Habari Mseto

Shinikizo Naibu Chansela ajiuzulu kufuatia mauaji ya mwanachuo

March 4th, 2018 1 min read

Na DAVID MUCHUI

MAUAJI ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Meru Evans Njoroge (pichani kushoto), yamezua malumbano makali kuhusu changamoto chuoni humo.

Huku uchunguzi ukiendelea kuhusu mauaji hayo ya mtetezi wa wanafunzi, shinikizo inaendelea kutolewa ili naibu chansela wa chuo hicho Prof Japhet Magambo (pichani kulia) ajiuzulu.

Prof Magambo ameongoza chuo hicho kwa miaka tisa sasa. Jumamosi, uchunguzi wa maiti ya mwendazake ulifanywa.

Viongozi kadhaa kutoka Meru wameitisha uchunguzi wa kina kuhusiana na mauaji hayo na kumtaka Prof Magambo kuondoka kwa madai ya usimamizi mbaya wa chuo hicho.

Wazee wa Njuri Ncheke ambao walitoa ekari 641 za ardhi kwa ujenzi wa chuo hicho jana walikutana ili kujadili changamoto zinazoathiri chuo hicho.

Chama cha wahudumu wa vyuo viku (KUSU), tawi la Chuo Kikuu cha Meru walisema changamoto zinazoendelea kushuhudiwa chuoni humo zinatokana na usimamizi mbaya.

Wanafunzi wamekuwa wakiitisha kupunguzwa kwa karo kutoka mwaka jana. Chuo hicho, bewa kuu, kilifungwa Oktoba 18, 2017 na Februari 1, 2018 kutokana na migomo ya wanafunzi.

Wanajamii wa soko ya Nchiru (ambako chuo hicho kimejengwa) walilalamikia migomo ya mara kwa mara kwa kusema ilikuwa ikiwafanya kupata hasara kubwa kutokana na uharibifu wa wanafunzi.

“Hatujui amani ni nini katika kijiji hiki kwa sababu ya vurugu kati ya polisi na wanafunzi. Polisi hurusha vitoa machozi hata nyumbani na kama jamii tunaomboleza na tunawaunga mkono wanafunzi kutafuta wanachotaka,” alisema Bw Ken Mwiti, mkazi wa eneo hilo.