Shinikizo Uingereza ichunguze mwanajeshi anayehusishwa na mauaji

Shinikizo Uingereza ichunguze mwanajeshi anayehusishwa na mauaji

Na MARY WAMBUI

SERIKALI ya Uingereza imeshinikizwa kufanya uchunguzi wa ndani na kumshtaki mwanajeshi wake, anayetuhumiwa kumuua mwanamke Mkenya kabla ya kutupa mwili wake.

Mwanajeshi huyo amedaiwa kutekeleza mauaji hayo alipokuwa kwenye mafunzo ya kijeshi nchini Kenya mnamo 2012.

Imebainika kuwa marehemu Agnes Wanjiru, wakati huo akiwa na umri wa miaka 21 na mwanawe wa miezi mitano, alionekana mara ya mwisho katika hoteli ya Lions Court mjini Nanyuki, kabla ya kutoweka.

Miezi mitatu baadaye, mwili wake ambao ulikuwa umeanza kuoza, ulipatikana ndani ya tangi la maji na mhudumu wa hoteli hiyo. Wakati mwili huo ulipopatikana, mafunzo hayo ya kijeshi yalikuwa yamekamilika na wanajeshi kurejea kwao.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa alifariki kutokana na majeraha ya kudungwa kisu kifuani na tumboni.

Hata hivyo, uchunguzi wa polisi mjini Nanyuki, ulikosa kuzaa matunda huku familia ya marehemu ikiendelea kusaka majibu kuhusu tukio lililotamatisha uhai wa mwanao zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Ufichuzi wa jarida la Sunday Times wikendi, ulisema kuwa wanajeshi wanne waliokodisha hoteli hiyo, walikuwa wametambuliwa na kuwaomba polisi nchini humo kuwahoji na kuchukua sampuli yao ya DNA.

Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ilisema kuwa uchunguzi kuhusu kifo hicho ulikwama, kwa kuwa sampuli ya DNA ya wanajeshi hao haikuchukuliwa.

Jana, Balozi wa Uingereza nchini, Bi Jane Marriott, kupitia taarifa alisema kuwa mnamo 2012, kitengo cha uchunguzi cha taifa hilo, kilitoa taarifa kwa polisi wa Kenya kuhusu masuala yaliyoibuliwa wakati huo kuhusiana na kifo cha Bi Wanjiru.

You can share this post!

Familia ya Masten Wanjala yamkana, mwili wasalia mochari

WANTO WARUI: Serikali isaidie kutafuta suluhu kwa visa vya...

F M