Habari

Shinikizo kumtaka Chebukati pia ajiuzulu

April 17th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

DARUBINI sasa imeelekezwa kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, na makamishna wawili waliobaki kwenye tume hiyo baada ya wenzao kujiuzulu.

Viongozi mbalimbali walisema inastahili Bw Chebukati ajiuzulu pamoja na makamishna Boya Molu na Prof Abdi Guliye, sawa na jinsi Naibu Mwenyekiti Consolata Nkatha Maina, Bw Paul Kurgat na Bi Margaret Mwachanya walivyojiuzulu  Jumatatu.

Bi Maina na wenzake walimshutumu Bw Chebukati, na kusema ameshindwa kuongoza tume kwa uthabiti.

“Katika uongozi wake, tume imegeuka kuwa kitengo cha kusambaza habari za kupotosha, kutoaminiana na kujitakia makuu ya kibinafsi,” wakasema kwenye taarifa iliyosomwa na Bi Mwachanya kwenye kikao cha wanahabari Nairobi.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen, na mwenzake wa Wachache, Bw James Orengo, walisema hatua ya makamishna kujiuzulu ni ishara tosha ya uozo ulio katika IEBC.

Bw Murkomen aliwapa makamishna hao siku saba waondoke la sivyo bunge libuni jopokazi kuchunguza utendakazi wao.

“Wito wangu kutaka makamishna wa IEBC wajiuzulu unatokana na mizozo ya hivi majuzi.

Inaonekana mwenyekiti hajawahi kuwa msimamizi awali kabla ya kuchaguliwa kusimamia IEBC,” akasema seneta huyo wa Elgeyo Marakwet.

Kwa upande wake, Bw Orengo alisema: “Hakuna cha makamishna wema wala wabaya katika IEBC. Asasi hiyo ina laana. Kujiuzulu kwa makamishna ni dalili ya maradhi yasiyotibika yanayokumba tume hiyo.”

 

Mtindo wa ‘timua timua’

Endapo makamishna wote watang’atuliwa, Kenya itakuwa ikiendeleza mtindo wa kuondoa makamishna wa tume za uchaguzi mamlakani kabla ya muda wao kukamilika, tangu Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Katika mwaka wa 2008 makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) wakiongozwa na marehemu Samuel Kivuitu, waliondolewa wakati bunge lilipounda Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC) kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Bw Issack Hassan, aliyeongoza IIEC (baadaye IEBC), alibanduliwa pamoja na wenzake mwaka wa 2016, walipoandamwa na madai ya ufisadi.

Wabunge Kanini Kega (Kieni), Kathuri Murungi (Imenti Kusini), James K’oyoo (Muhoroni) na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru, jana walisema inafaa maafisa wote wabadilishwe.

“Bw Chebukati anafaa kufanya jambo la uungwana ambalo ni kujiuzulu. Makamishna waliobaki pia wafuate nyayo zake,” akasema Bw Kega.

 

Maafisa wapya

Wakizungumza wakiwa Nanyuki, Bi Waruguru na Bw K’oyoo walisema IEBC inahitaji maafisa wapya.

Wito wa kutaka makamishna wachunguzwe ulitolewa pia na Shirikisho la Watumizi Bidhaa la Kenya (COFEK).

Kwa upande wao, wazee wa jamii za Rift Valley wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mzee Gilbert Kabage, walisema kuwa katika hali yake ya sasa, tume hiyo haiwezi kuaminiwa kuendesha uchaguzi mwingine wowote, kwani imezorota mno.

Bw Chebukati aliahidi kutoa taarifa ya kina kuhusu hali ya IEBC baadaye, ingawa taarifa hiyo haikuwa imetolewa kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa.

Haya yametokea huku uchunguzi alioagiza ufanywe kuhusu madai ya ubadhirifu katika IEBC ukiendelea, sawa na uchunguzi mwingine unaoendelezwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Umma (PAC).