Makala

SHINA LA UHAI: Mzigo mkubwa wa gharama ya matibabu ni kizingiti kikuu

August 20th, 2019 3 min read

Na PAULINE ONGAJI

ALIPOGUNDUA kwamba alikuwa na maradhi ya kansa ya Mlango wa Uzazi (Cervical Cancer), dunia ilimpasukia Rose Adero, 41, huku akipoteza matumaini ya kuendelea kuishi.

Ilikuwa ni mwaka wa 2015, mkazi huyu wa mtaa wa Umoja Innercore jijini Nairobi, alipogundua hali yake ya kiafya ambayo kwa takriban miaka minne sasa imemkosesha usingizi na kufyonza hela zote za familia yake.

“Masaibu yangu yalianza mwaka wa 2015 ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi na mwanajinalokojia, nilipatikana kuwa na kansa ya mlango wa uzazi,” aeleza mama huyu wa watoto wanne.

Alianza kufanyiwa matibabu yaliyohusisha upasuaji, taratibu za tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy). Lakini akiwa katika harakati, hizo alipata pigo baada ya mumewe kupatikana na kansa ya ini ambayo ilikuwa katika hatua ya nne (stage four).

“Nililazimika kusitisha matibabu yangu mara moja kwani nilikuwa nimepoteza ajira kama keshia katika mojawapo ya maduka makuu ya jumla nchini, na huku mume wangu akianza kupokea matibabu, hatungeweza kumudu gharama ya matibabu,” aeleza Bi Adero ambaye kwa sasa amesalia mjane baada ya mumewe kuaga dunia mwezi Mei 2018.

Lakini huo haukuwa mwisho wa masaibu yake kwani kutokana na gharama ya matibabu yake na ya mumewe, amelazimika kuuza baadhi ya mali waliyokuwa wamekusanya huku wanawe kati ya miaka mitano na 22 wakilazimika kusitisha masomo kutokana na ukosefu wa karo.

“Uchunguzi wa mwisho ulikuwa mwezi Julai mwaka jana ambapo daktari aliamuru nifanyiwe utaratibu a MRI katika sehemu ya tumbo na fupanyonga, uchunguzi ambao ungegharimu Sh36, 000. Aidha, nilipaswa kufanyiwa uchunguzi wa seli na tishu katika sehemu hii (biopsy) kubaini kiwango cha kansa hiyo mwilini mwangu, lakini sikuwa na pesa,” aeleza.

Kulingana na utafiti, ni asilimia tatu pekee ya wanawake nchini Kenya ambao huenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kansa hii huku hata wanaotafuta tiba mapema wakikumbwa na mzigo mkubwa wa gharama ya matibabu.

Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Kansa unaashiria kwamba gharama ya matibabu inasalia kuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ugonjwa huu ambapo uchunguzi wa kansa ya uzazi nchini Kenya humgarimu mwanamke angaa Sh3, 000.

Aidha, tiba ni ghali sana huku ikigharimu kati ya Sh172, 000 na Sh759, 000 kutibu kansa hii bila upasuaji, na Sh672,000 na Sh 1.2m kutibu maradhi haya endapo upasuaji utafanywa.

Haya yakijiri, takwimu za maradhi haya zaendelea kutisha ambapo kulingana na shirika la kimataifa la utafiti wa kansa, ni ya pili miongoni mwa kansa zilizokithiri sana nchini Kenya, baada ya ile ya matiti.

Kulingana na utafiti wa wizara ya Afya, maradhi haya husababisha vifo vya wanawake wanane kila siku nchini Kenya, idadi ambayo ni sawa na vifo 3,286 kila mwaka. Aidha, kansa hii husababisha vifo vingi; asilimia 12 miongoni mwa watu wanaopatikana kuugua ikilinganishwa na kansa ya matiti ambayo asilimia tisa ya wanaopatikana na maradhi haya hufariki.

Isitoshe, wanawake watatu kati ya 100 nchini Kenya wamo katika hatari ya kuugua maradhi haya, huku visa 5,250 vikiripotiwa kila mwaka nchini.

Jinsi inavyosambaa

Husambaa katika hatua nne.

• Katika hatua ya kwanza, kansa husambaa kwenye mlango wa uzazi hadi kwenye uterasi. Hapa, tiba inahusisha upasuaji unaojulikana kama hysterectomy ambapo sehemu au uterasi yote inaondolewa.

• Hatua ya pili inahusisha seli za kansa kuenea mbali kwenye mlango wa uzazi na hata kufikia sehemu ya uke. Hapa, tiba huhusisha tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy).

• Katika hatua ya tatu, maradhi haya huwa yameenea hadi kwenye ukuta wa fupanyonga na huenda ikachukua asilimia 33 ya sehemu ya uke na hata kusababisha figo kuvimba na kutatiza au hata kusitisha kabisa shughuli za kiungo hiki. Hapa pia, utaratibu wa tiba unahusisha tibakemia na tibaredio.

• Hatua ya nne na ya mwisho ni mbaya zaidi ambapo huenea hadi kwenye kibofu cha mkojo na hata kuathiri vinundu vya limfu na baada ya muda huenea katika sehemu zingine za mwili.

Chanzo

Kwa hivyo nini hasa kinachochea maradhi haya? Kulingana na Dkt John Ong’ech, mtafiti mkuu wa kimatibabu na mwanajinakolojia katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, baadhi ya mambo yanayoongeza uwezekano wa kukumbwa na maradhi haya ni pamoja na kushiriki ngono na watu kadha bila kinga.

“Hii huongeza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya HPV vinavyosababisha kansa hii,” aeleza.

Pia, anasema kwamba wanawake wanaoishi na virusi vya HIV wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maradhi haya baada ya kuambukizwa virusi vya HPV wakilinganishwa na wale wasio na virusi vya HIV.

Ishara

• Kuvuja damu katika sehemu ya uke baada ya tendo la ndoa

• Kuvuja damu katikati ya siku za hedhi au baada ya kukatikiwa

• Maji maji ya damu kutoka sehemu ya uke ambayo huenda yakawa mengi na kuandamana na harufu mbaya

• Uchungu wa fupanyonga au uchungu baada ya tendo la ndoa

Uchunguzi

Kulingana na Dkt Ong’ech, ugonjwa huu waweza kutambuliwa kupitia kipimo cha saratani ya mlango wa uzazi ( pap smear) kinachosaidia madaktari kugundua vidonda au seli zisizo za kawaida na ambazo zaweza kutibiwa kabla ya kusababisha kansa.

“Kila mwanamke anapaswa kufanyiwa uchunguzi huu angaa mara moja baada ya miaka mitatu hadi uhitimu miaka 70. Wanawake wengi huenda hospitalini wakiwa wamechelewa ambapo mara nyingi kansa hii huwa imeenea katika sehemu zingine, na hivyo kufanya iwe vigumu kupokea matibabu na kuokoa maisha ya mgonjwa,” aeleza.

Kulingana naye, hakuna mtu anayepaswa kufa kutokana na kansa kwani ni ugonjwa ambao waweza kukabiliwa iwapo utatambuliwa mapema.