Habari Mseto

Shinikizo Kiunjuri ajiuzulu

November 2nd, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Nandi Hills Afred Keter sasa anamtaka Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kujiuzulu baada ya kubainika kuwa mahindi ya thamani ya Sh7.6 bilioni yanahifadhiwa katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) ni mabovu.

Mbunge huyo Alhamisi alimpa waziri huyo makataa ya siku saba kung’atuka la sivyo atawasilisha hoja ya kumwondoa afisini kwenye Bunge la Kitaifa litakaporejelea vikao vyake Jumanne ijayo baada ya likizo fupi.

“Licha ya kupewa mamlaka na rasimali zote hitajika ameshindwa kukabiliana na magenge ambayo yanavuruga sekta ta mahindi kwa hivyo anafaa kujiuzulu mara moja ili kutoa nafasi kwa watu wengine kusimamia wizara hiyo,” Bw Keter akasema alipohutubia kikao cha wanahabari katika majengo ya bunge.

“Changamoto kubwa katika wizara ya Kilimo sio walaghai na wahusika wengine wa ufisadi bali ni utepetevu wa Waziri Kiunjuri. Iweje magunia milioni nne ya mahindi yanayohifadhiwa na NCPB yana sumu ya aflatoxin ilhali watu waliowsilisha mahindi hayo hawajachukuliwa hatua za kisheria?” akauliza.