SHINA LA UHAI: Nimonia: Nduli anayewaandama watoto kila uchao

SHINA LA UHAI: Nimonia: Nduli anayewaandama watoto kila uchao

LEONARD ONYANGO na STEPHEN ODUOR

UTAKAPOMALIZA kusoma makala haya, zaidi ya watoto 10 watakuwa wamefariki kote duniani kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu (nimonia).

Maradhi hayo huua mtoto mmoja kila baada ya sekunde 20 kote duniani.

Nchini Kenya, homa ya mapafu ndio ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi ikilinganishwa na corona, Ukimwi, kansa au malaria.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaolazwa hospitalini kutoka na nimonia humu nchini imekuwa ikiongezeka kila mwaka tangu 2015.

Kwa mfano, watoto 2,517,500 walipelekwa katika hospitali za umma kutibiwa nimonia 2019, kulingana na ripoti ya Hali ya Uchumi nchini ya 2020 inayoandaliwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Watoto milioni 2.2 na milioni 1.6 walipelekwa katika hospitali za umma wakiugua nimonia mwaka wa 2018 na 2017 mtawalia. Asilimia 17 ya watoto wanaolazwa katika hospitali za umma nchini Kenya wanaugua nimonia.

Rahma Swaleh, mkazi wa kijiji cha Wema, eneobunge la Garsen, Kaunti ya Tana River, angali mwenye huzuni licha ya kumzika mwanawe, Idris Swaleh, miezi sita iliyopita.

Rahma Swaleh katika mahojiano na Taifa Leo nyumbani kwake, kijiji cha Wema, Kaunti ya Tana River. Picha/ Stephen Oduor

Kila mara anapokumbuka tabasamu la Idris na jinsi alivyochangamkia wageni, Bi Rahma anagubikwa na majonzi ghafla.

Anasema kuwa wakati mwingine anajisahau anaposikia sauti ya mtoto wa jirani akilia na kudhania ni wake.

“Husimama na kumwendea mtoto wangu nje, lakini ninalokutana nalo ni kaburi tu kando ya nyumba. Hurejea ndani ya nyumba, machozi yakinilengalenga na kila mara humuuliza Mungu maswali kwa hasira kwa nini hangenichukua mimi na kumuacha mwanangu,” anaelezea kwa huzuni.

Mahojiano yetu yamechukua muda mrefu kwani kila Bi Rahma anapotaja jina la mwanawe anashindwa kujiuzuia na kuangua kilio.

Alikataa kufanyia mahojiano nje ya nyumba huku akisema kuwa kaburi la mwanawe linamkosesha amani.

“Mwanangu alianza kuugua homa, nikaona ni jambo la kawaida, nikawa nampa maji anakunywa na dawa za kupunguza joto,” anasema.

“Alikuwa akilalamikia kuumwa na kichwa nyakati za jioni. Nilidhani maumivu hayo ya kichwa yalisababishwa na baridi au upepo kwani alipelekwa shuleni kwa pikipiki kila asubuhi,” anaongezea.

Aidha, alidhani kwamba mwendesha pikipiki alimwangusha kwani kila aliporudi alisema kuwa alihisi ni kama kifua chake ‘kinadungwadungwa na kitu’.

“Akaanza kulalamikia uchovu na baridi ambayo ilikuwa ikimtetemesha jioni tu, nikawa namvalisha nguo za joto na kumkanda kwa maji moto,” anasimulia.

Wakati wa mchana, Idris aliyefariki akiwa na umri wa miaka minane, alionekana kuwa mchangamfu, ila usiku alisumbuka sana.

Ghafla, jioni moja joto lilimzidi akiwa usingizini, akaanza kupumua kwa shida.

“Kwa sababu baba yake hakuwepo nyumbani siku hiyo nilipiga mayowe, jamaa na majirani wakaja kuona kilichokuwa kimenisibu,” anasema.

Idris alikimbizwa katika zahanati ya mjini Lenda kwa kutumia pikipiki.

Lakini Bi Rahma anasema kuwa hakuhudumiwa kwani wahudumu wa afya waliwaeleza kuwa alikuwa amezidiwa sana.

“Ilibidi tumkimbize hadi mjini Hola kwa kutumia pikipiki kwani hatukuweza kupata gari la ambulansi – tulielezwa kwamba dereva hakuwepo na baadaye tukaambiwa kuwa halikuwa na mafuta,” anasema.

Lakini walipofika katika hospitali ya Hola hawakupata madaktari, muuguzi waliyempata alimwekea gesi ya oksijeni puani na kumdunga sindano.

Japo hali ya Idris ilionekana kutulia, muuguzi huyo aliwaambia kuwa ilibidi watafute matibabu zaidi ifikapo asubuhi kwani hali ilikuwa tete.

“Aliniuliza mbona tulichelewa kumpeleka mtoto hospitalini; nilikosa jibu, sikujua nimwambie nini, majibu yangu yalikuwa ni machozi tu,” anasema.

Hospitalini hapo, kulikuwa na watoto 12 ambao waliolazwa kwa ugonjwa wa nimonia, kulingana na Bi Rahma.

“Hakukuwa na mitungi ya kutosha ya oksijeni hivyo, mtoto mmoja akifa, oksijeni inahamishiwa mwingine kujaribu kunusuru maisha yake.

“Baada ya kutathmini ile hali, nilianza kuingiwa na wasiwasi huku nikihisi kwamba hapa mwanangu hatoboi. Siku mbili badaye, nilifanya mipango ya kumhamishia Malindi, Kaunti ya Kilifi,” anasema.

Ombi lake lilikubaliwa, na akaruhusiwa kumtoa kwa hiari yake japo madakitari hawakupendelea.

Walipokuwa njiani kuelekea Malindi, mtoto yule alizinduka ghafla na akamkumbatia mamake kwa sekunde kadhaa na akaendelea na usingizi. Hiyo ndiyo ilikuwa dakika ya mwisho kwa Bi Rahma kumuona mwanawe akiwa hai.

Naye Jane Simon, ambaye anaishi umbali wa mita chache kutoka kwa Bi Rahma, anasimulia jinsi hatua za haraka za wahudumu wa afya katika Hospitali Kuu ya Mombasa, zilisaidia kuokoa maisha ya mwanawe, Ashton, ambaye nusra aingie kwenye orodha ndefu ya maelfu ya watoto wanaofariki kila mwaka nchini Kenya kutokana na ugonjwa wa nimonia.

Jane Simon na mwanawe wakiwa nyumbani mjini Hola, Kaunti ya Tana River. Picha/ Stephen Oduor

“Ashton amepona baada ya kutibiwa na madakitari stadi katika Hospitali Kuu ya Mombasa,” anaelezea Bi Jane.

“Nilipofika naye tu, madaktari walichukua damu kupima, wakamuongezea maji mwilini na kumdunga sindano. Niliridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na madaktari,” anasema.

Baada ya muda mfupi, waliweza kumhakikishia kuwa atakuwa salama huku wakionya kuwa wangempoteza endapo angechelewa kumpeleka hospitalini.

“Hata baada ya kupona, Ashton angali anaonekana dhaifu na hajaanza kuchangamka kama hapo awali. Ni mnyonge na huchoka haraka akiwa michezoni au anapofanya shughuli za nyumbani,” anaelezea.

Tana River ni miongoni mwa kaunti zilizo na visa vingi vya maradhi ya nimonia nchini Kenya.

Kila mwezi, Kaunti hiyo hupoteza zaidi ya watoto 10 wa chini ya umri wa miaka mitano kutokana na ugonjwa wa nimonia.

Haya yanatokana na wazazi kupuuza au kukosa ufahamu kuhusiana na dalili za ugonjwa wa nimonia.

Wataalamu wa afya katika Kaunti hiyo hata hivyo, wanasema kuwa ukosefu wa ufahamu kuhusu dalili za nimonia kunasababisha wazazi wengi kupoteza watoto wao kutokana na maradhi hayo.

“Wazazi wanawaleta watoto hospitalini wakiwa hali mahututi, wakati ambapo homa hiyo imekula mapafu ya watoto na kumaliza,” anasema Ester Ndara, mtaalamu wa afya ya watoto Hola, Tana River.

Anasema kuwa maradhi ya corona yamesababisha uhaba wa mitungi ya oksijeni hivyo kuna uwezekano mkubwa kwa watoto wanaougua nimonia kufariki endapo watapelekwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi.

“Homa ya nimonia sio ugonjwa wa kuchelewesha, mzazi yeyote anapoona dalili za homa ni vyema kumkimbiza mtoto hospitalini afanyiwe uchunguzi,” anasema.

Anasema kuwa baadhi ya wazazi wanakimbilia kuwanunulia watoto wao dawa ya malaria wanapokuwa na joto mwilini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba dalili za malaria na nimonia zinafanana.

Ugonjwa wa nimonia, haswa miongoni mwa watoto husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Streptococcus na Haemophilus.

Bakteria hao husababisha muwasho kwenye mapafu na kumfanya mwathiriwa kuanza kukohoa kikohozi kikavu, kupatwa na joto, maumivu ya kichwa na kujihisi mchovu.

Bakteria zinazosababisha nimonia pia zinaweza kupatikana kwa kupumua hewa iliyo na matone ya mate mwathiriwa anapokohoa au kuchemua.

Bakteria hao wanaweza kuingia katika mwili wa mtoto kupitia damu mara tu baada ya mtoto kuzaliwa.

Dkt Angela Makini wa Hospitali ya Penda jijini Nairobi, anasema kuwa watoto wanaotumia pikipiki kwenda shuleni asubuhi bila kuvalishwa nguo za kuwapa joto wapo hatarini zaidi kupatwa na maradhi ya nimonia.

Dkt Makini pia anasema kuwa mtoto anaposafiri kwenda shuleni kwa kutumia bodaboda kwa zaidi ya dakika 30 bila kuvalia kofia ya helimeti au nguo za kumpa joto aweza kuugua nimonia kwa urahisi.

Utafiti uliofanywa nchini Kenya na shirika la Save the Children pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (Unicef) mnamo 2018, ulibaini kuwa watoto 9,000 wa chini ya miaka mitano walifariki kutokana na nimonia mwaka huo.

Hiyo inamaanisha kwamba watoto 24 hufariki kila siku kutokana na nimonia humu nchini kila siku.

Ripoti hiyo ilibaini kuwa idadi kubwa ya watoto wanaoathiriwa na nimonia ni maskini ambao hupata lishe duni na huduma mbovu za matibabu.

Kulingana na ripoti hiyo, watoto sita kati ya 1,000 walifariki kutokana na nimonia 2018.

You can share this post!

ODONGO: Wanaopinga Ruto wauze sera kujifaa kisiasa nchini

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nitaongezaje mafuta mwilini?