri wa miaka 14 tayari ameanza kuonyesha dalili za kuathiriwa na ulemavu huo huo kwani miguu yake imeanza kupooza na hawezi kutembea bila kusaidiwa.

Mikono yake haiwezi kushika kiti chochote vizuri kwani vidole vyake vimepooza.Kando na ulemavu wa miguuni, wavulana hao wanaweza kuzungumza vizuri na akili zao ni razini.

“Nimezuru hospitali kadhaa nikitafuta matibabu, nimetafuta usaidizi wa maombi kutoka kwa viongozi wa kidini, nimewaendea waganga, lakini tatizo linaloizonga familia yangu imesalia kitendawili,” akasema Bi Mwikali.

Isitoshe, mwana wa kiume wa dadake mkubwa pia alikumbwa na aina hiyo ya ulemavu alipokuwa katika darasa la nane. Lakini alibahatika na akasajiliwa katika shule moja maalumu mjini Thika ambako alikamilisha kidato cha nne.

Bi Mwikali anasema matusi ambayo familia yake imekuwa ikipokea kutoka kwa wakazi yamewavunja moyo na kuwapotezea matumaini maishani.

“Tunanyanyapaliwa kwa sababu mtoto wa dadangu pia alipata ulemavu sawa na ulioathiri wanangu. Wanadai shida hiyo inasababishwa na uchawi pamoja na laana za kifamilia. Nimefanya kila juhudi ili laana hiyo iondolewe lakini nikashindwa,” akasema.

Licha ya shida zinazomkabili, Bi Mwikali hujibidiisha kusaka vibarua kukimu familia yake, japo kwa machungu.

Lakini matumaini yake ni kwamba, siku moja, chanzo cha madhila yao kitajulikana na kwamba hakuna mtoto katika familia yake atawahi kuathirika tena.

Benson Kinyae, ambaye ni mmoja wa majirani zake, anaeleza kuwa familia hiyo imepitia wakati mgumu ikijaribu kutafuta suluhu kwa matatizo yanayoikumba.

“Watu kutoka eneo hili hudai kuwa familia hii imerogwa na ndio maana watoto wao ni walemavu. Hali hii imewaletea masononeko makubwa zaidi,” Kinyae aeleza.

Lakini Dkt Erastus Amayo, mtaalamu wa masuala ya mishipa, anasema kuwa ugonjwa ambao husababisha watoto wa kiume kupooza wanapofikia umri wa kubaleghe unajulikana kama Duchenne Muscular Dystrophy (DMD).

Ugonjwa huo huharibu misuli na kuifanya kuwa dhaifu. Huathiri watoto wa kiume tu.

“Hii ni kwa sababu ugonjwa huu hutokana na hitilafu katika jeni za kiume ambazo hupitishwa kutoka kwa mama hadi kwa watoto wa kiume pekee,” anasema Dkt Amayo.

“Udhaifu wa misuli ambao husababishwa na ugonjwa huu ndio huchangia waathiriwa kupooza na ushindwa kutembea; na hivyo kuwalazimu kutumia viti vya magurudumu,” anaongeza daktari huyo ambaye anahudumu jijini Nairobi.

Kulingana na Bi Scola Muthama, ambaye ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Wakfu wa DMD nchini Kenya, watoto wengi walioathirika na ugonjwa huu hulemewa na kushindwa kutembea wakiwa na umri wa kuanzia miaka 12 kwenda juu.

“Mtoto wangu, Ferdinand Mutugi, 13, alipatikana na ugonjwa huu akiwa na umri wa miaka saba na akaanza kutumia kiti cha magurudumu mnamo 2015,” anaeleza.

Anasema kutokana na kuimarika kwa huduma za matibabu, kwa sasa ugonjwa huu unaweza kutibiwa kwa mbinu inayojulikana kitaalamu kama stem cell-therapy.

“Mbinu hii inahusisha kuchanganywa kwa seli na kutofautisha misuli mbalimbali ya mwili,” anaeleza Bi Muthama, akiongeza kuwa ugonjwa huu haujaenea sana nchini Kenya.

You can share this post!

Liverpool nguvu sawa na Crystal Palace katika EPL baada ya...

Chelsea na Tottenham watoshana nguvu katika gozi la EPL...

T L