SHINA LA UHAI: Mto Ewaso Ng’iro hatarini kukauka

SHINA LA UHAI: Mto Ewaso Ng’iro hatarini kukauka

Na PAULINE ONGAJI

UNAPOTAZAMA kwa umbali utadhani kwamba hili ni jangwa.

Mchanganyiko wa matope na mchanga kwenye ardhi tambarare ambayo awali ilikuwa imefunikwa kwa maji ya Mto Ewaso Ng’iro.

Katika sehemu hii iliyoko eneo la Archer’s Post, Kaunti ya Samburu, limekuwa jambo la kawaida kukumbana na vijana wakipakia kwenye malori mchanga kutoka mtoni.

Kwa miaka sasa, uchimbaji mchanga katika sehemu hii umekithiri, huku wafanyabiashara kutoka sehemu za mbali kama vile Meru na hata jijini Nairobi, wakifurika humo ili kupata bidhaa hii muhimu.

Haya yakijiri, mawe na mchanga kwenye ukingo wa mto huu yanaendelea kumomonyoka na sehemu hiyo ikiendelea kukumbwa na uchafuzi wa maji na hewa, unaoathiri uhai wa mimea na viumbe.

Kulingana na John Lemasa, msimamizi wa kikundi cha uhifadhi wa wanyamapori cha Kalama katika Kaunti ya Samburu, athari zinazotokana na uchimbaji mchanga katika sehemu hii ni dhahiri.

John Lemasa, msimamizi wa kikundi cha uhifadhi wa wanyamapori cha Kalama akiwa katika Archer’s Post, Kaunti ya Samburu. Nyuma yake ni sehemu ya Mto Ewaso Ng’iro ambao unakauka huku lori la mchanga likionekana. Picha/ Hisani

“Viwango vya maji katika mto huu vimekuwa vikipungua, ilhali mmonyoko wa mawe na mchanga umesababisha mtiririko wa maji kuzidi kupungua. Na japo mtiririko huu umekuwa ukitegemea misimu, hatari ya mto kukauka kabisa iko wazi ,” anasema.

Takwimu zinaonyesha kwamba kumekuwa na upungufu wa maji ya mto katika eneo hili la Archer’s Post katika mwezi wa Februari (ambao ndio wa kiangazi zaidi), kutoka mita tisa mchemraba (9m3) kwa kila sekunde katika miaka ya sitini, hadi chini ya mita moja mchemraba (1m3) kwa kila sekunde, katika miaka ya 2000.

Lakini japo hatari hii inaendelea kuonekana, Bw Lemasa asema kwamba uchimbaji mchanga bado utaendelea.

“Mbali na kuwapa kazi vijana wengi wasio na ajira, asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hili wamepuuza ukweli kwamba shughuli hii huenda ikaathiri uwepo wa mto huu na hatimaye maisha yao,” aongeza.

Lakini ukosefu wa ufahamu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mto huu, hauonekani kuwa tatizo la eneo hili pekee. Ni changamoto ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika maeneo ya Mlima Kenya na safu ya Aberdare, sehemu ambapo Mto Ewaso Ng’iro huanzia, hadi katika kaunti zote saba zinazoathiri uhai wake.

Mto huu umegawanywa kwa mabonde mawili: bonde la juu (upper catchment area), na bonde la chini (lower catchment area). Bonde la juu la mto huu linapitia katika kaunti za Nyandarua na Laikipia, ilhali bonde la chini linapitia Kaunti za Samburu, Isiolo na Wajir. Kwa upande mwingine, kaunti za Nyeri na Meru, zina vijito vinavyomwaga maji yake mtoni.

Kulingana na John Mwangi, mwanasayansi mtafiti na msimamizi wa rasilimali za maji katika kituo cha Center for Training and Research in Asal -CETRAD, mto huu ni tegemeo kuu kwa jamii zinazoishi kwenye mabonde haya.

“Katika bonde la juu, mto huu ni chanzo cha maji kwa wakulima wadogo. Katikati, ni chanzo cha maji kwa wakulima wakubwa. Kwa upande mwingine, katika bonde la chini, ni tegemeo kwa jamii za wafugaji,” afafanua.

Bw Mwangi anasema mbali na athari za mabadiliko ya hali ya anga ambazo zimejitokeza kupitia violezo tofauti vya mvua, mabadiliko ya mtiririko wa maji ya mto na vyanzo vyake, yametokana na kubadilika pakubwa kwa mifumo ya matumizi ya ardhi.

“Vipande vikubwa vya ardhi vilivyonuiwa kutumika kwa ufugaji mifugo, vimegawanywa zaidi, kubadilishwa na kuwa mifumo midogo ya unyunyuziaji maji mashamba. Mabadiliko haya yamesababisha matumizi mengi ya maji ili kufanikisha aina hii ya kilimo katika kipindi chote cha mwaka,” afafanua.

Aidha, asema kwamba mabadiliko yanayoshuhudiwa ni kutokana na ongezeko la viwango vya kilimo biashara cha matunda na maua hasa kati ya miaka ya tisini na elfu mbili, yaliyosababisha ongezeko la visa vya ukusanyaji maji kutoka mitoni.

“Haja ya kukuza vyakula zaidi imesababisha uvamizi wa ardhi ya misitu na ukataji miti kwa minajili ya kuni na mbao na kuharibu kabisa vyanzo vya mto huu. Katika bonde la chini, sehemu zinazozingira vyanzo vyake zimebadilishwa na kutumika kama malisho ya mifugo hasa wakati wa misimu ya kiangazi na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa,” aeleza.

Kiongozi wa jamii katika eneo la Ziwa Olboisat (ambalo ni chanzo cha Mto Ewaso Ng’iro) katika Kaunti ya Nyandarua Thomas Ndiritu Macharia, anasema kwamba uvamizi wa sehemu zinazozingira ziwa hili kwa minajili ya kutoa makazi, ulianza katika miaka ya sabini na kuongezeka hata zaidi katika miaka ya tisini.

“Uvamizi huu umekuwa na athari kubwa kwa uhai wa mimea na viumbe katika eneo hili, huku viwango vya maji vya ziwa hili vikiendelea kupungua,” anaeleza.

Kulingana na Mary Waithera, afisa mkuu wa utalii na maliasili katika Kaunti ya Nyandarua, uvamizi huu umekuwa changamoto katika juhudi za kuhifadhi mto Ewaso Ng’iro na vyanzo vyake, huku visa vya wakulima wadogo kuvuta maji kwa mabomba moja kwa moja kutoka mlimani, vikiendelea kuongezeka.

Visa hivi vimesababisha wasiwasi mkuu miongoni mwa washikadau wengi katika bonde la Ewaso Ng’iro na kusababisha baadhi yao kuchukua hatua ili kukabiliana na tatizo hili.

Kwa mfano, Mohamed Liban, mwenyekiti wa Halmashauri ya Ustawi wa Bonde la Kaskazini la Mto Ewaso Ng’iro -ENNDA, anasema tayari wameunda upya baadhi miundo misingi ya maji iliyokuwa imeharibiwa na mafuriko ufuoni, na inapanga kujenga vifaa vya kuhifadhi maji ya mafuriko kwa matumizi wakati wa ukame.

“Kwa upande wetu kama Kaunti ya Nyandarua, tumehusika katika harakati za upanzi wa miti, huku tukiendelea kukuza tabia ya uhifadhi wa mazingira miongoni mwa watoto wanaoenda shuleni. Tumelenga kupanda takriban miti milioni mbili,” aongeza Bi Waithera.

Lakini hilo pekee halitoshi. Ili kukabiliana vilivyo na changamoto zilizopo na kurejesha hali ya awali ya Mto Ewaso Ng’iro, mbali na shughuli za kawaida zinazohusisha uhifadhi na ulinzi wa mabonde ya mto huu, Bw Liban anasema kwamba uhamasishaji wa jamii ni muhimu.

“Tatizo kubwa hata zaidi ni kuunganisha jamii tofauti zinazotegemea mto huu ili kuwa na nia moja ya kuuhifadhi,” asema.

Kwa mfano, mara kadha wa kadha, Gavana wa Kaunti ya Nyandarua, Francis Kimemia, amezungumzia kuhusu suala la manufaa ya uhifadhi wa mto huu kwa wakazi wa bonde la juu.

“Changamoto kuu imekuwa kushawishi jamii zinazoishi katika bonde la juu la mto kuelewa kwamba uhifadhi sio tu kwa manufaa ya jamii za bonde la chini, bali wao pia. Watu hapa wanadhani kwamba wanashughulikia uhifadhi wa mto sana kwa manufaa ya watu wengine. Swali ambalo limekuwa likichipuka mara nyingi ni je, nitanufaika vipi kwa kujishughulisha na uhifadhi huu? Ni suala ambalo lazima tulijadili,” asema Bi Waithera.

Kwa upande mwingine, kuna baadhi ya watu katika jamii zinazoishi katika bonde la chini wanaoamini kwamba hakuna aliye na haki ya kujigamba kwamba amehusika pakubwa katika uhifadhi wa mto huu.

Abdullahi Huka, mfugaji kutoka eneo la Malka Daka, Kaunti ya Isiolo, anaashiria jinsi suala hili la uhifadhi wa mto huu limekuwa mtihani mkubwa.

Anaamini kwamba maji ya mto yanatoka kwa mwenyezi Mungu, na hivyo hakuna watu walio na haki ya kuyatumia zaidi ya wengine.

“Tatizo ni kwamba kuna baadhi ya wakulima katika bonde la juu ambao licha ya kufurahia mvua ya kutosha, bado wanaziba mtiririko wa maji ya mto kwa minajili ya kilimo. Tayari maji hayafiki sehemu yaliokuwa yakifika miaka michache iliyopita,” asema.

Kauli ya Huka inaakisi maoni ya wafugaji wengi katika eneo la Isiolo na sehemu za bonde la chini la mto.

Na huku mjadala kuhusu nani anayepaswa kulaumiwa, au nani aliye na haki zaidi ya kunufaika na maji yake ukiendelea, suala kuu linasalia kuunganisha jamii zote zinazonufaika, ili kuafikia lengo la kuuhifadhi.

Ni mzozo ambao umeathiri matumizi ya rasilimali za bonde la mto na hata kusababisha maafa.

Abdia Mohamud kutoka Isiolo Peace Link, shirika linalohusika na masuala ya usalama katika jamii za wafugaji, anasema kwamba ghasia miongoni mwa jamii hizi zimeendelea kutokana na upungufu wa rasilimali za mto huu.

“Aidha, visa vya migogoro ya kimipaka vimeendelea kuripotiwa, huku idadi ya bunduki haramu katika jamii hizi, ikiongezeka,” afichua.

Kwa hivyo suluhisho ni lipi?

Kulingana na Bw Liban, suluhiso limo katika ushirikiano na majadiliano baina ya washikadau kuhusu uhifadhi wa mto, vile vile uhamasishaji wa jamii zote zinazonufaika.

“Kulaumiana au kujipiga kifua kamwe hakutatufaidi na tunapozidi kufanya hivi ndivyo tunavyozidi kupoteza muda, na kufumba kufumbua, tutajipata tumeupoteza kabisa,” asikitika.

Hii ndio sababu shirika la ENNDA limeanzisha mradi wa kila mwaka wa ‘Camel Caravan’ ili kuunganisha jamii husika katika mjadala kuhusu uhifadhi wa mto huu.

“Mradi huu unahusisha kuleta pamoja jamii zinazoishi katika mabonde yote ya Mto Ewaso Ng’iro,” anasema.

Bw Liban anasema tayari wamezuru kaunti kadhaa ikiwa ni pamoja na Isiolo, Laikipia na Samburu katika harakati za kurejesha hali ya awali ya mto huu.

“Tunapanga kuandaa mikutano ya jamii kutoka kaunti zote ambapo mto unapitia pamoja na vyanzo vyake, ikiwa ni pamoja na eneo la Ziwa Olboisat,” aashiria.

pongaji@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Lukaku alivyofufua makali yake nchini Italia na kusaidia...

Mchecheto PSG jeraha likitishia kumweka nje Mbappe katika...