SHINA LA UHAI: Jinsi ya kukabiliana na kiharusi cha muda mfupi

SHINA LA UHAI: Jinsi ya kukabiliana na kiharusi cha muda mfupi

Na PAULINE ONGAJI

ILIKUWA siku sawa na zingine ambapo Jeff (sio jina lake kamili), 42, aliamka kama kawaida kujitayarisha kwenda kazini.

“Niliamka na kwenda bafuni kuoga kama ada bila tatizo. Nilipokuwa nikijipangusa, nilijiangalia kwenye kioo na nikagundua mambo si shwari,” aeleza.

Anasema kwamba ghafla alishindwa kutembea na jicho lake la kulia halikuona vyema.

“Aidha, upande wangu wa kulia ulikufa ganzi huku mkono na uso ukiathirika. Upande wa kulia wa mdomo wangu ulianza kwenda kombo na nikashindwa kabisa kuzungumza,” aeleza.

Aidha, anasema kwamba hata hangeweza bonyeza vitufe kwenye simu yake ili kupiga simu.

“Muda mfupi baadaye, kwa bahati nzuri mamangu alinipigia simu kunijulia hali. Cha kushangaza ni kwamba nilishindwa kuzungumza na maneno kidogo niliyoweza kutamka, yalikuwa yakijikokota,” aeleza.

Hali hii iliendela kwa muda ambapo hakuweza kuwasiliana hata na jamaa zake.

“Nilishindwa zungumza na hata kutamka baadhi ya maneno. Sikuweza kujieleza kwa maandishi, suala lililozima kabisa uwezo wangu wa kuwasiliana hata kwa kuandika. Akilini mwangu nilikuwa najua nini cha kusema, lakini kuyatoa maneno hayo mdomoni ilikuwa ni balaa tupu,” asema.

Hilo lilibua wasiwasi nyumbani kwao na wakaamua kumpeleka hospitalini.

“Nilipelekwa kwa mtaalamu wa nyurolojia na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi,” asema.

Lakini hata kabla ya daktari kumkagua, alikuwa ameshaanza kurejelea hali yake ya kawaida.

“Nilianza kuzungumza na kutamka baadhi ya maneno yaliyokuwa yakinitatiza awali, na upande uliokuwa umekufa ganzi kidogo, ulianza kufufuka,” afunguka.

Baada ya kumuona daktari, alishauriwa kufanyiwa chunguzi kadha wa kadha ambapo baadaye daktari alimweleza kwamba alikuwa amekumbwa na shambulio la Transient Ischaemic Attack (TIA) au ukipenda kiharusi cha muda mfupi, shambulioa ambalo ni msururu wa ishara zinazoambatana na zile za kiharusi.

“Baada ya daktari kunishughulikia, niliandikiwa dawa na kuruhusiwa kurejea nyumbani, lakini tayari nilikuwa nimeanza kupata nafuu,” aeleza.

Kwa sasa hali yake Jeff inaendelea kuimarika huku akisubiri ukaguzi zaidi wa daktari katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

“Japo bado nakumbwa na changamoto za hapa na pale za matamshi na uandishi, sihisi maumivu wala udhaifu wowote,” aeleza.

Kulingana na huduma ya kitaifa ya afya nchini Uingereza (NHS), shambulio la TIA au kiharusi cha muda mfupi, ni hali ambapo damu inasitishwa kwa muda kutiririka katika sehemu fulani ya ubongo, suala linalokatiza msambao wa oksijeni kwenye ubongo.

“Ni hali ambayo huambatana na ishara sawa na kiharusi ikiwa ni pamoja na matatizo ya kuzungumza, kuona, kufa ganzi na udhaifu katika sehemu za uso, mikono na miguu,” asema Dkt Judith Kwasa, mtaalamu wa nyurolojia, jijini Nairobi.

Kulingana na Dkt Kwasa, ishara zake hasa huathiri uso, mikono, au mazungumzo.

“Mwathiriwa atahisi kana kwamba uso wake umeanguka upande mmoja ambapo atashindwa kutabasamu. Aidha, mdomo au jicho lake litaonekana kuuegemea upande mmoja.”

Kwa upande mwingine, anasema kwamba huenda mhusika ashindwe kuinua mkono mmoja au yote kwa sababu ya udhaifu na kufa ganzi.

“Aidha, huenda mwathiriwa akakumbwa na matatizo ya kusema ambapo anapozungumza, atasikika akikokoteza maneno na sauti, au ashindwe kuzungumza kabisa. Pia wakati mwingine huenda akawa na tatizo la kuelewa anachoelezwa,” asema.

Kulingana na American Heart Association, takriban 80% ya visa vya TIA hujitatua katika kipindi cha dakika 60 huku baadhi ya wagonjwa wakipata nafuu baada ya saa kadha, au ikizidi sana, saa 24.

Lakini japo kinyume na kiharusi athari za TIA hudumu kwa dakika chache, wataalamu wanasema kwamba sharti mgonjwa amuone daktari kabla ya kipindi cha saa 24 kukamilika.

“Pindi unaposhuhudia ishara hizi huna budi ila kutafuta huduma za kimatibabu za dharura,” aeleza Dkt Kwasa.

Kwa nini? Takwimu zinaonyesha kwamba takriban 10% ya wagonjwa wanaokumbwa na TIA watakumbwa na kiharusi kamili katika kipindi cha siku 90. Kati ya hao, nusu yao hukumbwa na kiharusi katika kipindi cha siku mbili.

“Huenda hali hii ikaashiria kwamba mgonjwa yuko katika hatari ya kukumbwa na kiharusi kamili, hali ambayo isipodhibitiwa yaweza sababisha ulemavu au hata kifo,” aongeza Dkt Kwasa.

Takriban mmoja kati ya watu watatu wanaokumbwa na TIA, hatimaye watapata kiharusi kamili, huku nusu wakiathirika katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya shambulio hili.

Takwimu kuhusu maradhi haya ulimwenguni sio dhahiri, ila kilicho dhahiri ni kwamba TIA ni tishio kwa maisha ya watu wengi. Wataalamu wanasema kwamba japo ni hali sahili na ambayo mara nyingi ina tiba, endapo mgonjwa hatapata huduma ya matibabu, ni hatari sana.

“TIA ni onyo kwamba huenda uko katika hatari ya kukumbwa na kiharusi baadaye ambapo kukaguliwa kutamsaidia daktari kutambua mbinu mwafaka za kupunguza uwezekano wa tatizo hili kutokea tena,” asema Dkt Kwasa.

Kulingana na NHS, katika awamu za kwanza za TIA, haiwezekani kutofautisha iwapo mwathiriwa anakumbwa na TIA au kiharusi, ndiposa inasisitizwa kwamba hata kama ishara zitatokomea, lazima umuone daktari.

Nini hasa kinachosababisha TIA?

Kulingana na Dkt Kwasa, kuna mambo kadha wa kadha yanayosababisha TIA.

“Wakati wa shambulio la TIA, mshipa mmoja wa damu unaosambaza damu iliyo na oksijeni kwenye ubongo wa mwathiriwa huziba. Hii husababishwa na mgando wa damu pengine katika sehemu nyingine ya mwili, na kusafiri kwenye mishipa inayosambaza damu kwenye ubongo,”

Hata hivyo, hali hii pia yaweza sababishwa na vipande vya mafuta (Cholestrol) au viputo vya hewa. Kuna mambo kadha wa kadha yanayoongeza hatari ya kuumbwa na TIA, ikiwa ni pamoja na uvutaji sigara, shinikizo la damu, uzani mzito, viwango vya juu vya cholesterol, kunywa pombe kwa wingi, mpigo wa moyo usio wa kawaida na kisukari.

Mara nyingi matibabu yatategemea na masuala kadha wa kadha kuhusu mhusika kama vile umri na afya.

“Mara nyingi utatakiwa kubadilisha mtindo wa kimaisha ili kuzuia hatari zaidi ya kukumbwa na kiharusi, na kupewa dawa za kutibu kinachosababisha TIA.”

Kwa mujibu wa NHS, kuna wakati ambapo huenda upasuaji kwa jina carotid endarterectomy ukahitajika ili kuzibua mishipa ya carotid arteries, ambayo ni mishipa mikuu inayosambaza damu kwenye ubongo.

Lakini mbinu mwafaka ya kukabiliana na hali hii, Dkt Kwasa asema, ni kuzuia kupata shambulio hili.

“Pasipo kuzingatia iwapo umekumbwa na TIA au kiharusi, kuna mbinu kadhaa ambazo zaweza punguza hatari ya kukumbwa na hali hizi mbili katika siku zijazo. Kwa mfano kudumisha uzani ufaao, kuhakikisha lishe bora, kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya pombe na uvutaji sigara. Pia, itasaidia ikiwa mgonjwa atapata matibabu ya matatizo mengine ya kiafya yanayoongeza hatari ya kukumbwa na hali hii, kama vile maradhi ya kisukari na shinikizo la damu,” afafanua.

Ishara za TIA

  • Ngozi kuparara
  • Kushindwa kupumua
  • Moyo kupiga kasi
  • Kutokwa kijasho baridi
  • Uchovu
  • Kisunzi
  • Maumivu begani, shingoni, mkononi, au mgongoni
  • Kichefuchefu au kutapika
  • Kukosa usingizi
  • Maumivu tumboni

You can share this post!

ODONGO: Wanasiasa wamakinike katika mchakato wa BBI

PATA USHAURI WA DKT FLO: Kiharusi cha muda huletwa na nini?