Habari Mseto

Shinikizo zazidi Kagwe ajiuzulu au afutwe kazi

September 5th, 2020 1 min read

FAITH NYAMAI na ONYANGO K’ONYANGO

MUUNGANO wa Makanisa ya Kipentekosti unamtaka Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, ajiuzulu kuhusiana na madai ya ufujaji wa fedha za Covid-19 katika Wizara yake.

Mwenyekiti wa Muungano huo, Askofu Jonah Kariuki alisema, Waziri anastahili pia kukamatwa na kushtakiwa kuhusu fedha hizo zilizodhamiriwa kuwasaidia Wakenya dhidi ya Covid 19.

‘Waziri ni mfano mbaya kabisa kwa uongozi tunaotaka katika taifa hili ndiposa kama kanisa tunamtaka ajiuzulu na kumruhusu mtu mwingine kuongoza Wizara ya Afya,’ alisema.

Aidha, muungano huo umemtaka Rais Uhuru Kenyatta ashirikiane na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, kuangamiza ufisadi nchini.

‘Rais alitueleza atapiga vita ufisadi lakini yote tunayoona nchini hayakubaliki kamwe,’ alisema Askofu Kariuki.

Alisema kanisa halitaunga mkono ufisadi kukita mizizi nchini huku raia wakiteseka.

“Tumeshangaa kwamba hela zilizotengwa kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 nchini zimeporwa katika usimamizi wa Waziri Kagwe,’ alisema.

Maaskofu hao wanamtaka Bw Kagwe kuelezea kwa kina jinsi fedha hizo zilitumika.

Kwingineko, Seneta wa Bomet Dkt Christopher Lang’at anamtaka Rais Kenyatta amfute kazi Bw Mutahi Kagwe na Katibu wa Wizara Susan Mochache.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Usambazaji Dawa Kenya (Kemsa) Jonah Manjari kuwahusisha wawili hao Ijumaa iliyopita, na sakata ya mabilioni ya fedha za Covid-19.

Dkt Langat alisema huu ni muda mwafaka kwa Rais Kenyataa kuonyesha kwa vitendo kwamba amejitolea kuangamiza ufisadi kama sehemu ya kujenga kumbukumbu yake.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa wakati wa mjadala kuhusu ugavi wa raslimali, Dkt Lang’at alisema Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) unaweza tu kufanikiwa ikiwa rais atawateua watu ambao hawataruhusu ubadhirifu wa fedha za umma chini ya usimamizi wao.