Makala

SHINA LA UHAI: Uavyaji ulivyosalia 'mada ngumu' licha ya wengi kufariki

March 10th, 2020 5 min read

Na MARY WANGARI

TANGU jadi, suala la ngono na uzazi kuhusu jinsia ya kike huibua mjadala na kuvutia hisia kali kila wakati.

Japo maendeleo katika teknolojia ya habari na mawasiliano ikiwemo utandawazi yamesababisha mabadiliko makubwa katika nyanja ya kisiasa na kiuchumi, ni bayana kwamba kuna baadhi ya masuala nyeti ambayo jamii haiko tayari kabisa kujadili.

Iwe ni mapuuza tu au woga wa kukabili uhalisia uliopo, ni wakati tu utakaoweza kuamua.

Mwakilishi Mwanamke katika Kaunti ya Nairobi Esther Passaris anafahamu vyema ukweli huu baada ya kuweka wazi maoni yake hivi majuzi kuhusu uavyaji mimba miongoni mwa wanawake nchini.

Bila shaka mwanasiasa huyo hakujua kilichomsubiri aliposema kwamba uamuzi wa kuavya au kubakia na mimba unapaswa kuachiwa mwanamke.

Kusema kwamba Bi Passaris alijipalilia makaa hakutoshi kuelezea hisia kali zilizoibuka kufuatia kauli yake huku baadhi ya Wakenya wakiungana kumponda na kumzomea pasipo huruma.

Kwamba uavyaji mimba ni suala nyeti nchini Kenya si siri na aghalabu huzungumziwa kwa minong’ono huku kitendo hicho kikilaaniwa vikali na makundi ya kidini na kuonekana kama mwiko miongoni mwa wanajamii.

Licha ya kwamba uavyajiu mimba ni marufuku kulingana na sheria nchini Kenya, utafiti unaonyesha kwamba thuluthi moja ya wanawake wanaoavya hawajali kuhusu hilo.

Isitoshe, takwimu zinaonyesha vinginevyo huku ikibainika kwamba sheria, dini, itikadi za kitamaduni pamoja na unyanyapaa hazijafanikiwa kuwazuia wanawake kujihusha na ngono na hata kuavya mimba zisizotakikana.

Kulingana na ripoti mpya iliyotolewa majuzi na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Kituo cha Idadi ya Watu na Utafiti wa Afya Afrika, (APHRC) iliibuka kwamba zaidi ya wanawake nusu milioni huavya mimba nchini kila mwaka.

Hii inamaanisha kwamba zaidi ya wanawake 500,000 huavya mimba kila mwaka idadi ambayo ni sawa na wanawake zaidi ya 40,000 wanaoavya mimba zisizotakikana kila mwezi hapa nchini.

Isitoshe, utafiti huo unaashiria kwamba asilimia 40 ya wanawake katika mataifa yanayoendelea hupata mimba zisizotakikana ambapo asilimia 55 huishia kuavya mimba hizo.

Hata hivyo, kutokana na mfumo wa sheria nchini usioruhusu haki ya uavyaji mimba kwa hiari, unyanyapaa pamoja na mtazamo wa kijamii, utafiti unaonyesha kwamba idadi kubwa ya wanawake wanaoavya mimba aghalabu huishia mikononi mwa madaktari feki.

Wengi wa wanawake hawa hufariki au hata kugeuka walemavu kutokana na matatizo yanayowapata kufuatia uavyaji mimba usio salama.

Kando na madaktari hao bandia kukosa ujuzi wa kutoa huduma ya matibabu baada ya uavyaji mimba, vituo hivyo pia huwa havina vifaa muhimu, kulingana na mtaalam wa utafiti kuhusu masuala ya afya ya uzazi ikiwemo uavyaji mimba na madhara yake nchini Kenya na mataifa mengineyo barani Afrika, Kenneth Juma.

“Ni vigumu kupata huduma ya matibabu ya baada ya uavyaji mimba maadamu idadi kubwa ya vituo vya afya nchini Kenya hata hospitali za rufaa hazina vifaa mwafaka vya kutibu matatizo ya wanawake hawa,” anaeleza.

Si ajabu kwamba kwa baadhi ya wanawake hasa wasiojiweza kifedha, uamuzi wa kuavya mimba huwa ni suala la kufa au kupona.

Kisa cha mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Caroline Mwatha kilichogonga vichwa vya habari nchini na kimataifa ni kielelezo tosha kuhusu jinamizi la uavyaji mimba wa kisiri nchini.

Mnamo February 2019, ripoti kuhusu kifo cha mkereketwa huyo kutoka Dandora, Nairobi, zilitikisa wengi hasa baada ya upasuaji kufichua kwamba alifariki akiavya mimba ya miezi mitano.

Ripoti ya upasuaji iliyotolewa na mwanapatholojia Peter Ndegwa ilionyesha tumbo la uzazi la marehemu liliharibiwa vibaya hali iliyomfanya kuvuja damu kupita kiasi alipokuwa akijaribu kuavya kijusi hicho.

Bi Mwatha ni mfano tu wa maelfu ya wanawake nchini ambao wameaga dunia katika harakati za kuavya mimba wasizozitaka hasa kutokana na matatizo ya kiafya yanayojitokeza baadaye.

Japo Kenya imepiga hatua katika kuboresha sekta ya afya katika siku za hivi karibuni, ni bayana kwamba bado ina safari ndefu katika kukomesha vifo vya kina mama na watoto wachanga wakati wa kujifungua, ikiwemo matatizo ya kiafya kutokana na mchakato wa uzazi, suala ambalo limesalia kuwa kero kuu.

Takwimu zinaashiria uhalisia wa kutisha kwamba asilimia 90 ya wanawake katika mataifa yanayoendelea ikiwemo Kenya hufariki kutokana na uavyaji mimba usio salama.

Hii ni idadi ya kuhofisha mno ikilinganishwa na wanawake 47,000 wanaofariki kote duniani kutokana na uavyaji mimba kulingana na utafiti wa “Visa na Matatizo ya Uavyaji Mimba usio Salama Kenya”.

Isitoshe, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa mwaka jana ilionyesha kuwa wanawake na wasichana chipukizi aghalabu huamua kujihusisha na uavyaji mimba usio salama baada ya kushindwa kupata huduma salama.

Ripoti hiyo vilevile inafichua kuwa kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa mwanamke yeyote aliye na ujauzito usiotakikana kushiriki uavyaji mimba usio salama.

Wanawake wasio na uwezo wa kifedha pia wana uwezekano zaidi wa kushiriki uavyaji mimba usio salama hivyo kukabiliwa na hatari zaidi ya kufariki, kujeruhiwa au kupata matatizo ya kiafya ikilinganishwa na wanaoshiriki uavyaji mimba salama, WHO inaeleza.

Aidha, kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa wanawake wanaoavya mimba kwa mara ya kwanza kufanya hivyo tena kulingana na utafiti uliofanywa na Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH).

Ripoti hiyo ya kuhofisha ilifichua kwamba uavyaji mimba unahusisha wanawake wote waliofikisha umri wa uzazi pasipo kujali dini, hadhi katika jamii na kiwango cha elimu na kuhusisha wasichana kuanzia umri wa miaka 10.

Isitoshe, ripoti hiyo inaashiria kwamba miongoni mwa wanaotafuta matibabu ya baada ya uavyaji mimba katika vituo vya afya, asilimia 16.5 ni wasichana walio na umri wa kati ya miaka 10 na 19; asilimia 31.7 ni walio na umri kati ya miaka 20 na 24 huku nusu nyingine wakiwa walio na umri zaidi ya miaka 25.

Isitoshe, ripoti iliyotolewa na mtandao wa Google ilithibitisha kwamba swali la mtandaoni la “jinsi ya kuavya mimba” lilikuwa ndilo swali maarufu lililosakwa miongoni mwa Wakenya.

Ripoti hiyo ya Google Zeitgeist ilionyesha kwamba swali nambari moja la “jinsi ya” lililokuwa likivuma lilikuwa la Wakenya wakitatafuta habari kuhusu jinsi ya kuavya mimba.

Baadhi ya mambo yanayochangia uavyaji mimba usio salama

* Ukosefu wa huduma salama za uavyaji mimba

* Ukosefu au uhaba wa huduma za upangaji uzazi

* Sheria kali zinazozuia kutolewa kwa huduma za uavyaji salama wa mimba.

* Bei ghali ya huduma hizo

* Uhaba au kudibitiwa kwa huduma hizo

* Unyanyapaa hasa kutokana na itikadi za kidini na kitamaduni ambapo wanaoshiriki kudunishwa katika jamii

* Pingamizi kila mara kutoka kwa watoaji huduma ya afya

* Masharti mengi ikiwemo kipindi cha lazima cha kungoja, ushauri nasaha wa lazima, habari za kupotosha, uidhinishaji wa mtu wa tatu pamoja na vipimo vingi vya kiafya vinavyochelewesha utowaji huduma.

Kinyume na dhana ya wengi kwamba uavyaji mimba huwaathiri wanawake pekee, utafiti uliofanywa na APHRC unafichua kwamba wanaume vilevile huathirika kiafya kutokana na shughuli hiyo.

Utafiti huo kuhusu Dhana ya Jamii kuhusu Uavyaji Mimba, Wanawake wanaoavya na Wanaotoa huduma hizo nchini, ulionyesha kwamba idadi kubwa ya wanawake na wasichana wachanga hupendelea maduka ya kuuzia dawa maadamu yana usiri zaidi ikilinganishwa na hospitali na kliniki hivyo kuwalinda wahusika dhidi ya unyanyapaa.

Matatizo ya kiafya yanayowapata wanawake kutokana na uavyaji mimba usio salama

* Uavyaji mimba ambao haujakamilika – Hali hii hujitokeza wakati kiwiliwili cha kijusi kinapokosa kutolewa chote au kijisehemu kuachwa kwenye tumbo la uzazi

* Kuvuja damu kupita kiasi – hii ni mojawapo wa sababu kuu ya vifo.

* Maambukizi ya maradhi ikiwemo HIV kutokana na kushiriki vifaa

* Kujeruhiwa na kuharibiwa kwa nyungu ya uzazi – Hii hutokana na kudungwadungwa kwa kwa kutumia vifaa vyenye makali

* Kuharibiwa kwa njia ya uzazi, kwa kuingiza vifaa hatari kama vile sindano za kushonea, vijiti au vigae kwenye sehemu nyeti.

Matatizo ya uavyaji mimba yanayowaathiri wanaume

Data iliyokusanywa na APHRC ilithibitisha kwamba wanaume pia huathirika kiafya kutokana na uavyaji mimba wa wake au wapenzi wao.

Baadhi ya matatizo hayo ni:

* Kupoteza uzani pamoja na kukonda kupindukia – hali hii huchangiwa hasa na msongo wa mawazo, majuto, kujilaumu pamoja na kujisuta nafsi

* Matatizo ya kisaikolojia

* Vifo kutokana na matatizo ya kiafya kama vile shinikizo la damu na kadhalika.

Dalili ya matatizo kutokana na uavyaji mimba usio salama

* Kuvuja damu kupindukia

* Uchungu mkali kwenye tumbo

* Maambukizi

* Kufa ganzi kufuatia baada ya mfumo wa kusambaza damu mwilini kuvurugika

Jinsi ya kutibu matatizo yanayotokana na uavyaji mimba usio salama

* Uvujaji damu kupita kiasi – Huhitaji matibabu ya dharura ikiwemo kuongezwa damu maadamu kuchelewesha kwa njia yoyote husababisha madhara hatari hata kifo.

* Maambukizi ya maradhi – Ni muhimu kwa mwathiriwa kupata matibabu haraka iwezekanavyo pamoja na kufanyiwa vipimo muhimu ili kumzuia dhidi ya madhara zaidi

* Uavyaji mimba ambao haujakamilika – Hakikisha kwamba viungo au viwiliwili vyovyote vilivyosalia kwenye tumbo la uzazi vimeondolewa kabisa kwa kusafishwa na mtaalam

* Kujeruhiwa kwa sehemu nyeti na viungo vya ndani mwilini – Ikiwa mwathiriwa anashukiwa kuwa na hali hiyo, ni muhimu kwenda katika kituo cha afya na kupata matibabu haraka iwezekanavyo.

 

[email protected]