Makala

SHINA LA UHAI: Mbu ‘wapya’ wanaotishia wakazi mijini

September 22nd, 2020 4 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKATI wa likizo ya Aprili mwaka 2019 Jane Wesonga ambaye ni mkazi wa Githurai, jijini Nairobi, aliwapeleka binti zake wawili katika eneo la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma kumtembelea babu yao.

Baada ya siku mbili, mmoja wa binti zake Juliet, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Roysambu, Nairobi, alikataa kula na mwili wake ulikuwa na joto jingi.

“Mwanzoni tulidhani kwamba huo ulikuwa uchovu wa safari kwani hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri mbali kutoka Nairobi,” anakumbuka Bi Wesonga.

“Siku nne baadaye, hali yake ilidorora na tukaamua kufunga safari ya ghafla na kurejea jijini Nairobi ili nimpeleke hospitalini,” anaongezea.

Walipowasili walifululiza hadi katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki na alipopimwa alipatikana na malaria.

“Lakini alikata roho saa chache baada ya kuwekewa chupa ya maji. Na huo ndio ulikuwa mwisho wa binti yangu, Juliet. Madaktari waliniambia kuwa kama ningempeleka mapema katika hospitali za huko Bungoma, nisingempoteza kwani malaria huhitaji matibabu ya haraka,” anasema huku uso wake ukionekana kujawa na huzuni.

Juliet ni miongoni mwa zaidi ya Wakenya 23,000, wengi wao wakiwa watoto, waliofariki kutokana na malaria mwaka jana. Alikuwa miongoni mwa visa milioni 4.7 vya waathiriwa wa malaria vilivyoripotiwa.

Wakenya milioni 4.7 waliugua malaria, kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi ya 2020 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Asilimia 74 ya visa vya waathiriwa wa malaria vilitokea katika ukanda wa ziwa, unaojumuisha Kaunti za Kisumu, Siaya, Migori, Homa Bay, Kakamega, Busia, Bungoma na Vihiga. Watu 366 kati ya 1,000 waliugua malaria.

Jiji la Nairobi ambalo limeorodheshwa miongoni mwa maeneo salama, lilikuwa na visa 90,183 vya malaria. Wataalamu wanasema kuwa vingi vya visa hivyo vinatokana na watu wanaosafiri kutoka maeneo yaliyo na maambukizi ya juu kama vile Magharibi mwa Kenya.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa Wakenya wanaoishi katika maeneo yaliyo na visa vichache vya malaria huwa na kinga dhaifu – miili yao haina uwezo wa kukabiliana na viini vya malaria.

Watu wanaoishi Nairobi, kwa mfano, huwa hatarini wanapozuru maeneo ambapo malaria imekolea.

Watafiti wanasema kuwa mbu jike ambaye hueneza malaria nchini Kenya, anayejulikana kama Anopheles gambiae, anapendelea zaidi maeneo ya vijijini kuliko mijini.

Aina hiyo ya mbu ambao husababisha vifo vya zaidi ya Wakenya 23,000 kila mwaka kutokana na maradhi ya malaria ‘hawapendi’ maeneo ya mijini.

Mbu aina ya Anopheles gambiae ndio hueneza malaria kote barani Afrika.

Tafiti zinaonyesha kuwa aina hiyo ya mbu hawajajifunza jinsi ya kuzaana katika matenki ya kuhifadhia maji ndani na nje ya nyumba ambayo hupatikana kwa wingi katika maeneo ya mijini.

Kulingana na wataalamu, mbu hao pia hukumbwa na changamoto ya kuzaana kwenye vyanzo vya maji machafu kama vile Mto Nairobi ambao umesheheni kemikali na takataka za kila aina na huzaana kwa wingi kwenye vyanzo vya maji safi.

Mbu wapya

Hata hivyo, wataalamu sasa wanaonya kuwa maeneo ya mijini, yakiwemo majiji ya Mombasa na Nairobi, huenda yakavamiwa na aina ‘mpya’ ya mbu anayejulikana kama Anopheles stephensi.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza umebaini kuwa Mombasa na Nairobi ni miongoni mwa majiji 44 barani Afrika yaliyo katika hatari ya kuvamiwa na mbu hao hatari wanaopendelea maeneo ya mijini.

Malaria iliua zaidi ya watu 400,000, barani Afrika mnamo 2018, wengi wao wakiwa watoto. Malaria husababishwa na aina 40 ya viini ambavyo husambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine wakati wa kunyonya damu.

Mbu wa Anopheles stephensi wanapatikana zaidi bara Asia, haswa mataifa ya China na India na waliripotiwa kwa mara ya kwanza barani Afrika mnamo 2012.

Mbu hao walivamia jiji la Djibouti kabla ya kusambaa katika nchi za Sudan na Ethiopia. Aidha walithibitishwa kuwepo nchini Ethiopia mwaka jana.

Lakini utafiti wa kusaka mbu hao ulianza mnamo 2016 na uliendeshwa na Chuo Kikuu cha Jigjiga cha Ethiopia.

Mbu hao wamejifunza kutaga mayai na kuzaliana kwenye matenki na vyombo vya kuhifadhia maji ndani na nje ya nyumba za mijini.

“Hii ndiyo aina ya mbu walio na uwezo wa kuzaana na kueneza ugonjwa wa malaria katika maeneo ya mijini,” inasema ripoti ya utafiti huo.

Kulingana na utafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford, mbu hao sasa huenda wakasababisha watu milioni 126 zaidi kuwa katika hatari ya kuambukizwa malaria barani Afrika.

Asilimia 40 ya watu barani Afrika huishi katika maeneo ya mijini.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 14.8 wanaishi katika maeneo ya mijini humu nchini, kwa mujibu wa sensa ya 2019.

Tofauti na mbu wanaopatikana barani Afrika ambao hupendelea ‘kuuma’ watu gizani usiku wakiwa usingizini, hawa huuma zaidi nyakati za jioni kabla ya kulala hivyo kufanya vyandarua kukosa kazi.

Mbali na mijini, mbu hao pia wanaweza kuzaana katika maeneo ya vijijini na iwapo watawasili humu nchini, idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwa kiasi kikubwa.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford wanasema kuwa iwapo watavamia Kenya, watu watalazimika kuweka vyandarua madirishani na milangoni kuwazuia kuingia ndani ya nyumba.

“Mbinu nyingine ya kuwaangamiza ni kufunika matenki ya maji yaliyoko nje au ndani ya nyumba. Mbinu hii imesaidia pakubwa taifa la India kukabiliana na mbu hao hatari,” anasema Dkt Marianne Sinka wa Chuo Kikuu cha Oxford aliyeongoza watafiti hao.

“Mbu hao wanaishi katika mazingira sawa na mbu aina ya Aedes aegypti ambao husababisha viini vinavyosababisha homa ya manjano na Zika. Mbinu zilizotumika kuwadhibiti zinaweza kutumiwa kukabiliana na Anopheles stephensi,” anaongezea.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford walilinganisha hali ya hewa kama vile joto na mvua, wakabaini kuwa Ethiopia ina sifa sawa na Kenya.

“Iwapo mbu aina ya Anopheles stephensi watavamia miji muhimu kama vile Mombasa, Nairobi, Dar es Salaam (Tanzania) na Khartoum (Sudan), vifo vinavyotokana na malaria huenda vikaongezeka maradufu na kurejesha nyuma hatua zilizopigwa kukabiliana na maradhi hayo,” linasema shirika la WHO.

Kulingana na utafiti huo, mbu hao huenda wakawasili humu nchini kupitia vyombo vya usafiri.

Shirika la WHO mwaka jana lilionya kuhusu kuwepo kwa mbu hao na kwamba iwapo watasambaa katika mataifa yote ya Afrika, visa vya maambukizi ya malaria vitaongezeka maradufu.