Makala

SHINA LA UHAI: Kasoro ya kimaumbile imemnyima shangwe maishani

October 6th, 2020 4 min read

Na PAULINE ONGAJI

ALIGUNDUA kwamba hakuwa na viungo vya uzazi akiwa na umri wa miaka 17.

Naam, Julian Peters, alizaliwa bila viungo vya mfumo wa uzazi, yaani uterasi, lango la uzazi na uke.

Julian anakumbwa na hali inayofahamika kama Mayer-Rokitansky-Küster-Hauser (MRKH), ambapo mwanamke anazaliwa akiwa na sehemu za uzazi ambazo hazijakomaa, au hazipo kabisa.

Ni tatizo alilogundua baada ya kupigwa picha za skeni, na japo amefanyiwa upasuaji mara kadhaa ili kuunda njia kwenye sehemu ya uke, hawezi pata watoto.

Hali hii imemsababishia mateso na majonzi ambapo anakumbuka mara kadha wa kadha, ametengwa na kukataliwa na wachumba kutokana na udhaifu wake.

“Kuna watu ambao mwanzoni walihusisha hali yangu na uavyaji mimba au ushirikina,” aeleza.

Lakini kwa Julian, japo ilimchukua muda kukubali hali yake, amejifunza kujipa nguvu na kujikubali jinsi alivyo.

MRKH ni kasoro ya kuzaliwa ambapo mfumo wa uzazi wa msichana haujakua vilivyo, au haupo kabisa.

Ulimwenguni, hali hii huathiri takribani mmoja kati ya wanawake 4,500. Hapa nchini Kenya, hakuna takwimu kamili zinazoonyesha idadi ya watoto wasichana wanaozaliwa wakiwa na kasoro hii.

Kulingana na Dkt Jemimah Kariuki, mtaalamu wa masuala ya uzazi na mwanajinalokojia, kwa wasichana wanaokumbwa na hali hii ambayo pia inafahamika kama vaginal agenesis, ni kawaida kwao kuwa na uterasi ndogo au kutokuwa nayo kabisa. Aidha, huenda mwathiriwa pia akakosa lango la uzazi.

Kwa kawaida mfumo wa uzazi huanza kujiunda katika miezi michache ya kwanza ya uhai wa kijusi. Hii inahusisha ogani za uzazi; uterasi, lango la uzazi, uke, ‘fallopian tubes’, na ovari.

Kulingana na Dkt Kariuki, MRKH hutokea mfumo wa uzazi unapokosa kukamilika kujiunda au kutokuwepo kabisa. “Hali hii inapotokea, huenda uke ukawa mfupi au mwembamba kuliko kawaida. Ovari (ogani zinazounda homoni kwa kawaida zinakuwa za kawaida),” anasema.

Pengine unajiuliza ni vipi Bi Julian aligundua tatizo hili akiwa na miaka 17?

Kulingana na Dkt Kariuki, kwa kawaida wasichana wanaokumbwa na MRKH hupitia awamu ya kubalehe sawa na vijana wengine, na hata wanaonyesha ishara zingine za kubalehe kama vile kuota nywele katika sehemu za siri, na hata matiti kuwa makubwa.

“Kwa hivyo ni nadra kwa mhudumu wa kiafya kushuku kuwepo kwa tatizo mapema kabla ya mwathiriwa kutimu umri huu,” aeleza.

Kulingana na wataalamu, umri wastani wa hali hii kutambulika ni kati ya miaka 15-18. “Wasichana au wanawake wanaokumbwa na hali hii hawashuhudii hedhi kutokana na sababu kuwa uterasi haipo. Kwa kawaida, ishara ya kwanza ya hali hii ni kwamba mwathiriwa hatoshuhudia hedhi kufikia miaka 16 (primary amenorrhea),” aeleza Dkt Kariuki.

Aidha Dkt Kariuki asema kwamba, mara nyingi, msichana atapelekwa kwa daktari katika umri huu ikiwa hajashuhudia hedhi kwa mara ya kwanza.

Aidha, sio kawaida kwa ukaguzi/uchunguzi wa nyonga kufanywa wakati wa kuzaliwa au katika umri wa utotoni, kumaanisha kwamba sio rahisi kwa hali hii kutambuliwa kabla ya umri wa kubalehe.

Ikiwa mhudumu wa kiafya atafanya ukaguzi wa ndani ya uke wa mwathiriwa, huenda tatizo likagundulika mara moja. “Kuna wakati mwingine ambapo msichana atashauriwa akaguliwe na mwanajinakolojia ambapo atafanyiwa ukaguzi kama vile picha za ultrasound kwenye nyonga au za MRI (magnetic resonance imaging), ili kuthibitisha ikiwa uterasi yaweza onekana au la.

Mbali na taratibu hizi, wakati mwingine uchunguzi wa damu pia waweza fanywa ili kuthibitisha jeni za kike (karyotype) za kawaida, vile vile utendakazi wa ovari.

TIBA

Kwa mujibu Chama cha madaktari wa uzazi na wanajinakolojia nchini Amerika (American College of Obstetricians and Gynecologists), matumizi ya vitanuzi, vifaa vya kutanua uke (vaginal dilators), hutumika kama mbinu ya kwanza ya matibabu.

Kulingana na wataalamu hawa, mbinu hii ni mwafaka kwani mwanamke mwenyewe anaweza jifanyia kwa siri tena akiwa nyumbani mwake.

Kwa kawaida vifaa hivi huingizwa katika sehemu ya uke ili kuipanua sehemu hii, pamoja na njia ya uzazi.

Lakini kabla ya kufanya hivi, wataalamu hawa wanasema kwamba lazima mwathiriwa akaguliwe na mwanajinakolojia ili apate ushauri kuhusu jinsi ya kukitumia vyema na hivyo kuzuia uharibifu katika sehemu hii.

Wanasema kwamba kama mwathiriwa, unapaswa kuhakikisha unatumia aina hii ya tiba kwa kumwendea mwanajinakolojia ambaye kazi zake za awali zinatambulika.

Wataalamu wa masuala ya uzazi wanasema kwamba aina ya kwanza ya kitanuzi inatoshana na saizi ya kisodo cha kuingizwa ukeni, ambapo kuanzia na saizi ndogo kabisa ya kifaa hiki, msichana atajifunzia kukishika na kukishinikiza ili kupanua uke.

“Baadaye, jinsi uke unavyoendelea kupanuka, saizi kubwa ya kitanuzi yaweza tumika baadaye. Kwa kawaida, aina hii ya tiba ina matokeo mazuri, ila itategemea na masuala kadha wa kadha, kama vile mafunzo na utaalamu wa wahudumu wa kiafya wanaowafunza waathiriwa kuhusu matumizi ya kifaa hiki,” asema Dkt Gillian Rose, mwanajinakolojia katika Hospitali ya Queen Charlotte’s and Chelsea, nchini Uingereza.

Kulingana naye, ni muhimu kuzingatia kwamba matumizi ya kifaa hiki yanapaswa kukaguliwa kila wakati, kumaanisha kwamba sharti mwathiriwa achunguzwe na mwanajinakolojia angaa mara mbili kwa mwezi.

Mbali na matumizi ya kifaa hiki, kuna tiba ya upasuaji unaofahamika kama vaginoplasty, utaratibu ambao hufanywa hasa ikiwa hali ya mwathiriwa ni mbaya zaidi.

Upasuaji unahusisha kutumia tishu kutoka sehemu zingine za mwili ili kuunda sehemu ya uke. Hapa, kipandikizi cha ngozi kutoka sehemu nyingine ya mwili kama vile matumbo na makalio, kinatumika kuunda uke.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba mwathiriwa bado atalazimika kutumia vitanuzi. “Hii inamaanisha kwamba upasuaji sio suluhu ya haraka, au mbinu ya kuepukana na matumizi ya vitanuzi,” aeleza Dkt Rose.

Aidha, wataalamu wanasisitiza kwamba mbinu hii ya matibabu inapaswa kuwa tu chaguo la mwisho, endapo matumizi ya vitanuzi hayatafanikiwa.

Kulingana na Dkt Kariuki, MRKH sio maradhi ya kurithiwa au hayatokani na jeni. “Ni kasoro ya kuzaliwa inayotokea kijusi kinapoendelea kukua tumboni. Hakuna kinachosababisha hali hii, na hakuna kitu chochote ambacho mama mjamzito anaweza fanya ili kuzuia hali hii kumkumba bintiye,” aeleza.

Kulingana na Dkt Rose, licha ya tatizo hili, kuna uwezekano wa muathiriwa kufurahia tendo la ndoa maishani. “Kwa kawaida, wanawake hawahisi uchungu wakati wa tendo la ndoa baada ya kutibiwa. Na ikiwa hii itafanyika, basi huenda mhusika akahitajika kutumia mafuta yanayotumika kulainisha sehemu hii wakati huu,” aeleza.

Lakini mtaalamu huyu anasema kwamba uamuzi huu pia utakuwa baada ya kupata ushauri kutoka kwa mwanajonakolojia.

Kuhusu ikiwa mwathiriwa atakuwa na uwezo wa kupata watoto katika siku zijazo, wataalamu wanasema kwamba ikiwa umezaliwa bila uterasi au ikiwa sehemu hii ni ndogo, haitawezekana kushika mimba.

“Hata hivyo ikiwa ovari zake ni za kawaida na zinaweza unda mayai, basi mayai yake yaweza tungishwa kupitia mbinu za kitaalamu. Ikiwa alizaliwa bila uke lakini ana uterasi ya kawaida, kuna uwezekano kwamba atashika mimba kwa usaidizi wa mbinu za kisasa kama vile in-vitro fertilization-IVF,” asema Dkt Rose.

Kulingana na Dkt Rose, kuna wazazi ambao huenda wakajawa wasiwasi pindi wanapogundua kwamba binti yao anakumbwa na hali hii.

Kama mzazi, asema, unapaswa kutambua kwamba uamuzi wa kupokea matibabu na wakati wa kufanya hivyo unapaswa kuwa wa mwathiriwa.

“Kumbuka kwamba, kama mzazi au mlezi ungependa binti yako kuangazia suala hili mapema iwezekanavyo ili kumsaidia kutatua shida hii. Lakini kutokana na sababu kuwa ni mwili wa mhusika, yeye mwenyewe anapaswa kudhibiti utaratibu atakaofanyiwa na wakati upi.”

Mbali na hayo, anasema kwamba ni kawaida kwa wasichana wanaokumbwa na hali hii kuwa na mabadiliko ya muda ya mihemko na tabia, huku wakijaribu kuelewa matatizo ya kimwili yanayowakumba.

Hata hivyo huenda wasiwasi huu ukapungua muda unavyozidi kusonga huku mwathiriwa akiendelea kupokea matibabu.