SHINA LA UHAI: Je, wajua muziki ni dawa ya maradhi mbalimbali?

SHINA LA UHAI: Je, wajua muziki ni dawa ya maradhi mbalimbali?

NA JURGEN NAMBEKA

KWA watu wengi, muziki hutumika tu kwa ajili ya kujiburudisha.

Lakini je, wajua kwamba muziki pia ni dawa na waweza tumika kama tiba?

Kulingana na wataalamu, katika baadhi ya maradhi, muziki waweza kusaidia mgonjwa kupata nafuu ya haraka, na hivyo kuongeza kasi ya kupona.

Ndiposa sasa kuna nyanja ya tibamuziki inayotia fora sio tu katika mataifa ya magharibi pekee, bali pia humu nchini.
Willis Ochieng Ngei, al-maarufu Fololo (anayecheza gitaa), ni mwanamuziki ambaye amekuwa akitoa huduma hii katika Hospitali ya Mater jijini Nairobi, ambapo hutoa huduma hii kila siku ya wiki kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa nane mchana.

“Kawaida sisi huwa hospitalini kwa muda saa manne ili kuwapa tiba wagonjwa katika wadi mbalimbali. Lakini kabla ya kufanya hivi, sisi hufanya tathmini ya kila mgonjwa na kuamua ni aina gani ya tibamuziki atakayopewa,” aeleza.

Anasema kwamba wao pia hutembelea hata vyumba vya wagonjwa mahututi mara moja kila wiki.

Bw Willis Ochieng Ngei, almaarufu ‘Fololo’ mwanamuziki ambaye amekuwa akitoa huduma ya tibamuziki katika Hospitali ya Mater jijini Nairobi. PICHA | HISANI

Hali ni hiyo hiyo kwa wanabendi wa kundi la Daraja ambao pia kila siku ya wiki, wamejitolea kutoa huduma ya tibamuziki kwa watoto wanaougua kansa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Wanamuziki hawa wanasema kwamba walipokea ujuzi wao kutoka kwa wataalamu wa nchi za nje. Walilazimika kupata mafunzo haya ughaibuni kwani humu nchini aina hii ya tiba bado haijazingatiwa sana.

“Nilifuzu katika fani hii mwaka wa 2018 nchini Amerika ambapo nilipokea mafunzo kutoka kwa wataalamu waliokuwa wakitibu magonjwa ya kiakili na marekebisho ya viungo vya mwili,” aeleza.

Wanabendi wa Daraja pia walijifunza haya kutoka kwa daktari mmoja aliyekuwa amezuru nchini kwa utafiti wa tiba hiyo.
Na japo taaluma hii bado haijakumbatiwa vilivyo humu nchini, wataalamu wanasisitiza kwamba, matokeo yake ni makubwa katika matibabu.

Kulingana na Beryl Adoyo, afisa wa mipango wa tibamuziki katika shirika la kuwahudumia wagonjwa wa kansa la Faraja, ripoti za madaktari zinaonyesha kwamba muziki unachangia pakubwa katika tiba ya watoto walio na maradhi haya.

Ruth Moraa, mtaalamu wa tibakazi (occupational therapy) katika hospitali ya akili ya Mathari, Nairobi, asema kwamba katika shughuli zao, tibamuziki ni muhimu sana.

Kwa kawaida, kazi yake inahusisha kuwasaidia watu walioshindwa kutekeleza majukumu mbalimbali baada ya kupatwa na ajali ama kukumbwa na ugonjwa ambao huwazuia kufanya kazi hiyo.

“Katika tiba yetu sisi hutumia tibamuziki kumsaidia mgonjwa kurejea katika hali yake ya awali kiakili ama hata kimwili. Mara nyingi ukigundua mgonjwa anachangamkia aina fulani ya muziki, kumchezea kutamuwezesha kupata uponyaji haraka,” aeleza Bi Moraa.

Kulingana na mtaalamu huyu, tibamuziki husaidia sana wagonjwa wanaougua bipolar, walio na ugumu wa kupenda chochote maishani, na wale ambao sehemu ya mwili wao imeacha kufanya kazi.

“Tiba muziki ni muhimu sana. Kwa mfano unampata mtu ameumia sehemu ya mwili na tunapaswa kuinyoosha. Tukifanya uchunguzi wetu na tupate ana penda muziki au kusakata densi. Tutampa tibakazi inayohusisha kusakata densi. Baada ya muda utagundua kwamba mwili umeanza kunyooka,” asema.

Dkt Hemed Tahir, daktari wa watoto katika hospitali ya Aga Khan mjini Mombasa, anaeleza kuwa tibamuziki inatumika sana katika mataifa yaliyostawi kiuchumi ikilinganishwa na humu nchini.

“Tibamuziki ni mbinu nzuri ya tiba ila hatujaitumia sana kwa kuwa inatumika zaidi kutibu magonjwa sugu(Chronic). Katika nchi yetu tunaangazia sana magonjwa yanayoambukizwa hivyo haituizingatii sana,” aeleza Dkt Tahir.

Kulingana naye, muziki unatumika tu kama sehemu ya matibabu na mara nyingi haihesabiwi kama tiba kamili.

Licha ya hayo anaeleza kuwa muziki una nafasi muhimu kwa afya ya mwili na wengi hawafahamu umuhimu huo.

“Tibamuziki ipo kila mahali. Mtu anapokuwa amekwazika, atacheza muziki na apate nafuu. Unapokwenda katika afisi ambazo zinashughulikia idadi kubwa ya watu, muziki unatumika kuwatuliza huku wakisubiri kuhudumiwa. Kwenye kumbi za mazoezi, muziki unachezwa kusahaulisha mwili uchungu unaohisi wakati huo,” asema Dkt Tahir.

Tibamuziki ilianzishwa mnamo 1940 nchini Amerika ili kuwafariji wanajeshi waliokuwa wakikabiliwa na msongo wa mawazo na wasiwasi baada ya vita vya kwanza vya dunia.

Utafiti uliofanywa mwaka wa 2013 na madaktari Daniel Levitin na Monalisa Chinda kutoka Amerika, ulionyesha kuwa muziki unatoa uponyaji licha ya kutopimika.

Uchambuzi wao wa tafiti 400 zilizofanywa kuhusu tibamuziki, ulionyesha kuwa muziki unaimarisha kingamwili.

“Kwa kushiriki katika zoezi la kuimba, kucheza au kuskiza muziki, mwili wa mgonjwa hutoa kinga spesheli ya mwili iitwayo immunoglobin A,” utafiti huo unaeleza.

Kinga hii spesheli hupatikana katika mfumo wa kupumua, na kupitia muziki, wanaougua magonjwa ya kupumua kama vile kifua kikuu (TB) na maradhi ya pumu (asthma) wanaweza kupata nafuu.

Ripoti ya uchunguzi wa madaktari hao inaeleza pia kuwa tibamuziki husaidia kuunda seli za kuua virusi mwilini.
Kuna aina mbili ya tibamuziki kulingana na wataalamu hao; inayohusisha mgonjwa kushirikishwa kwenye muziki kwa kupiga makofi, kuimba au kucheza ala ya muziki.

Aina ya pili inahusisha wagonjwa walio katika hali mahututi au wasio na uwezo wa kusonga kupokea tiba hiyo kwa kuimbiwa tu.

Takwimu za Muungano wa Wanasaikolojia wa Amerika (APA), zinaeleza kuwa takriban watu milioni 1.6 duniani hutafuta tibamuziki kila mwaka.

Kulingana na muungano wa APA, muziki husaidia sana watoto wagonjwa walio katika chumba cha dharura. Isitoshe, kuna uhusiano mkubwa kati ya muziki na kukabiliana na msongo wa mawazo.

Kwa sasa taifa la Amerika linaongoza katika tiba hiyo likiwa na takriban wataalamu wa tibamuziki 26,000 ambao wamesajiliwa kulingana na APA.

APA inaeleza kuwa, wataalamu hao humwongoza mgonjwa kucheza ala ya muziki kwa siku kadhaa. Kwa mfano muathiriwa wa msongo wa mawazo, anaweza kupewa awamu 20 za kucheza ngoma.

Kulingana na Dkt Tahir, tibamuziki hutumika kama nyongeza kwa tiba ya magonjwa ya moyo, msongo wa mawazo, uraibu wa dawa za kulevya, ugonjwa wa kupoteza fahamu, usonji (Autism) na mengineyo.

Aidha wataalamu wanasema kwamba tibamuziki inaweza kuponya watu ambao wanasumbuka na ukosefu wa usingizi.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Brazil wakomoa Uswisi na kuingia...

Chumvi nyingi huzidisha msongo wa mawazo – Utafiti

T L