Michezo

Shinikizo EPL ikamilike Juni 30

April 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WASIMAMIZI wa klabu za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanatarajiwa kujadili kuhusu athari za kuwawekea waendeshaji wa kipute hicho msimu huu wa 2019-20 makataa ya kukikamilisha rasmi kufikia Juni 30, 2020.

Ingawa si klabu zote zitahusishwa katika majadiliano hayo, ukweli ni kwamba uwezekano wa kurejelewa upya kwa kivumbi hicho mnamo Mei 2020 utakuwa mgumu huku wamiliki wa baadhi ya vikosi wakipania kutafuta jinsi ya kuepuka utata wa hali zitakazohusiana na mikataba ya wachezaji.

Kandarasi za wachezaji wengi wa EPL zinatazamiwa kutamatika mnamo Juni 30 na baadhi ya wanasoka hao ni kiungo wa Chelsea, Willian na beki matata wa Tottenham Hotspur, Jan Vertonghen.

Isitoshe, Liverpool wanatarajiwa kubadilisha mdhamini wa jezi zao kutoka kampuni ya New Balance hadi Nike; sawa na Watford na Newcastle United pia wamefichua azma ya kubadilisha mdhamini wa jezi za wanasoka wao.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ambalo limekiri kuelewa hali ilivyo kwa sasa katika ulingo wa kabumbu na limefichua mipango ya kuwapa vinara wa klabu idhini ya kuwaachilia au kurefusha muda wa kuhudumu kwa wachezaji wote ambao mikataba yao inatamatika mwishoni mwa Juni 2020. Msimu wa sasa wa soka katika takriban mataifa yote duniani bado umesitishwa kwa muda usiojulikana kwa sababu ya virusi vya corona.

Hata hivyo, kisheria, wachezaji hawawezi kulazimishwa kutoa saini kandarasi mpya katika klabu wasizotaka kuziwajibikia zaidi. Hili linaibua uwezekano wa baadhi ya vikosi kupoteza huduma za wanasoka wao tegemeo kabla ya hata kampeni za msimu huu kutamatishwa rasmi.

Japo maoni tofauti yametolewa kuhusiana na masuala haya, nyingi za klabu zinataka Juni 30 iwe siku ya mwisho ya kutamatika rasmi kwa soka ya EPL katika msimu huu wa 2019-20 hata kama janga la corona halitakuwa limedhibitiwa vilivyo.

Kwa mujibu wa Tony Bloom ambaye ni mmiliki wa kikosi cha Brighton, hatua hiyo italetwa mwanga zaidi kuhusiana na jinsi msimu wa 2020-21 utakavyokuwa kwa sababu huo ndio muhula muhimu zaidi kwa sasa hata kuliko huu wa 2019-20.

Aidha, ameshikilia kwamba itakuwa vigumu zaidi kwa mechi zozote za msimu huu kupigwa baada ya Juni 30.

“Kuna wakati ambapo huwezi kusubiri zaidi na ikabidi uchukue hatua. Naona ugumu wa mchuano wowote wa EPL kusakatwa baada ya Juni 30 kwa sababu ya masuala ya mikataba, japo hali ya sasa inahitaji kutathminiwa upya,” akasema Bloom.

Pendekezo la Bloom kwa vinara wa soka ya Uingereza ni kupandisha daraja vikosi vya Leeds United na West Bromwich Albion ambavyo vimejitahidi zaidi katika Ligi ya Daraja la Kwanza msimu huu hadi EPL msimu ujao.

Kwa mtazamo wake, itakuwa busara iwapo msimu huu wote wa EPL utafutiliwa mbali, pasiwepo mshindi wala vikosi vyovyote vitakavyoteremshwa ngazi.

“Vikosi vyote vilivyoshiriki EPL msimu huu visalie kuwania ubingwa wa muhula ujao bila ya chochote kudondoshwa. Hata hivyo, Leeds na West Brom wajumuishwe ili kipute cha EPL kiwe na washiriki 22 mnamo 2020-21,” akaongeza.

Mtazamo wa Bloom umepingwa na kocha Chris Wilder wa Sheffield United ambaye ametaka vipute vya EPL, Europa League na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kutamatishwa rasmi hata kama itachukuwa muda kiasi gani kwa soka ya Ligi Kuu tano za bara Ulaya kurejelewa.

Kwa mujibu wa Wilder, upo muda wa kufanyia msimu ujao mabadiliko makubwa, ikiwemo mikakati ya kucheza nyingi za mechi katikati ya wiki na kupangua kalenda ya mechi za kimataifa za kirafiki na za kufuzu kwa baadhi ya mashindano ambayo tayari yameratibiwa hadi 2021 na 2022.