Makala

SHINA LA UHAI: Wanaume mashujaa dhidi ya saratani wanaohimili familia zao

November 19th, 2019 5 min read

Na PAULINE ONGAJI

HUKU ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya kuwatambua wanaume, takwimu zinaonyesha kwamba licha ya kuchangia pakubwa katika kuwashughulikia wagonjwa wa kansa, bado wahudumu wa kiume hawapokei utambuzi kuambatana na huduma wanazotoa.

Geoffrey Mwangi, 54, anawakilisha asilimia ndogo ya wanaume ambao wanakabiliwa na mzigo mzito wa kuwahudumia wagonjwa wa saratani.

Kwa takribani miaka mitano sasa mkazi huyu wa mtaa wa Kariobangi, jijini Nairobi, amekuwa akimshughulikia mkewe, Eunice Nyambura, 49, ambaye tangu 2014 amekuwa akiugua kansa ya matiti, maradhi ambayo yameathiri titi lake la kushoto, na hata kusababisha likatwe.

Bw Geoffrey Mwangi akiwa na mkewe Bi Eunice Nyambura wakati wa mahojiano nyumbani kwao mtaani Kariobangi, jijini Nairobi, Jumamosi, Novemba 16, 2019. Picha/ Pauline Ongaji

Bi Nyambura ambaye kabla ya kuanza kuugua alikuwa mkulima, sasa kwa mwaka mmoja amepooza upande wa kushoto na kamwe hawezi kujishughulikia kwa vyovyote.

“Kabla ya kupooza nilikuwa nikimhudumia lakini angeweza kujifanyia mambo ya kawaida kama vile kwenda chooni na kuoga. Lakini kwa sasa hawezi, na hivyo ni mimi nimekuwa nikikumbwa na majukumu haya yote,” aeleza Bw Mwangi.

Sio hayo tu kwani Bw Mwangi ambaye ni mchuuzi wa bidhaa za rejareja pia amekuwa akilazimika kumbeba mkewe mgongoni kila anapompeleka hospitalini. Kutokana na sababu kuwa hawezi kumudu nauli ya teksi, mara nyingi amekuwa akitumia mbinu ya usafiri wa umma.

Kwa hivyo mara nyingi amekuwa akimbeba hadi kwenye kituo cha matatu mtaani, kisha wanaelekea hadi hospitalini.

“Nikifika kwenye kituo cha mabasi katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta, tena nambeba, kumshukisha na kumkalisha kando. Nami nakimbia ndani kuchukua kiti cha magurudumu na kurejea kumchukua,” asema huku akiongeza kwamba kuna nyakati ambapo amekuwa akipata usaidizi kutoka kwa majirani.

Kwa kawaida siku yake huanza saa kumi na moja asubuhi, ambapo yeye huamka na kumchemshia mkewe maji ya kunywa na kumpa akiwa angali kitandani. “Ikiwa kuna maziwa basi nampikia chai, lakini ikiwa hakuna basi siku hiyo hanywi chai,” aeleza.

Baada ya kunywa chai anamuosha, anamrejesha kitandani na kuendelea na kazi zingine za nyumbani kama vile kufua na kuosha nyumba.

“Kabla ya saa saba mchana lazima nimtafutie mtu atakayemshughulikia na kumpa chakula huku nami nikienda kusaka riziki. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo nalazimika kutoenda kazini, hasa anapozidiwa na maumivu,” aeleza.

Kwa kawaida Bw Mwangi huandaa chakula kingi wakati wa jioni, ili kiweze kumtosheleza mkewe siku ifuatayo wakati wa mchana.

“Kuna nyakati ambapo mimi hupata usaidizi wa wasamaria wema ambao huleta chakula kilichopikwa.”

Lazima Bw Mwangi arejee angaa saa kumi jioni kutoka biashara zake ndogondogo ili amshughulikie mkewe.

“Hawezi kuenda msalani mweyewe ambapo mimi humuachia ndoo nyumbani anayotumia kwenda choo, na hivyo lazima nirejee mapema kumwaga uchafu na kumsafisha.”

Japo huenda ukadhani kwamba huu ni mzigo mkubwa, Bw Mwangi hana ugumu wowote wa kufanya kazi hii kwani anaamini kwamba ni jukumu lake kama mume, kumshughulikia mkewe.

“Ikiwa sitomshughulikia basi nani afanye hivi? Naamini kwamba ingekuwa ni mimi mgonjwa hivi, hata yeye angenishughulikia,” asema.

Lakini changamoto kuu imekuwa riziki. Mbali na kazi hizi, lazima Bw Mwangi ahakikishe kwamba anapata pesa sio tu za kukidhi mahitaji yao ya kila siku, bali pia za kugharamia dawa ambazo mkewe hutumia.

“Tangu aanze kuugua amefanyiwa awamu nne za tibakemia na kumi za tibaredio. Mbali na hayo, kwa takriban miaka miwili sasa amekuwa akitumia dawa maalum ambazo anapaswa kuendelea kuzitumia kwa miaka mitano. Dawa hizi zinagharimu Sh6,000, na lazima pia nitafute pesa hizi,” aeleza.

Aidha, anasema kwamba imekuwa vigumu kulipa kodi ya nyumba. “Nyumba hii yetu ni Sh3,000, pesa ambazo sizipati kwa urahisi, na hata tunavyozungumza nina deni la miezi mitano,” aeleza

Kwa Eugene Liondo, licha ya umri wake mdogo, amelazimika kupanua mawazo vilivyo na kufahamu mengi kuhusu jinsi ya kuwashughulikia wagonjwa wa saratani.

Liondo mwenye umri wa miaka 15 na ambaye anatarajiwa kujiunga na kidato cha pili mwakani, amekuwa akimshughulikia mamake, Bi Miliceny Kagonga tangu mwaka wa 2016 alipogundulika kuugua kansa ya njia ya uzazi.

“Mamangu alipatikana kuwa na hatua ya nne ya maradhi ya kansa ya njia ya uzazi. Wakati huo, alikuwa mdhaifu sana na hivyo pamoja na dadangu mdogo tulilazimika kurejea mashambani kwa nyanya yetu. Tulikuwa tukija wakati wa likizo na kumshughulikia kisha kurejea shule zilipofunguliwa,” aeleza.

Lakini wakiwa mashambani, habari zilienea kwamba mamake alikuwa amezidiwa na kwamba hakuwa na wa kumhudumia.

“Kwa hivyo mwisho wa mwaka wa 2017, wakati huo nikiwa na miaka 13 na mwanafunzi wa darasa la saba, tulirejea tena kuishi naye,” aeleza.

Mbali na kazi za kawaida za nyumbani kama vile kuosha nyumba na kufua, Liondo alikumbwa na jukumu ambalo kwa baadhi ya jamii ni mwiko kwa mtoto mvulana kumfanyia mamake.

“Mwanangu alikuwa akifua nguo zilizokuwa na uchafu wa damu. Nilikuwa nikienda choo kwenye ndoo. Ni yeye tu ndiye alikuwa anaumwaga na kusafisha kila kitu,” aleza Bi Kagonga.

Kando na hayo, Liondo pia alikumbwa na jukumu la kumpeleka mamake hospitalini huku akitembea idara tofauti katika hospitali ya Kenyatta kila mamake alipokwenda kutibiwa.

“Nimefanyiwa awamu tatu za tibakemia, awamu 25 za tibaredio na awamu tatu za brachytherapy ambapo mara nyingi mwanangu aliandamana nami hospitalini,” asema Bi Kagonga.

Lakini haijakuwa rahisi kwa Liondo.

“Kwa muda nilisikia watu hata jamaa zetu wakizungumza vibaya na kusema kwamba mamangu hangeweza kupona, huku baadhi yao wakikataa kujihusisha nasi,” aeleza Liondo.

Pia, haikuwa rahisi ambapo kuna nyakati ambapo mvulana huyu alilemewa na mihemko na kulia na hata kuzimia, hali ya mamake ilipozidi kuwa mbaya.

Lakini Bi Kagonga alibahatika kupata nafuu na sasa amekuwa akipokea matibabu machache huku akiendelea na shughuli zake za kawaida huku akisubiri kupata pesa ili afanyiwe utaratibu kubaini iwapo bado ana maradhi ya kansa ya njia ya uzazi.

Lakini kwa Bw Harun Mwangi, hakubahatika, kwani majuma mawili yaliyopita alimpoteza mkewe, marehemu Rosemary Wangu kutokana na kansa ya matiti.

Mkewe alipokuwa akiugua, mkazi huyu wa mtaa wa Mundia, mjini Thika alikuwa na jukumu la kumshughulikia kwa vyovyote hasa ikizingatiwa kwamba kwa miaka mitatu kabla ya kifo, Bi Wangu alikuwa amelemazwa na maradhi haya.

Ni maradhi yaliyomfanya kupoteza titi lake la kushoto huku hali yake ikizidi kuwa mbaya hasa ikizingatiwa kwamba mwanzoni uchunguzi wa kutambua maradhi haya ulikuwa wa makosa.

Ugonjwa huu ulikuwa umemlemaza kiasi cha kwamba hangeweza kuzungumza na hata kujishughulikia kama vile kuoga na kwenda choo au kutembea. Kwa hivyo Bw Mwangi aliachiwa majukumu haya, suala lililomlazimu kuacha kazi ili kumshughulikia.

“Mara nyingi alikuwa anategemea nepi. Hakuwa anaweza kuvaa nguo. Ilikuwa lazima nimuoshe nimpikie, nimsafishie mavazi na kumbadilisha nguo na bandeji kifuani ili kuuguza kidondo kifuani,” asema Bw Mwangi.

Matibabu ya mkewe

Hii ni mbali na kitita kikubwa cha pesa alicholazimika kutumia katika matibabu ya mkewe. Sio hayo tu, uchunguzi huo wa kimakosa ulimlazimu kumpeleka mkewe katika hospitali mbali mbali kwa matumaini ya kupata tiba, bila mafanikio, suala lililowafilisi na kuwaacha bila chochote.

Wakati huo, walilazimika kutegemea wahisani, suala ambalo anasema lilimshusha hadhi kama mwanamume. Lakini kwa sasa japo bado anamuomboleza mkewe, Bw Mwangi hana budi ila kupata nguvu na kuendelea kuwashughulikia watoto wawili alioachiwa.

Utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na shirika la National Alliance for Caregiving (NAC) nchini Amerika ulionyesha kwamba asilimia 58 ya watu wanaowashughulikia wagonjwa wa kansa ni wanawake.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka wa 2012 na kituo cha utafiti wa huduma ya kiafya na ukunga katika Australian National University nchini Australia, ulionyesha kwamba japo wanaume pia wamechangia pakubwa katika kuhudumia wagonjwa wa kansa, sio wengi wanaotambuliwa kwa kazi wanayofanya.

Hii ni huku wataalamu wakisema kwamba, sawa na wahudumu wa kike, pia wa kiume wanakumbwa na matatizo yanayotokana na kumshughulikia jamaa mgonjwa, kama vile kuhofia kifo na kukumbwa na mafadhaiko, kwa maana kwamba pia wao wanapaswa kushughulikiwa.

Wahisani wanaoweza kusaidia familia hizi wanaombwa kuwasiliana na shirika la Symbol Of Hope Warriors, kupitia nambari 0724904284