Makala

SHINA LA UHAI: Tatizo la mwasho wa ngozi na matibabu

February 18th, 2020 4 min read

Na BENSON MATHEKA

KUJIKUNA ngozi sio jambo la kawaida jinsi baadhi ya watu wanavyodhani.

Ukikumbwa na hali hii, nenda ukamuone daktari kwa sababu inaweza kuwa dalili ya tatizo kubwa la kiafya.

Wataalamu wanaonya kuwa kuwasha kwa ngozi ya mwili kunakopelekea mtu kujikuna hakufai kupuuzwa.

“Miongoni mwa matatizo ya kiafya ambayo yanasumbua watu wengi duniani na kuwanyima raha ya maisha, ni ngozi kuwasha. Kwa baadhi ya watu, hili linaweza kuwa tatizo sugu. Ingawa ni la kiafya, baadhi ya watu hulihusisha na imani potofu kwa kukosa habari sahihi,” asema mtaalamu wa maradhi ya ngozi, Dkt Epha Swaka.

Anasema kwamba kuna sababu nyingi zinazochochea tatizo hili na baadhi zina madhara makubwa na hata kuhatarisha maisha.

Udhaifu wa kinga

Miongoni mwa sababu za kutokea kwa mwasho wa ngozi baada ya kuoga ni za kimazingira na baadhi zinahusiana na hitilafu katika mfumo wa kinga ya mwili wa mhusika. Huwa ni moja ya dalili za mwanzo za Ukimwi.

“Tatizo hili linaweza kuwa ni dalili za magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama vile matatizo ya figo, ini, tezi shingo, matatizo ya mfumo wa damu, kisukari, saratani na msongo wa mawazo,” aeleza Dkt Swaka.

Mazingira machafu

Tafiti zimebainisha kuwa sababu nyingine ni uchafuzi wa mazingira, kemikali zenye sumu zinazopatikana katika moshi wa tumbaku, mifuko ya plastiki, dawa za kufanyia usafi majumbani, dawa za kuua wadudu au vumbi ndani ya nyumba inayobeba vimelea vya maradhi.

Mzio (Allergy)

Hii hufanya mwili kuathirika na kutokea kwa mwasho pindi mwili unapopata msisimko, hali ambayo hujulikana kama mzio.

“Mzio huanza pale mfumo wa kinga ya mwili unapobainisha mwili umevamiwa na kemikali na kuamuru seli husika kujibu kwa kuzalisha kemikali maalumu ambazo husababisha ngozi kuwaka kwa lengo la kuvunja nguvu za kemikali vamizi,” asema Dkt Swaka.

Watu wengi wana mzio wa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na dawa za tiba, kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni, vipodozi, aina fulani za vyakula, kemikali zinazowekwa katika maji kama vile ‘chlorine’, maji ya kuoga yenye chumvi nyingi na kemikali zinazotumika katika utengenezaji wa nguo, ikiwa ni pamoja na taulo ya kuogea.

Vyakula

Vyakula kama vile mayai, maziwa, samaki, nyama, karanga, vyakula vitokanavyo na unga wa ngano, kahawa, pombe na baadhi ya vyakula na vinywaji vinavyotengenezwa viwandani kwa kutumia kemikali vinaweza kusababisha ngozi kuwasha. Hali hii pia inaweza kutokea kutokana na kula vyakula vyenye mchanganyiko wa vikolezo kama pilau na viungo vingi.

Wataalamu wanasema watu wengi hawatumii kiasi cha kutosha cha matunda, mboga na mafuta yanayotokana na mimea au samaki, jambo ambalo huathiri vibaya afya ya ngozi.

Sumu mwilini

Tatizo jingine linalochangia mwili kuwasha wakati wa kuoga ni kutotumia kiasi cha kutosha cha maji ya kunywa kila siku. Hali hiyo inafanya mwili kuwa na upungufu wa maji na kuathiri vibaya afya ya ngozi na uwezo wake wa kuondoa sumu mwilini.

Ngozi isiyokuwa na afya njema inashindwa kutunza kiasi cha kutosha cha unyevu na kusababisha ukavu. Ngozi inapokuwa kavu, husisimka kupita kiasi wakati wa kuoga na kusababisha mwasho.

Maradhi ya zinaa/fangasi

Kuwashwa sehemu za siri kunaweza kuwa dalili ya maradhi ya zinaa. Bila kujali jinsia, mwasho unaweza kusababishwa na ugonjwa wa ngozi, magonjwa ya zinaa au mzio.

Sababu kuu za kuwashwa makalioni ni kutojisafisha vizuri, kula vyakula vyenye viungo vingi sana, kuhara, vidonda kwenye njia ya haja kubwa, maambukizi ya fangasi, minyoo na kadhalika.

Mara nyingi mwasho sehemu za siri huhitaji matibabu ya hali ya juu zaidi, ikiwa unawashwa kwa muda mrefu ni vyema kuzungumza na daktari.

Kuwashwa uume au sehemu zingine za siri za mwanaume husababishwa na sababu zilezile zinazosababisha mwasho sehemu zingine za mwili. Maambukizi hasa ya magonjwa ya zinaa ndio chanzo kikuu cha kuwashwa uume. Sababu nyingine ni maradhi ya fangasi, ugonjwa wa upele, kuwepo kwa chawa, mzio na maambukizi ya bakteria.

Kwa wanawake, mwasho unaweza kusababishwa na fangasi waitwao Candida. Dalili kuu ni kuwashwa ukeni, kuvimba na kutoa uchafu mweupe kama maziwa ukeni.

Saratani

Saratani ya ngozi na damu inaweza kusababisha ngozi kuwasha na kufanya mtu kujikuna.

Wasiwasi (Generalized Anxiety Disorder)

Ni ugonjwa ambao unatokana na hofu ya matukio fulani. Wakati mwingine husababisha kujikuna sehemu mbalimbali hata sehemu za siri.

Ugonjwa wa Sjogren (Sjogren’s Syndrome)

Ni ugonjwa katika mfumo wa kinga ya mwili unaoathiri tezi zinazosaidia mwili kutengeneza unyevunyevu kwenye macho na mdomo. Ugonjwa huu huathiri wanawake zaidi kuliko wanaume.

Kisukari

Ni ugonjwa unaosababishwa na kasoro katika utengenezaji wa Insulin au utendaji kazi wake. Kisukari kilichokomaa kinaweza kusababisha maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kizunguzungu na kuwashwa sehemu za siri.

Sababu zaidi

• Matatizo ya ngozi kama kukauka (xerosis), kuchomeka, makovu na kuumwa na wadudu

• Maradhi ikiwemo saratani ya damu, matatizo ya figo, kukosa madini.

• Matatizo ya neva

• Maradhi ya akili

• Mimba

Ufanyeje?

1. Wanaume kuosha vizuri uume, na wale ambao hawajatahiriwa wanapaswa kuosha kwa umakini zaidi hadi sehemu za ndani za ngozi.

2. Ziweke sehemu zako za siri kuanzia ndani ya makalio katika hali ya usafi na ukavu, kwa maana unyevunyevu unaweza sababisha maambukizi. Matumizi ya poda ya ‘Cornstarch’ yanaruhusiwa hasa kipindi cha joto kali.

3. Vaa nguo isiyobana sana, iliyotengenezwa kwa vitu asilia kama pamba. Badili nguo ya ndani (chupi) angalau kila siku.

4. Vaa kondomu kila unaposhiriki ngono na mwanamke usiyejua hali yake kiafya kiujumla.

5. Wanawake wanapaswa kuosha sehemu za siri kuanzia mbele kwenda nyuma ili kuzuia bakteria kutoka njia ya haja kubwa kuingia ukeni.

Hali ikizidi

Kulingana na tovuti ya www.mayoclinic.com, mtu anapaswa kumuona daktari;

• Ngozi ikiwashwa kwa zaidi ya wiki mbili bila kutulia.

• Hali inakuwa mbaya na kukuzuia kutekeleza majukumu yako ya kila siku na kukukosesha usingizi

• Mwili unaanza kuwasha ghafla na haufahamu chanzo chake

• Kuwashwa kunaandamana na dalili nyingine kama vile uchovu mwingi, kupunguza uzani wa mwili, kukojoa sana, kuhisi joto jingi au rangi ya ngozi kuwa nyekundu.

Kupunguza mwasho

• Kunywa maji kwa wingi

• Kuoga kwa haraka na kutotumia maji moto

• Kutotumia sabuni zilizo na marashi kali

• Kujipaka losheni zisizo na kemikali kali baada ya kuoga

• Kuepuka kutumia sabuni zilizo na marashi kufua nguo.

• Wataalamu wanasema watu walio na umri mkubwa hasa kuanzia miaka 65 huwashwa na ngozi kwa sababu huwa inabadilika kuwa nyepesi na isiyodumisha kiwango cha maji kinachohitajika mwilini.

• Mtu anaweza kuwashwa na ngozi wakati anapotumia au baada ya kutumia dawa fulani kama ‘aspirin’, za kutibu msukumo wa damu au saratani.