SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa tezi umeanza kuweka wadau wasiwasi

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa tezi umeanza kuweka wadau wasiwasi

NA WANGU KANURI

BAADA ya Sarah Katule kujifungua kifungua mimba wake, 2011, alianza kuhisi uchovu mwingi, midundo ya moyo wake ikawa inasikika kwa nguvu, akawa anapunguza kilo licha ya kula vizuri, akawa mwenye hisia nyingi za kighafla huku maziwa yakikosa kumtoka alipokuwa akimnyonyesha mtoto wake.

Isitoshe, Bi Katule alikuwa anahisi nguvu zikimwishia kila mara na licha ya kuenda hospitalini kupata matibabu, madaktari hawakuwa wanaweza kumweleza kiini cha dalili alizokuwa nazo zaidi ya kumpatia dawa kila mara.

Siku moja alipokuwa akimpeleka mtoto wake kupata chanjo hospitalini, alianguka akipanda matatu.

“Nilidhani nimekanyaga vile vidato vya gari lakini sikuwa,” anaeleza.

Bi Katule alirudi nyumbani, akamwacha mtoto wake na kuenda hospitalini huku akiwa mwenye hasira nyingi kwani alijihisi hakuwa sawa licha ya kugharamia matibabu mara nyingi bila ya madaktari kugundua ugonjwa aliokuwa akiugua.

Wakati huo shingo yake ilikuwa imeanza kutokezea mbele na kufura. Muuguzi alipoingia chumbani kumpima, Bi Katule alipinduka na daktari akaweza kuona shingo yake na kuelewa kiini cha dalili alizokuwa nazo.

Baada ya kufanyiwa vipimo, Bi Katule alielezwa kuwa aliugua ugonjwa wa tezi (thyroid disease) unaofanya tezi kufura baada ya kupata mtoto (postpartum thyroiditis).

Ugonjwa huo husababishwa na tezi kutengeneza homoni kwa wingi (hyperthyroidism). Hali kadhalika tezi inaweza kukosa kutengeneza homoni za kutosha (hypothyroidism).

Dkt Roselyn Ngugi, Mtaalamu wa homoni katika Hospitali ya AAR, Nairobi anaeleza kuwa homoni ya tezi husaidia kudhibiti kasi ya kutumika kwa nguvu inayotoka kwa chakula anachokula mtu kila siku, kuwasaidia wanawake wakati wa hedhi, kukua kwa akili ya mtoto na mwili wa mtu mzima.

Isitoshe, ugonjwa huu huenezwa kijeni huku zaidi ya asilimia 60 ya visa vya ugonjwa huo ukiwa miongoni mwa wanafamilia.

“Kitambo, ugonjwa huu ulikuwa umekithiri miongoni mwa Wahindi lakini ndoa za mseto na mazingira wanayoishi watu yamechangia katika uenezi,” anasema.

Dalili za hypothyroidism ni pamoja na kuhisi uchovu, baridi jingi, kukaukiwa uendapo chooni, kuwa na ngozi ngumu, kutokumbuka matukio, kuongeza uzani, uhafifu wa mishipa ya mwili na kuhisi usingizi sana.

Aina hii ya ugonjwa wa tezi husababishwa na maambukizi ya virusi ambayo hufanya seli za mwili kushindwa kutofautisha seli halisi na geni, hivyo kushambulia zile halisi (autoimmune infections). Vilevile, ugonjwa huu huathiri sana watu wazee haswa walio na zaidi ya miaka 65 na wanawake.

Kwa upande mwingine, hyperthyroidism, huathiri sana watu wadogo na hata watoto huku dalili zake zikiwa kushindwa kupata usingizi, kuhisi uchovu, kuharisha, misuli kuwa hafifu, kukojoa zaidi, kuhisi kiu kingi na kuhisi kujikuna.

Hata hivyo, hyperthyroidism huua ikilinganishwa na hypothyroidism licha ya magonjwa haya ya tezi yakitokea mara kwa mara.
Huku ugonjwa huu ukiathiri watu wote bila kubagua umri au jinsia, matibabu yake ni ghali sana.

Bi Katule anakumbuka alivyosumbuka akitafuta matibabu huku akizungushwa kwa madaktari wa masuala ya koo, pua na macho.

“Kwa zaidi ya miaka sita, nilikuwa nikipewa dawa zingine mbadala (generic) zilizofanya homoni za tezi kutolingana ili niweze kufanyiwa upasuaji na tezi yangu kuondolewa,” anaeleza.

Mwishoni mwa 2017, Bi Katule aliweza kufanyiwa upasuaji huku akieleza alichukua hatua hiyo baada ya kuchoka kumeza tembe za ugonjwa huo.

Zaidi ya hayo, wagonjwa wa hyperthyroidism hawapaswi kumeza dawa kwa zaidi ya miaka miwili kwani kingamwili yao huanzia kuzorota na Bi Katule alikuwa amemeza dawa kwa miaka sita hivi.

Sarah Katule, mwathiriwa wa ugonjwa wa tezi (thyroid) ambaye mashaka aliyopita yalimlazimu kuanzisha wakfu wa kusaidia waathiriwa wa maradhi hayo kupata msaada. PICHA | FRANCIS NDERITU

Ili kuweza kuwasaidia wagonjwa wengine wa tezi, Bi Katule aliweza kuanzisha Wakfu wa Wagonjwa wa Tezi (TDAK) ambao unawaleta pamoja waathiriwa.

“Sikuwa na mtu ambaye alinipa mwongozo au kunishauri na kupitia masaibu niliyopitia nikitafuta matibabu na pia kuelewa ugonjwa huu, nilitaka watu wengine wasihangaike,” anasema.

Dkt Ngugi anaeleza kuwa vipimo vya skrini vya ugonjwa wa tezi huwa ghali sana huku mgonjwa akilazimika kulipia Sh3,000-Sh4,000 kila mara apatapo matibabu.

Tembe za ugonjwa huo hugharimu Sh20-Sh50, huku dawa nyingine zikiwa za mwigo (generic) ambazo humrudisha nyuma mgonjwa aliyekuwa akipona.

Vile vile, wagonjwa wa tezi hulazimika kumeza tembe zaidi ya 10 kila siku kwa mwezi au zaidi kulingana na ukali wa ugonjwa huo mwilini mwao.

Huku mwezi jana – Septemba – ukiadhimisha magonjwa haya ya tezi, Dkt Ngugi anaeleza kuwa ugumu wa ugonjwa huu kugundulika na kutibiwa mapema umechangiwa na ukosefu wa madaktari nchini Kenya wanaouelewa ugonjwa huo.

“Isitoshe, hospitali nyingi za rufaa zinapaswa kuchunguza na kupima uwepo wa ugonjwa huu kwa wagonjwa wote wanaofika hospitalini kama wafanyavyo shinikizo la damu,” anapendekeza.

Huku ndoa zikivunjika kutokana na ugonjwa huu, Dkt Ngugi anasema wagonjwa wa tezi huwa wapweke kwani watu wengi hawaelewi dalili za mgonjwa haswa hisia anazoonyesha.

“Wakati mwingine, ugonjwa wa tezi hufanya wagonjwa kukodoa macho huku watu wakiwatoroka,” anasema.

Kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) ugonjwa wa tezi unaweza ukasababisha kansa ya tezi huku kila mwaka wanaume 12,000 na wanawake 33,000 wakipata kansa hiyo ya tezi.

“Wanaume 950 na wanawake 1,100 hufariki kutokana na ugonjwa huo.”

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Ruto akabili ubadhirifu, ufisadi kufufua...

BORESHA AFYA: Vyakula kutuliza uchungu wa hedhi

T L