Makala

SHINA LA UHAI: Mkurupuko wa homa ya Corona ni nini na utaepukaje?

February 11th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

KENYA ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyo katika hatari kubwa ya kupatwa na maambukizi ya homa ya Corona ambayo imeua zaidi ya watu 1,018 nchini China.

Kulingana na wataalamu, mipaka ya Kenya na mataifa jirani ‘imetoboka’ hali ambayo huenda ikasababisha wageni walio na homa ya Corona kuingia humu nchini bila kutambuliwa.

Wanasema ukosefu wa mipango kabambe ya kuwatenga na kuwatibu wagonjwa pia inaweka Kenya hatarini.

Mtandao wa Prevent Epidemics, preventepidemics.org, ambao hutumia takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kutathmini ikiwa nchi imejiandaa kukabiliana na mkurupuko wa maradhi, unasema kuwa Kenya imefikia asilimia 50 ya mambo yaliyomo kwenye mwongozo wa WHO kuhusu hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kukabiliana na homa ya Corona.

Nchi zinafaa kutimiza angalau asilimia 80 ili kuchukuliwa kwamba imejiandaa kikamilifu kukabiliana na mkurupuko wa maradhi.

Kwa mfano, mwongozo wa WHO unasema kuwa kunapotokea mkurupuko wa maradhi hatari duniani, serikali inafaa kuchukua hatua za dharura na kuhakikisha kuwa wageni wanaoingia nchini kupitia bandarini, viwanja vya ndege na mipaka ya nchi kavu wanapimwa kikamilifu.

Mwongozo wa WHO pia unahitaji kuwepo kwa madaktari waliohitimu, vifaa na dawa ya kutosha kukabiliana na maradhi hayo.

Kenya imekuwa ikipeleka sampuli za watu wanaoshukiwa kuwa na homa hiyo ili kufanyiwa vipimo vya kina nchini Afrika Kusini. Hali hiyo, wataalamu wanasema, ni ithibati kwamba Kenya haijajiandaa kikamilifu.

Kenya hupokea angalau ndege tatu kutoka China kwa siku na serikali iliagiza kuwa wageni wote wapimwe wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege.

Lakini wataalamu wanasema kuwa maradhi hayo yanaweza kuingia humu nchini kupitia mipaka ya kati ya Kenya na mataifa jirani kama vile Tanzania, Sudan Kusini, Uganda, Ethiopia na Somalia.

Serikali ya Kenya, hata hivyo, imeshikilia kuwa mikakati imewekwa kukabiliana na homa hiyo.

“Tunawahakikishia Wakenya kwamba nchi ingali haina kisa cha mwathiriwa wa virusi vya Corona na tumeweka mikakati mwafaka kuhakikisha kuwa maambukizi hayafiki humu nchini,” wizara ya Afya iliambia wanahabari Januari 31.

Shirika la WHO tayari limetangaza hali ya dharura duniani kufuatia mkurupuko huo ulioanzia jijini Wuhan, China.

Watu zaidi ya 40,000 wameripotiwa kuugua homa hiyo kote duniani. Wengine zaidi ya 3,000 wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Watu wasiozidi watatu wameripotiwa kufariki kutokana na homa hiyo nje ya China.

Ufilipino, mnamo Februari 2, ilitangaza kifo cha mwathiriwa wa homa hiyo. Hong Kong ambalo linajitegemea licha ya kuwa chini ya China lilithibitisha kifo cha kwanza cha mwathiriwa wa homa hiyo Jumanne, wiki iliyopita.

Homa hii imesambaa kwa idadi kubwa zaidi kuliko Homa ya Mfumo wa Kupumua (SARS) iliyoanzia China na kuzua hofu duniani kati ya 2002 na 2003.

Homa ya Corona ni nini?

Kulingana na WHO, Corona ni mkusanyiko wa virusi ambavyo husababisha maradhi kama vile mafua na magonjwa hatari kama vile homa ya mfumo wa kupumua.

Virusi hivyo vinaaminika kuambukizwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu.

Watafiti wanaamini kuwa virusi vinavyosababisha homa hiyo vimetoka kwa popo au nyoka.

Virusi vilivyotokana na homa ya SARS, kwa mfano, vinaaminika kutoka kwa aina fulani ya paka wa porini.

“Kuna mamilioni ya aina ya virusi wanaoambukizwa kutoka mnyama mmoja hadi mwingine lakini havijafika kwa binadamu,” linasema shirika la WHO.

Jina corona linatokana na lugha ya Kilatino kumaanisha kofia. Wanasayansi wanasema kuwa virusi vinavyosababisha homa vina umbo la kofia vinapoangaliwa kwa kutumia darubini.

Dalili za homa ya Corona

Kulingana na WHO, mtu aliye na virusi vya Corona anahisi joto, kukohoa, kuhisi kupungukiwa na pumzi na kupumua kwa shida.

Virusi hivyo pia vinaweza kusababisha ugonjwa wa nimonia, kufeli kwa figo na hata kifo.

Muda ambao virusi hivyo huchukua mwilini kabla ya dalili kuanza kujitokeza haujulikani. Lakini madaktari wanaamini kuwa dalili za maradhi hayo hujitokeza baada ya kati ya siku 10 na 14.

Corona sasa imepiku SARS iliyosababisha vifo vya watu 800 kote duniani, wakiwemo 300 nchini China kati ya 2002 na 2003.

Visa vingi vya waathiriwa vimeripotiwa katika mkoa wa Hubei, nchini China.

Juhudi za kupata chanjo zinaendelea huku madaktari wakisema kuwa kinga hiyo huenda ikaanza kusambazwa kote duniani kabla ya mwaka kesho.

Serikali ya China tayari imepiga marufuku kutoka na kuingia jijini Wuhan lililo katika mkoa wa Hubei.

Mataifa mbalimbali yamekuwa yakiendelea na juhudi za kuokoa raia wake kutoka maeneo yaliyoathiriwa na virusi hivyo hatari ikiwemo Amerika.

Jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona

1. Wizara ya Afya inashauri watu kunawa na kuepuka baadhi ya vyakula haswa wanyamapori.

2. Epuka kugusana na watu wanaougua maradhi ya mapafu yasiyojulikana.

3. Epuka kugusana na wanyama wa porini.

4. Funika mdomo wakati wa kukohoa au

kupiga chafya na kisha unawe mikono.

5. Watu walio na joto jingi, wakohoa, wana ugumu wa kupumua na kupiga chafya na walizuru China hivi karibuni, wakimbizwe hospitalini.

Tahadhari zilizowahi kutolewa na WHO kuhusu maradhi hatari

Shirika la WHO limewahi kutangaza hali ya dharura ya kiafya mara tano tangu kupewa mamlaka hayo mnamo 2005.

Shirika hilo lilitangaza hali ya hatari duniani kufuatia mkurupuko wa maradhi ya homa ya nguruwe (Swine Flu) ambayo yaliambukiza kati ya watu 123,000 na 575,400 mnamo 2009.

Shirika hilo lilitangaza hali ya hatari tena 2014 kufuatia mkurupuko wa maradhi ya kupooza (polio).

Mwaka huo huo pia WHO ilitangaza ugonjwa wa Ebola kuwa hatari duniani baada ya kuangamiza watu 11,000 na kuambukiza watu 30,000 katika mataifa ya Afrika Magharibi kati ya 2014 na 2016.

Mnamo 2016, ugonjwa wa Zika ulikurupuka na kusambaa kwa kasi Amerika hivyo kulazimu WHO kuutangaza kuwa hatari duniani.

Mwaka 2019 WHO ilitangaza Ebola kuwa janga la kimataifa baada ya kuangamiza watu kadhaa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).