Habari za Kitaifa

Shinikizo za kumtaka Chebochok ajiuzulu zazidi


WAKURUGENZI wa Bodi ya Majanichai wa kiwanda cha Tegat /Toror wamemtaka John Chebochok ajiuzulu kutoka kwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Shirika la Ustawi wa Majanichai (KTDA) zoni ya Ainamoi.

 Chebochok alichaguliwa kama mkurugenzi wa KTDA katika zoni hiyo lakini anapingwa kutoka na sababu za kimaadili. Hii ni kutokana na kukabiliwa na sakata ya kuwadhulumu kimapenzi wale ambao wanafanya kazi katika sekta ya majanichai hapo awali.

Kwa mujibu wa bodi ya Tegat/Toror kujiuzulu kwake kutawaokoa wakulima wadogo wadogo wa majanichai dhidi ya kupoteza biashara.

Tayari kampuni kubwa za Liptons na James Finlays zimesitisha ununuzi wa majanichai kutoka kwa kiwanda hicho hadi Bw Chebochok ajiuzulu.

“Kama bodi tunamtaka Chebochok ajiuzulu kutoka kwa wadhifa wake. Akifanya hivyo, atakuwa akiwaokoa wakulima ambao huenda wakapoteza biashara kutokana na suala la maadili ambalo linazingira kuchaguliwa kwake,” akasema Bw Japheth Chepkwony, Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Tegat/Toror.

Wenyehisa katika kiwanda cha Tegat/Toror wanatarajiwa kukongamana kwa mkutano wa dharura mnamo Julai 18, 2024 ili kukataa au kuidhinisha kuchaguliwa kwa Chebochok.

Wakurugenzi wengine wa zoni ambao kuchaguliwa kwao kutaidhinishwa au kukataliwa ni Kemboi Geoffrey Kipkirui (Kapsaos),  Philiph kipkoech (Mosop), Japeth Chepkwony ( Kapsuser), Chepkirui Korir (Sosiot) na Evans Kiplangat (Waldai).

Masaibu ya Chebochok yalianza pale shirika la habari la BBC mnamo Februari 2023 lilipotoa video ikionyesha jinsi alivyokuwa akitaka uhusiano wa kimapenzi na wafanyakazi wa kike katika sekta ya majanichai.

Chebochok hakuwasaza wale ambao walikuwa wakisaka kazi katika Kampuni ya James Finlays ambako kampuni ya majanichai ilikuwa na kandarasi ya kutoa huduma.

“Tunawaomba radhi wanunuzi wa majanichai, mawakala na washikadau wengine kutokana na suala hili. Tunawahakikishia kuwa tumechukua hatua madhubuti ili  kuhakikisha sheria zinafuatwa na wale ambao wanashikilia nyadhifa muhimu wana maadili,” akaongeza Bw Chepkwony.