SHINA LA UHAI: Juhudi zaidi zahitajika kukabili kansa ya lango la uzazi

SHINA LA UHAI: Juhudi zaidi zahitajika kukabili kansa ya lango la uzazi

NA PAULINE ONGAJI

NI siku chache tu baada ya Kenya kumuaga aliyekuwa mtangazaji nyota wa televisheni marehemu Catherine Kasavuli, aliyefariki kutokana na maradhi ya kansa ya lango la uzazi.

Kifo chake kiliibua mjadala mkali kuhusu uwezo wa mfumo wa kitaifa wa afya kupambana na gonjwa hili, na jinsi umekuwa tishio kwa wanawake sio tu humu nchini bali ulimwenguni kote.

Takwimu za maradhi haya zimezidi kutisha ambapo kulingana na shirika la kimataifa la utafiti wa kansa, kansa ya njia ya uzazi ni ya pili miongoni mwa kansa zilizokithiri sana nchini Kenya, baada ya kansa ya matiti.

Hapa nchini, maradhi haya yamekuwa janga kiasi cha kwamba nchi hii imeorodheshwa miongoni mwa mataifa yaliyoathirika pakubwa na ugonjwa huu. Viwango vya kansa ya lango la uzazi hapa nchini ni zaidi ya visa 40 kwa kila wanawake 100,000 wanaofanyiwa uchunguzi kila mwaka.

Kulingana na Wizara ya afya, kansa ya lango la uzazi husababisha vifo vya wanawake wanane kila siku nchini Kenya, idadi ambayo ni sawa na vifo 3,286 kila mwaka.

Aidha, wanawake watatu kati ya 100 nchini Kenya wamo katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya kansa ya njia ya uzazi, huku visa 5,250 vya maradhi haya vikiripotiwa kila mwaka nchini.

Kansa ya lango la uzazi aidha husababisha vifo vingi miongoni mwa wanawake wanaogunduliwa kuwa na maradhi haya, ikilinganishwa na kansa ya matiti ambayo imekithiri sana miongoni mwa wanawake, ambapo asilimia tisa ya wagonjwa hufariki. Asilimia 12 ya wanawake wanaopatikana kuugua kansa ya lango la uzazi hufariki.

Bi Rose Adero, ni mmoja wa waathiriwa wachache wa kansa ya lango la uzazi ambao wamebahatika kupona baada ya kuugua maradhi haya.

Oktoba 2022, alipokea hakikisho kutoka kwa daktari kwamba alikuwa ameshinda vita dhidi ya maradhi haya.
Kulingana na Bi Adero, haijakuwa safari rahisi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

“Niligunduliwa kuwa na awamu ya 1B ya kansa ya lango la uzazi mwaka wa 2015, na kuanzishiwa matibabu mara moja,” asimulia.

Matibabu yake yalihusisha upasuaji, taratibu kadhaa za tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy), zilizogharimu pesa nyingi. Isitoshe, katika harakati za matibabu yake alipata pigo baada ya mumewe ambaye ni marehemu sasa kupatikana na kansa ya ini ambayo ilikuwa katika hatua ya nne. Hii ilimlazimu kusitisha matibabu yake hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa amepoteza ajira kama keshia katika mojawapo ya maduka makuu ya jumla nchini.

“Ilikuwa lazima mume wangu aanzishiwe matibabu mara moja, na hivyo hatungeweza kumudu kugharimia taratibu zetu sote,” aeleza Bi Adero.

Kuna wakati ambapo hata walilazimika kuuza baadhi ya mali waliyokuwa wamekusanya kugharamia matibabu, na hata kusitisha masomo ya watoto wao kutokana na ukosefu wa karo.

Bi Rose Adero wakati wa mahojiano nyumbani kwake mtaani Umoja, Kaunti ya Nairobi. PICHA | PAULINE ONGAJI

Lakini licha ya changamoto hizi, Bi Adero asema anashukuru kwamba hatimaye maradhi haya yamethibitishwa kupona.

“Nilibahatika kwamba yaligunduliwa katika awamu ya mwanzo.”

Hapa nchini utafiti unaonyesha kwamba ni asilimia tatu pekee ya wanawake wanaoenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kansa ya njia ya uzazi (pap smear).

Dkt Catherine Nyongesa, mtaalamu wa matibabu ya kansa jijini Nairobi, asema kwamba japo viwango vya uhamasishaji dhidi ya maradhi haya vimeongezeka, idadi ya wanawake wanaoenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi huu ingali chini.

Dkt Catherine Nyongesa, mtaalamu wa matibabu ya kansa jijini Nairobi. PICHA | MAKTABA

Anasema kwamba baadhi ya sababu ambazo zimechangia hali hii ni kwamba bado kuna wanawake wanaokumbwa na hofu kuwa huenda utaratibu huu unaambatana na maumivu au ni ghali. Aidha, kuna wale wanaohofia matokeo ya uchunguzi,” aeleza.

Kulingana na Dkt Nyongesa, uchunguzi wa pap smear hugharimu kati ya Sh1,000 katika hospitali za umma na hata kufikia Sh10,000 katika baadhi ya hospitali za kibinafsi.

“Wakati mwingine, gharama ya kufanyiwa pap smear haihusishi tu utaratibu huu kwani huenda ukahitajika kumuona daktari ili sampuli zichukuliwe na kufasiriwa,” aeleza.

Kwa Wakenya wengi, hiyo ni gharama ya juu, lakini Dkt Nyongesa asema kwamba haina budi kwa wanawake kuzingatia umuhimu wa utaratibu huu.

“Utaratibu huu ni muhimu sana kwa sababu kansa ya lango la uzazi kwa kawaida haionyeshi ishara mapema, na hii huenda ikawa njia ya kipekee ya kutambua mabadiliko ya mapema ambayo husababisha kansa,” asema.

Na kwa wale wanaobainika kuugua maradhi haya – hata iwe mapema, mzigo wa matibabu wanaokumbana nao ni mzito ajabu. Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Kansa unaashiria kwamba gharama ya matibabu inasalia kuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ugonjwa huu.

Maradhi ya kansa ya njia ya uzazi huendelea kuenea kwa hatua nne. Katika hatua ya kwanza, kansa inasambaa katika kina kwenye njia ya uzazi hadi kwenye uterasi.

Hapa, tiba inahusisha upasuaji unaojulikana kama hysterectomy ambapo sehemu au uterasi yote inaondolewa.

Hatua ya pili inahusisha seli za kansa kuenea mbali kwenye njia ya uzazi na hata kufikia sehemu ya uke. Hapa, tiba huhusisha tibakemia na tibaredio.

Katika hatua ya tatu, maradhi haya huwa yameenea hadi kwenye ukuta wa fupanyonga na huenda unachukua asilimia 33 ya sehemu ya uke na hata kusababisha figo kuvimba na kutatiza au hata kusitisha kabisa shughuli za kiungo hiki.

Hapa pia, utaratibu wa tiba unahusisha tibakemia na tibaredio.

Hatua ya nne na ya mwisho ni mbaya zaidi ambapo huenea hadi kwenye kibofu cha mkojo na hata kuathiri vinundu vya limfu na baada ya muda huenea katika sehemu zingine za mwili.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyakazi wa kaunti wakaa njaa kwa miezi 2 sasa

Mbunge wa zamani apongeza vijana kwa kuweka akiba hadi...

T L