Makala

SHINA LA UHAI: Wasiwasi wa wauguzi uhaba wa damu ukikithiri

March 3rd, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

MAELFU ya wagonjwa nchini wanakabiliwa na hatari ya kuaga dunia baada ya kubainika kuwa nchi hii inakabiliwa na upungufu mkubwa wa damu kwa mahitaji ya kiafya.

Ni majuzi tu ripoti zilisema wagonjwa 10 wa saratani katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta walilazimika kutumwa nyumbani kutokana na ukosefu wa damu waliyohitaji kwa matibabu ya tibakemia.

Shirika la afya Ulimwenguni, (WHO), linakadiria kuwa ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa kuongeza damu inayohifadhiwa kwa mahitaji ya dharura, Wakenya wengi watapoteza maisha yao.

Hofu ya wataalam na washikadau katika sekta ya afya ni kuwa hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi ikiwa Kenya itakumbwa na janga kubwa linalohitaji watu wengi kuongezewa damu kwa dharura.

“Tuko katika hali mbaya mno kwa sababu kiwango cha damu kinachohifadhiwa na Serikali hakitoshi mahitaji ya wagonjwa,” asema Fridah Govedi, mkurugenzi wa kituo cha kitaifa cha kuhifadhi damu.

Dkt Govedi asema kuwa idadi ya watu wanaohitaji kuongezewa damu inazidi kuongezeka kila siku na ipo haja ya mikakati kubuniwa ili kuhamasisha watu wengi watoe damu.

“Ni kweli nchi hii inakabiliwa na upungufu wa damu jambo ambalo ni hatari kwa nchi,” asema Dkt Fidelis Ouma anayehudumu na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Afya. Anatoa mfano wa wakati wa mashambulizi ya kigaidi na ajali za barabarani ambapo damu huhitajika kwa wingi kuokoa maisha ya waathiriwa.

Mahitaji ya dharura

“Inaonyesha wazi kuwa Kenya inafaa kuwa na damu ya kutosha ili kukabiliana na mahitaji ya dharura,” aeleza.

Dkt Ouma asema kuwa habari njema ni kwamba idadi ya watu wanaojitolea kutoa damu imeonyesha dalili za kuimarika japo haijafikia kiwango cha mataifa mengine na kuthibitisha hofu ya washikadau kuhusu uwezekano wa kutoafikia kiasi cha kutosha cha damu.

Kinachowafanya wengi kuchelea kutoa damu, aeleza, ni hofu kuwa huenda wakapimwa virusi vya ukimwi na magonjwa mengine na mila zinazopotosha kuhusu utoaji wa damu.

“Kuna jamii zinazoamini kuwa damu inaweza kutumiwa katika ushirikina. Wengine wanapotoshwa kwa kuambiwa kuwa watapimwa ukimwi jambo linalowafanya wengi kujikokota kutoa damu,” asema na kuongeza kuwa ingawa damu inayohifadhiwa kwa mahitaji ya afya ni sharti iwe salama, wahudumu wa afya hawapimi watu ukimwi bila hiari yao.

Na huku Wakenya wakiendelea kuwa ‘wachoyo’ na damu yao idadi ya wanaohitaji kuongezewa damu inazidi kuongezeka.

Kulingana na WHO, mataifa yaliyo na upungufu wa damu salama kwa mahitaji ya kiafya yanakabiliwa na tishio la kutoafikia malengo ya kudumu kuhusu afya.

Shirika hilo linasema kuwa asilimia 25 ya vifo vinavyotokea akina mama wakijifungua vinasababishwa na upungufu wa damu mwilini huku asilimia 15 ya vifo vya watoto barani Afrika vikitokana na hali kama hiyo.

Wataalam wanapendekeza kuwa serikali isilegeze kampeni ya kuwahamasisha watu umuhimu wa kutoa damu.

Dkt Govedi aeleza kuwa kampeni iliyoendeshwa na shirika lake imeanza kuzaa matunda na idadi ya watu waliojitolea kutoa damu imeongezeka.

Takwimu za kituo cha kuhifadhi damu cha kitaifa zinaonyesha kuwa kwa mwaka Kenya huhitaji paini 500,000 za damu lakini ni 164,275 ambazo hukusanywa kwa mwaka.

Kuokoa maisha

Kituo hicho kinasema watu 200,000 huwa wanahitaji kuongezewa damu kwa mwaka ili kuokoa maisha yao.

Kituo hicho kinasema katika kila dakika tatu watu saba huwa wanahitaji kuongezwa damu nchini ili kuokoa maisha yao.

Kuna vituo 27 vya kutoa damu kote nchini ambavyo watu wanaweza kutembelea kutoa damu. Vituo hivi vinapatikana katika hospitali za rufaa za kaunti za kiwango cha Level Five.

Aidha, mashirika ya kukabiliana na Mikasa yamekuwa yakishirikiana na kituo Cha Hifadhi ya Damu kufanya kampeni za watu kutoa damu maeneo tofauti. Kila mwaka wakati wa Sikukuu ya Wapendanao, kituo hicho kimekuwa kukiandaa kampeni ya watu kutoa damu kama njia ya kuonyesha upendo.

Licha ya kampeni hizi, Kenya haina damu ya kutosha kwa mahitaji ya afya.

Dkt Ouma anasifu juhudi za shirika la Msalaba Mwekundu za kuhakikisha kuwa nchi hii imekuwa na hifadhi ya damu ya kutosha na salama kwa mahitaji ya kiafya.

Mtaalam huyu anatoa wito kwa mashirika mengine kujiunga na kampeni hii Ili watu wengi waelewe umuhimu wa zoezi hili kwa taifa.

Anasema kuwa kwa kuokoa maisha ya watu nchi itapata kustawi na kuimarika kiuchumi.

“Ni vyema pia kuwaelimisha watu wadumishe afya njema ili kuepuka maradhi ambayo yanaweza kuwazuia kutoa damu kwa mahitaji ya afya,” apendekeza Dkt Ouma.

Ili kuepuka changamoto zilizopo, wataalam wanapendekeza kuwa Wizara ya Afya itenge pesa za kutosha katika bajeti yake za kuendesha shughuli hiyo kila mwaka jambo linaloungwa mkono na wahudumu wa afya nyanjani.

Dkt Ouma asema shughuli hii inahitaji mchango wa watu wote.

Mashirika ya kijamii

Anawahimiza watu binafsi, mashirika ya kijamii na kampuni kushiriki kikamilifu katika shughuli ili kuepusha nchi hii na hatari inayoikodolea macho.

“Ni wajibu wa kila mmoja kuchukua hatua na kukubali ukweli ili tuepushe nchi na hatari inayonukia kwa kukosa damu,” asema na kuongeza kuwa majanga yameongezeka kote na yanahitaji idara za serikali kuwa zimejiandaa.

Hospitali Kuu ya Kenyatta inasema ina chini ya asilimia 20 ya damu katika hifadhi yake.

KNBTS inashirikiana na mashirika ya BloodlLink Foundation, Shirika la Msalaba Mwekundu, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU), NHIF na AMREF miongoni mwa mengine katika juhudi za kuimarisha utoaji wa damu nchini.

Kaunti ambazo zinakumbwa na uhaba mkubwa ni Nairobi, Embu, Nakuru, Kisumu, Mombasa, Machakos na Kisii. Nyingine ni Meru, Kericho, Nyeri, Garissa, Bungoma, Migori, Busia na Narok. Imebainika kuwa Kenya pia ina uhaba wa kemikali za kusafisha damu iliyotolewa na hifadhi zake.