SHINA LA UHAI: Jinsi mihadarati inavyoua vijana kwa maradhi ya moyo

SHINA LA UHAI: Jinsi mihadarati inavyoua vijana kwa maradhi ya moyo

Na LEONARD ONYANGO

IDADI kubwa ya vijana katika maeneo ya Pwani walishindwa kujiunga na jeshi wakati wa shughuli ya kusajili makurutu iliyokamilika wiki iliyopita baada ya vipimo kuonyesha kwamba walikuwa na dawa za kulevya mwilini.

Katika mkutano ambapo viongozi mbalimbali walikutana na waziri wa Usalama, Fred Matiang’i wiki iliyopita katika Ukumbi wa Jumba la Tononoka, ilibainika kuwa mihadarati imechangia idadi ndogo ya vijana kutoka Mombasa kusajiliwa jeshini.

Ni katika mkutano huo, ambapo viongozi walilalamika kuwa jiji la Mombasa limebadilishwa kuwa ‘jalala’ la kutupa kokeini, bangi kati ya dawa nyinginezo za kulevya ambazo zimewaathiri pakubwa vijana.

Mbali na kuwakosesha nafasi za ajira, wataalamu wa afya sasa wanahofia kuwa dawa za kulevya huenda zikasababisha Kenya kupoteza idadi kubwa ya vijana kutokana na maradhi yasiyoambukizwa (NCDs) kama vile maradhi ya moyo, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

Takribani vijana 18 kati ya 100 wanaotumia dawa za kulevya humu nchini wako katika hatari ya kufariki mapema kabla ya kufikisha umri wa miaka 50 kutokana na maradhi yasiyoambukizwa, kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dkt Lilian Mbau wa chama cha kukabiliana na maradhi ya moyo, (Cardiac Society of Kenya) anasema kuwa idadi ya vijana wanaopatwa na magonjwa yasiyoambukizwa humu nchini inaongezeka kwa kasi.

“Hii ni kwa sababu vijana wengi wa chini ya umri wa miaka 25 wamejitosa katika matumizi ya sigara (tumbaku), pombe na aina nyinginezo za dawa za kulevya. Vilevile, vijana wengi wanakula vyakula vilivyosagwa kwa ulaini kama vile soseji na hawafanyi mazoezi,” anasema Dkt Mbau.

Magonjwa ya moyo kama vile shinikizo la damu, mshtuko wa moyo na kiharusi (stroke) yanachangia kwa kiasi kikubwa vifo vinavyotokana na maradhi yasiyokuwa ya kuambukizwa.

Dkt Mbau anasema kwamba kampuni za kutengeneza pombe, sigara na vyakula hatari kwa afya zimekuwa zikilenga vijana katika matangazo hivyo kuwatia hatarini.

“Vijana wanakulia kwenye mazingira ambayo yamejawa na vishawishi tele vya kuwaingiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya,” anasema.

Ripoti ya Hali ya Uchumi ya 2018 iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) inaonyesha kuwa maradhi ya moyo ni miongoni mwa magonjwa 10 yanayoua Wakenya wengi zaidi nchini.

Kwa mfano, mnamo 2016, maradhi ya moyo yalikuwa ya saba kwa kuua watu wengi zaidi nyuma ya malaria, nimonia, kansa, Ukimwi, kifua kikuu na ukosefu wa damu mwilini (anemia).

Mwaka huo, maradhi ya moyo yalisababisha vifo vya watu 5,799. Mnamo 2017, watu 4,786 walifariki kutokana na maradhi ya moyo humu nchini.

Tafiti ambazo zimefanywa katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu vya humu nchini zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watoto na vijana wamezama katika matumizi ya mihadarati.

Utafiti uliofanywa miongoni mwa wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo kikuu cha Nairobi na matokeo yake kuchapishwa katika jarida la Plos One mwaka 2020, ulionyesha kuwa asilimia 22 ya wanafunzi walikunywa pombe, asilimia 8 walivuta bangi na 7% walivuta sigara. Asilimia 13 ya wanafunzi walitumia aina zote za vileo kama vile pombe, bangi, kokeini, sigara.

Utafiti huo ulibaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoishi nje ya chuo wanatumia mihadarati ikilinganishwa na wenzao wanaoishi chuoni.

Wanafunzi

Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya nchini (NACADA) mnamo 2018, ulibaini kuwa asilimia 17 ya wanafunzi katika shule za msingi wanakunywa pombe au kutumia mihadarati.

Kulingana na ripoti ya Nacada, asilimia 22 ya wanafunzi wa shule za msingi wamewahi kuonja au wanaendelea kutumia mihadarati.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nacada Profesa Mabel Imbuga anaamini kuwa vurugu ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika shule mbalimbali tangu kufunguliwa kwa shule Januari 4, mwaka huu, huenda zinasababishwa na wanafunzi wanaotumia mihadarati.

“Bodi za Usimamizi wa shule (BOM) zinafaa kuweka mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata ushauri nasaha na mafunzo ya kuwahamasisha kuhusu madhara ya dawa za kulevya,” anasema Prof Imbuga.

“Visa vingi vya ukosefu wa nidhamu shuleni vinatokana na matumizi ya dawa za kulevya. Tangu kutokea kwa janga la virusi vya corona, tumesitisha programu za kutoa mafunzo shuleni na badala yake tunatumia vyombo vya habari kuhamasisha wanafunzi kuhusu madhara ya dawa za kulevya,” anasema.

Prof Imbuga anashauri viongozi wa dini kuweka mikakati ya kuhamasisha vijana kuachana na dawa za kulevya.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni iliyowasilishwa Bungeni mwezi uliopita, mamlaka ya Nacada inasema kuwa watoto wa kuanzia umri wa miaka minne wanatumia dawa za kulevya.

Mamlaka hiyo iliambia wabunge kwamba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanapata kwa urahisi pombe na dawa nyinginezo za kulevya.

Nacada inalaumu wazazi kwa kuwaingiza watoto wao katika matumizi mihadarati.

“Takwimu zinaonyesha kuwa wazazi wanaotumia dawa za kulevya wanasababisha watoto wao kujiingiza katika uraibu huo,” inasema ripoti hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa Nacada, Victor Okioma.

Nacada inataka adhabu dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya iongezwe hadi faini ya Sh50 milioni au kifungo cha maisha gerezani.

Utafiti uliofanywa nchini Amerika na matokeo yake kuchapishwa kwenye jarida la Journal Heart wiki iliyopita, unaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa watoto wanaotumia dawa za kulevya, kupatwa na maradhi ya moyo kabla ya kufikisha umri wa miaka 40.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kunywa pombe, kuvuta sigara na matumizi ya mihadarati hata kwa kiasi kidogo kunaweza kumweka mtumiaji katika hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo.

Watafiti hao walisema kuwa uwezekano wa wanawake wanaotumia vileo hivyo kupatwa na maradhi ya moyo uko juu ikilinganishwa na wanaume.

“Tulifahamu kuwa pombe, sigara na mihadarati inasababisha maradhi ya moyo lakini hatukujua kwamba hata kutumia kiasi kidogo ni hatari,” inasema ripoti hiyo.

Watafiti hao walichunguza watu 1,112,455 waliokuwa na maradhi ya moyo. Waligundua kuwa idadi kubwa ya waathiriwa walikuwa wakivuta sigara, ni wabugiaji wa pombe na walitumia mihadarati kama vile bangi, kokeini kati ya vileo vinginevyo.

Kwa mujibu wa watafiti hao, uwezekano wa watu wanaovuta sigara na kubugia pombe kwa kiasi kidogo kupatwa na maradhi ya moyo ni asilimia 50.

Wanaotumia kokeini, bangi na aina nyinginezo za mihadarati wako katika hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo maradufu ikilinganishwa na wenzao wanaokunywa pombe.

“Mishipa ya wanawake inayosafirisha damu kutoka kwenye moyo hadi sehemu nyinginezo za mwili hupatwa na hitilafu zaidi wanapotumia mihadarati ikilinganishwa na wanaume. Wanawake wanaovuta sigara pia wako katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi ya moyo ikilinganishwa na wanaume,” unasema utafiti huo.

Dkt Mbau analaumu serikali kwa kuwatelekeza vijana katika juhudi za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa.

“Kenya imekuwa ikitumia chini ya asilimia 10 ya mapato yake katika sekta ya afya tangu 2002, kinyume na Mkataba wa Abuja wa 2001 ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika waliahidi kutenga asilimia 15 ya bajeti zao,” akasema.

Anasema kuwa serikali haina takwimu sahihi kuhusu idadi ya vijana walio na maradhi ya moyo na magonjwa mengineyo yasiyoambukizwa hivyo ni vigumu kukabiliana na tatizo hilo.

Shirika la WHO linakadiria kuwa watu milioni 17.3 hufariki kila mwaka kutokana na maradhi ya moyo kote ulimwenguni. Maradhi hayo huchangia asilimia 30 ya vifo vyote duniani.

Shirika hilo linakadiria kuwa kufikia 2030, watu milioni 23.6 watakuwa wakifariki kila mwaka.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Uvimbe kwenye titi na chuchu

TAHARIRI: Vijana wasikubali kutumiwa kisiasa