Makala

SHINA LA UHAI: Ufahamu ugonjwa wa Tetekuwanga na matibabu yake

October 29th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

MOJA kati ya maradhi yanayowasumbua watoto wachanga na watu wazima katika maisha yao, ni Tetekuwanga, tetewanga au ukipenda tetemaji (Chicken pox) na wataalamu wanasema yanaweza kusababisha upofu yasiposhughulikiwa kwa wakati.

Huu ni ugonjwa ambao matabibu wanasema kila mtu hutazamiwa kuugua mara moja katika maisha yake.

“Inaaminika kwamba ni sharti kila mtu augue tetekuwanga katika maisha yake. Asipougua akiwa mtoto, basi utampata akiwa mtu mzima,” asema Dkt Bonface Wanjau wa hospitali ya watoto ya Provide International, jijini Nairobi.

Hata hivyo, anasema kilicho muhimu ni kuhakikisha kuwa watoto wamekingwa na maradhi haya sawa na mengine.

Mtaalamu huyu asema kuwa maradhi haya husababisha vipele katika mwili wa mtoto, ngozi yake huwasha, kisha vidonda vilivyo na umajimaji hujitokeza mwilini.

Dkt Wanjau asema kwa sasa wazazi hawafai kuwa na wasiwasi watoto wao wanapougua kwa sababu kuna chanjo ya kuudhibiti.

Anasema ugonjwa huu huenea kwa haraka. “Unaweza kuambukizwa kwa kushika kidonda au ngozi ya mtu anayeugua. Aidha mtu anayeugua akipiga chafya au kukohoa anaweza kukuambukiza virusi vyake,” asema.

Maradhi haya hujitokeza katika muda wa siku 21 baada ya kuambukizwa. Visa vingi huripotiwa miongoni kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 10.

Hata hivyo, kulingana na Dkt Wanjau, watoto ambao wazazi wao walipata chanjo ya kuzuia ugonjwa huu, hawawezi kuupata kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.

Hii ni kwa sababu chembechembe za damu ya mama yao huwasaidia kuimarisha kinga dhidi yake na maradhi mengine.

Aidha Dkt Wanjau asema maradhi haya yanaweza kuwalemea watoto ambao wana kinga hafifu ya mwili.

Japo wataalamu wa afya ya watoto wanasema mtu huugua maradhi haya mara moja tu maishani, athari zake kwa watoto si mbaya mno ikilinganishwa na kwa mtu mzima.

“Ili kuzuia ugonjwa huu, mpeleke mtoto wako kwa daktari achanjwe,” asema Teresa Kairu muuguzi aliyewahudumia watoto na akina mama kwa miaka mingi katika kituo cha afya cha Mama Ippolita, mtaani Embakasi, Nairobi.

Wataalamu wanasema mtoto hupata kati ya vidonda vidogo 250 – 500 vyekundu vinavyowasha na vilivyojaa umajimaji.

Bi Kairu asema vidonda hivyo haviachi kovu mwilini vinapopona hasa endapo havijapata bakteria hatari.

Kumbuka vipele hivi havijitokezi kwa wakati mmoja, hivyo wakati vingine vinapona, kuna vingine vitakuwa vinatokeza.

Mgonjwa huendelea kuhisi vibaya mpaka vipele vikauke, na hatua hii huweza kuchukua hadi wiki mbili kabla ya vipele kutoweka kabisa.

Wataalamu wanasema watoto wakichanjwa mapema, hupona haraka kuliko wale ambao hawajachanjwa.

Tetekuwanga husababishwa na nini?

Tetekuwanga husababishwa na virusi ambavyo kwa kitaalamu hujulikana kama Varicella Zoster (VZV). Mara nyingi huambukizwa kutokana na kugusana na mtu mwenye ugonjwa huu.

Virusi vyake huendelea kuwa na uwezo wa kuambukiza mpaka vipele vitumbuke na kukauka. Hivyo epuka kugusana na mgonjwa mpaka vipele vitakapokauka kabisa.

Virusi hivi huweza kuambukizwa kwa njia zifuatazo;

• Mate

• Kukohoa

• Kupiga chafya

• Kugusa majimaji ya malengelenge ya tetekuwanga

Walio kwenye hatari ya kupata Tetekuwanga

Kwa watu waliowahi kuugua au kutumia kinga za tetekuwanga, ni vigumu sana kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Pia, mtoto mchanga huweza kulindwa dhidi ya maambukizi kutokana na kinga kutoka kwa mama yake ambayo huzaliwa nayo.

Lakini wataalamu wanaonya kuwa kinga hii huendelea kudumu kwa miezi mitatu tu.

Mtu yeyote ambaye hajawahi kupata tetekuwanga, yupo kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu. Hata hivyo wataalamu wanasema makundi yafuatayo yapo kwenye hatari kubwa zaidi;

  1. Wanaoishi na wagonjwa wa tetekuwanga
  2. Walio chini ya umri wa miaka 12
  3. Wanaoishi na watoto wanaogua
  4. Wanaohudumia watoto kwenye vituo vya kulea watoto au shule za watoto
  5. Walio na kingamwili hafifu

Matabibu wanashauri watu kwenda hospitali mara moja baada ya kuona vipele visivyoeleweka, hasa kama vinaambatana na baridi yabisi au homa.

Daktari huvichunguza ili kuhakikisha kama kweli ni vya ugonjwa wa tetekuwanga.

Wataalamu wanasema ugonjwa huu ukimpata mama mjamzito anaweza kujifungua mtoto mwenye tatizo la kukua vizuri, mwenye kichwa kidogo au matatizo ya macho.

Ikiwa mtoto wako ana Tetekuwanga;

• Jaribu kumzuia kukuna vidonda: Huenda akaathiriwa zaidi au kuwa na uchungu. Ikibidi kata kucha za mtoto wako.

• Usifunike vidonda: Wataalamu wanaonya wazazi dhidi ya kufunika vidonda kwa sababu vinaweza kubadilika na kuwa mbaya zaidi.

• Mtenge na wengine: Weka mtoto wako mbali na watu ambao hawajapata chanjo ya ugonjwa huu.

• Maumivu: Mpe dawa ya kupunguza maumivu.

• Kuvitunza vidonda: Mpake dawa kwa kutumia kitambaa kilicho na maji au muoshe mara moja kwa siku ili kuweka vidonda vikiwa safi.

Wataalamu wanaonya dhidi ya kumpatia mtoto dawa iliyo na aspirin au brufen ikiwa anaugua tetekuwanga.

Wanasema viungo hivi viwili vinaweza kumdhuru mgonjwa.

Wazazi pia wanashauriwa kumzuia kucheza na watoto wengine ili asiwaambukize. Vilevile wanasema hatua hii itasaidia vidonda vyake kupona haraka.

Hivyo mpumzishe mtoto kwenda shule hadi apone kabisa.