SHINA LA UHAI: Wengi wakabiliwa na upofu unaoweza kuepukika

SHINA LA UHAI: Wengi wakabiliwa na upofu unaoweza kuepukika

Na PAULINE ONGAJI

CYBIL Ambogo, 25, alipogundulika kuugua myopia (near-sightedness), tatizo la macho ambapo mwathiriwa huona vitu vilivyo karibu naye pekee, hakujua kwamba safari ya kutafuta matibabu ingekuwa ndefu.

Alianza kukumbwa na matatizo ya kuona mwaka wa 2012, wakati huo akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule moja ya upili katika Kaunti ya Kakamega.

“Nilikuwa na mazoea ya kukaa nyuma darasani. Mambo yalikuwa shwari hadi nilipoanza kushindwa kuona ubao vizuri. Mwanzoni nilipuuza na kudhani kwamba tatizo lingetatuliwa pindi tu nitakaposonga karibu na ubao,” aeleza.

Kwa muda hali ilikuwa sawa baada ya kusonga karibu na ubao. Lakini uwezo wake wa kuona uliendelea kudorora siku zilivyokuwa zikisonga, hasa katika mazingira yenye mwangaza mwingi.

Hali ilizidi kuwa mbaya msimu wa mtihani ulipowadia.

“Mara nyingi nilitaabika kufanya mitihani yangu na hasa endapo karatasi la mtihani lingekuwa la rangi nyeupe,” aeleza.

Bi Ambogo anasema alisumbuka sana kupata usaidizi, huku vizingiti vikuu vikiwa kufikia huduma ya matibabu na gharama yake.

“Kumbuka kwamba shule yangu ilikuwa eneo la Kakamega, na wakati huo ilikuwa vigumu kupata mtaalamu wa macho sehemu hiyo. Kwa hivyo nililazimika kusafiri hadi Kaunti ya Kisumu ili kufanyiwa uchunguzi,” anasema.

Baada ya hapo, changamoto ilikuwa gharama ya miwani.

“Wazazi wangu walilazimika kutoa Sh8, 700 ili kulipia bidhaa hii, na haikuwa rahisi,” aeleza.

Lakini takriban mwongo mmoja baadaye, Bi Ambogo anafurahia kuendelea na maisha, huku kufikia sasa akiwa amebadilisha miwani yake mara moja.

Mtaalamu wa macho Diana Langat (kushoto), akimpima miwani Cybil Ambogo (mgonjwa wa macho) katika duka la Lapaire Glasses, Nairobi mnamo Mei, 15, 2021. Picha/ Bonface Bogita

Ana bahati kwamba tatizo lake lilitambuliwa mapema na kutibiwa. Yeye ni asilimia ya watu wachache barani Afrika walio na uwezo wa kufikia huduma hizi, huku wengi wakiendelea kutaabika bila usaidizi.

Ni tatizo ambalo limechangia visa vya upofu, sio tu hapa nchini, bali Afrika nzima. Kulingana na Shirika la Afya Duniani -WHO- watu milioni 28 duniani kote, wanakumbwa na matatizo ya kuona, miongoni mwao wakiwa Wakenya 750,000.

Kati ya watu milioni 39 wanaokumbwa na tatizo la upofu duniani kote, 224,000 ni Wakenya. Ajabu ni kwamba asilimia 80 ya upofu nchini Kenya ni kutokana na sababu ambazo zaweza kutibiwa.

Mojawapo ya sababu kuu ni refractive errors, umbo la jicho kushindwa kupinda mwangaza vizuri na hivyo kumsababisha mhusika kuona picha zilizo na ukungu.

Matatizo mengine yanayochangia upofu kwa kukosa tiba ni pamoja na myopia (near-sightedness) hali iliyomkumba Bi Ambogo; hyperopia (far-sightedness) tatizo la kuona vitu vilivyo mbali pekee; presbyopia (kupoteza uwezo wa kuona kutokana na umri), na astigmatism (shida ya kuona iinayotokana na tatizo la konea).

Mbali na hayo kuna matatizo zaidi kama vile mtoto wa jicho au cataract (tatizo ambalo lenzi ya macho hufunikwa kwa wingu na hivyo kupunguza uwezo wa kuona); trachoma (maradhi ya kusambaa yanayosababishwa na bakteria inayoitwa chlamydia trachomatis); diabetic retinopathy (hali inyosababishwa na maradhi ya kisukari); glaucoma (kikundi cha matatizo ya macho yanayoharibu neva za sehemu hii), na upofu wa utotoni kutokana na ukosefu wa huduma ya tiba.

Hapa barani takwimu kuhusu matatizo ya umbo la jicho kushindwa kupinda mwangaza vizuri (refractive errors) sio bayana. Hata hivyo kwa mujibu wa utafiti wa kampuni ya Lapaire Glasses, Nairobi ambayo imehusika katika uchunguzi wa zaidi ya watu 60,000 barani kote, 60% ya waathiriwa wanaweza tibiwa.

Kwa mfano, mojawapo ya njia za kukabiliana na hali hii ni kuvalia miwani ifaayo baada ya kukaguliwa na mtaalamu. Lakini upungufu wa wataalamu, vile vile ukosefu wa uwezo wa kifedha ni changamoto kuu.

“Wengi hawawezi kumudu gharama ya huduma hii kutokana na umaskini na ukosefu wa bima ya kusimamia miwani,” yasema kampuni ya Lapaire.

Aidha, kuna tatizo la ugumu wa kufikia huduma za daktari wa macho kutokana na idadi ndogo ya wataalamu hawa.

Kwa mfano hapa nchini, uwiano baina ya daktari wa macho na idadi ya wagonjwa ni 1: 600,000, tofauti na mapendekezo ya WHO ya daktari mmoja kwa wagonjwa 250,000.

Aidha, inakadiriwa kwamba barani Afrika, watu milioni 550 wanahitaji miwani, lakini ni asilimia moja pekee walio na uwezo wa kufikia vifaa hivi (watu 1.3 milioni).

Wizara ya Afya nchini inakadiria kwamba asilimia 15.5 ya Wakenya (watu 7.5 milioni), wanahitaji huduma za afya ya macho kama vile upasuaji, tiba ya macho na urekebishaji kwa miwani.

Ni suala ambalo limesababisha wengi kutafuta mbinu mbadala za kupata miwani.

“Kwa mfano kuna wale wanaoamua kutumia miwani kwa pamoja na wenzao, huku wengine wakiamua kununua miwani bandia mtaani,” asema Diana Lang’at, mtaalamu wa macho na miwani jijini Nairobi.

Kulingana na Bi Lang’at, kuna hatari kubwa ya kufanya hivi.

“Kwanza, watu wanapaswa kuelewa kwamba japo huenda ukapatikana na tatizo sawa na la mwenzio, viwango vya kasoro huwa tofauti, kumaanisha kwamba shida yenu haiwezi kutatuliwa kwa aina moja ya lenzi,” aeleza.

Kuna hatari kadha wa kadha ambazo zaweza jitokeza kwa kuvalia miwani aina yoyote ile unayonunua mtaani.

“Kuna uwezekano wa kukumbwa na tatizo la kudumu la retinal detachment, hali ambayo huenda ikakosa kutatuliwa kabisa, na hivyo kusababisha matatizo ya kudumu kiwango kwamba hata baada ya kuvalia miwani, bado mwathiriwa atashindwa kuona vizuri,” aeleza.

Mbali na hali ngumu ya kiuchumi, Bi Lang’at asema kwamba, hapa nchini ukosefu wa elimu kuhusu afya ya macho unachangia visa vya matatizo ya kuona.

Kulingana naye kuna tahadhari nyingi ambazo zikifuatwa, huenda tukapunguza visa vya matatizo ya kuona.

Kwa mfano, asema, kuna matatizo yanayosababishwa na mtindo wa maisha ambayo yaweza suluhishwa kwa kula mboga na kunywa maji ya kutosha kuzuia ukavu.

“Aidha, kuna matatizo ambayo husababishwa na mwangaza kutoka kwenye skirini kabla ya kulala na miyale ya jua,” aongeza.

Katika enzi hizi za teknolojia ya mawasiliano ambapo watu wengi wanatumia muda mwingi kwenye kompyuta na vifaa vingine vya kieletroniki, anasema kuna athari ambazo zaweza kudhibitiwa endapo muhusika atakuwa na ufahamu wa kutosha.

“Kwa mfano hakikisha unapotumia vifaa vya kieletroniki kama simu na kompyuta, unafuata sharti la 20:20:20 ambapo kila baada ya dakika 20 za matumizi ya vifaa hivi, unapumzika kwa sekunde 20 na kuelekeza macho yako kwa kitu kilichoko futi 20,” aeleza Bi Lang’at.

Kulingana na Oliver Wambile, afisa wa mahusiano mema wa kampuni ya Lapaire Glasses, haja ya kuhamasisha jamii na kutoa tiba ya macho barani Afrika ni kubwa na ni jambo linalofaa kuchukuliwa kuwa la dharura.

“Ndiposa tumejipa jukumu la kuendesha shughuli za kuhamasisha jamii kuhusu matatizo ya macho na hata kutoa huduma za bure kupima macho,” aongeza.

You can share this post!

ONYANGO: BBI: Hisia za wanasiasa zadhihirisha unafiki wao

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nakumbwa na hofu kuu ya kujifungua