Michezo

Shinikizo mashabiki warejee uwanjani

July 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Sinisa Mihajlovic wa Bologna amesema itakuwa heri kwa kipute cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kutochezwa kabisa msimu ujao iwapo kitaendelea kusakatwa bila ya mahudhurio ya mashabiki uwanjani.

Msimu huu wa Serie A ulirejelewa Juni 13, 2020 bila mashabiki uwanjani baada ya kusitishwa kwa miezi mitatu kutokana na janga la corona.

Mihajlovic, 51, alihiari kuendelea kudhibiti mikoba ya Bologna licha ya vipimo vya afya alivyofanyiwa kubaini kuwa anaugua saratani ya damu (leukaemia).

Kwa mujibu wa mkufunzi huyo, mechi za ligi kwa sasa zimepoteza ladha na ni zinaudhi sana huku kiwango cha ubora kikishuka zaidi kuliko hata mechi za nyakati za vipindi vya mazoezi.

“Si suala la wachezaji na wanasoka kukosa hamasa, lakini kucheza bila mashabiki uwanjani ni kuchungu sana na hakusaidii kitu. Kunaudhi na kuchukiza,” akatanguliza.

“Kucheza uwanjani bila mashabiki kunachosha na kuchusha. Naelewa kwamba ilikuwa ndiyo njia ya pekee kwa kampeni za msimu huu kukamilika. Hata hivyo, nina matumaini kwamba viwanja kwa sasa vitakuwa wazi kwa mashabiki kuanzia Septemba 2020,” akasema.

“Iwapo ningepewa fursa ya kuchagua kati ya kutoongoza kabisa kikosi change kucheza msimu ujao au kucheza bila mashabiki uwanjani, ningekuwa mwepesi sana wa kuteua hilo la kwanza: kutocheza kabisa. Na ieleweke kwamba si mimi pekee ninayefikiria hivyo. Hizi mechi bila mashabiki ni duni zaidi kuliko hata za mazoezi kambini,” akaongeza.

Bologna kwa sasa wanashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama 43 sawa na Fiorentina.

Waziri wa michezo nchini Italia, Vincenzo Spadafora amesema kwamba huenda mashabiki wakakubaliwa uwanjani kuhudhuria mechi mbalimbali kuanzia Septemba 2020 japo maamuzi hayo yatategemea hali ya afya ya umma nchini Italia kufikia wakati huo.