Shirika la feri lakubali lawama kuhusu ajali

Shirika la feri lakubali lawama kuhusu ajali

NA BRIAN OCHARO

SHIRIKA la Huduma za Feri (KFS), limekiri kwamba ajali iliyosababisha vifo vya Mariam Kighenda na bintiye Amanda Mutheu mwaka wa 2019 ingeepukwa iwapo feri hiyo ya Mv Harambee isingeruhusiwa kuhudumia wananchi ikiwa na hitilafu.

Akiwa mbele ya jopo la mahakma la kusikiliza kesi hiyo, mkuu wa shirika hilo alikiri kuwa gubeti ya feri haikuwa shwari ndiposa gari la marehemu likateleza hadi baharini akiwa ndani na binti yake.

Vile vile, mahakama iliambiwa hakukuwa na pesa za kukarabati feri wakati huo.

Gubeti ni sehemu ya feri ambayo huinuka wakati chombo hicho kikiwa majini ili kuzuia magari na binadamu kuteleza kutoka kwa feri, na huteremka kuwezesha uabiri mbali na kuepusha maji kuingia chomboni.

“Kama gubeti zingekuwa katika hali nzuri, zingezuia gari kurudi nyuma na kutumbukia ndani ya bahari. Ni bahati mbaya feri hiyo iliruhusiwa kuhudumu katika hali hiyo,” alisema Mkurugenzi mkuu wa KFS, Bw Bakari Gowa.

Alikabiliwa na wakati mgumu kuelezea ni hatua zipi alichukua kufanya marekebisho licha ya changamoto hizo kufikishwa kwake.

Bw Gowa alisema kuwa angefanya ukarabati kamili wa vyombo hivyo iwapo fedha za kutosha zingetolewa na serikali ya kitaifa.

“Shuguli za jumla za KFS ni jukumu langu lakini mikono yangu imefungwa ikiwa hakuna pesa. Inasikitisha kuwa ajali hiyo ilitokea. Ni kitengo cha uhandisi kinachohusika katika kurekebisha vyombo hivyo lakini uangalizi wa shuguli zote katika KFS ni jukumu langu,” alisema.

Bw Kennedy Mukhebu, ambaye ni mhandisi katika KFS aliambia jopo lililosimamiwa na Hakimu Mkuu wa Mombasa, Bi Martha Mutuku, kwamba dosari katika gubeti ndiyo ilisababisha ajali hiyo.

Bw Mukhebu alisimulia alivyoshuhudia ajali hiyo akiwa kwenye feri jioni hiyo

“Siwezi kusema kuwa Mv Harambee ilikuwa katika hali nzuri. Gubeti hizo zisingeweza kuinuliwa kwani zilikuwa mbovu. Nilisikia sauti ya tairi. Nilipotazama nyuma, gari hilo tayari lilikuwa limeteleza kupitia sehemu za mbele,” alisema shahidi huyo.

Shahidi huyo pia alikanusha madai kuwa bahari ilikuwa chafu wakati huo na kuchangia ajali hiyo.

“Hakukuwa na msukosuko ndani ya bahari. Hata kama kungekuwa na mawimbi, hayangweza kutikisa chombo hicho,” aliongeza Bw Mukhebu.

Shahidi huyo aliambia mahakama kuwa kabla ya ajali alikuwa ameandaa orodha ya kasoro katika vyombo hivyo ambavyo vilikuwa vinahitaji kufanyiwa marekebisho.

Hata hivyo, Bw Gowa alijitetea akisema kuwa feri hizo zimekuwa na matatizo ya mitambo hata kabla ya yeye kuchukua usukani mwaka wa 2016. Alisema serikali pamoja na uongozi wa awali ilikuwa inafahamu changamoto zinazokabili vyombo hivyo.

Kwa mfano, Bw Gowa alisema kuwa mwaka wa 2015, kulikuwa na hitilafu nyingi za feri na kusababisha wananchi kulalama lakini alipoingia, alijaribu kurekebisha vyombo hivyo.

Alisema feri zote ikiwemo Mv Harambee sasa zimetengenezwa na ziko katika hali nzuri. Vikao hivyo vitaendelea Julai 17.

  • Tags

You can share this post!

Nitajenga kwangu kasri la kula na kunywa – Rigathi

Uingereza wakomoa Italia na kufuzu kwa fainali ya Euro U-19...

T L