Makala

Shirika la kanisa la Faith Evangelistic Ministry lawapa matumaini wasichana wa Kiandutu

January 4th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwajali vijana waliokosa matumaini na wangetaka usaidizi unaostahili maishani.

Shirika moja la kanisa la Faith Evangelistic Ministry la Karen, Nairobi limejitolea kuwajali wasichana wa kijiji cha Kiandutu mjini Thika kwa kuwapa vyakula na kuwapa chakula cha kiroho.

Mchungaji Joseph Maina , mkewe na mshiriki mwenzao walizuru Chuo cha Africana College of Professionals mjini Thika, ambapo waliwashauri wasichana kutoka kijiji cha Kiandutu ambao wamepitia masaibu mengi ya kimaisha.

Wasichana hao wapatao 20 walijumuika katika chuo hicho ili kupokea ushauri wa kisaikolojia na maombi ya kiroho kwa pamoja.

Wasichana hao waliweza kupewa vyakula vya unga wa ngano, mahindi, mchele, na mafuta ya kupikia.

Shirika limejitolea kuwajali wasichana wa kijiji cha Kiandutu mjini Thika kwa kuwapa vyakula na kuwapa chakula cha kiroho.

Shirika moja la kanisa la Faith Evangelistic Ministry la Karen, Nairobi lawajali wasichana wa kijiji cha Kiandutu mjini Thika kwa kuwapa vyakula na kuwapa chakula cha kiroho. Picha/ Lawrence Ongaro

Mmoja wa wasichana wanaoishi maisha anayosema yana masaibu tele alisema wamekuwa wakidhulumiwa kingono kijijini huku wakiingilia uvutaji wa bangi na dawa za kulevya.

Lakini siku ya Jumamosi waliamua kubadili mienendo yao na kufuata maisha ya ukristo na ya matumaini.

“Mimi ninaishi katika kijiji cha mabanda cha Kiandutu ambapo wazazi wangu hawajiwezi kifedha na kwa hivyo ninapata maisha inakuwa sio ya kutamanika tena,” alisema msichana huyo.

Msichana mwingine alisema maisha Kiandutu ni magumu ajabu ambapo “hata baada ya kupata mtoto nilishindwa jinsi ya kumlea kwa sababu mwanamume ambaye alihusika na kunipa mimba alipotea kabisa na sijamuona tena.”

Wengi wa wasichana hao waliofika katika mashauriano hayo walielezea maisha magumu ambayo wamepitia kwa muda mrefu na baada ya kuombewa na kupokea ushauri walichangamka na kuahidi ya kwamba watakuwa watu wema wa kuigwa na wengine.

Mchungaji Maina aliwahimiza wasome Biblia kila mara ili kujiliwaza kimaisha kwa sababu Mungu pekee ndiye kimbilio la kila mmoja wetu.

“Ningetaka msome Mathayo 6: 26 ambapo maandiko yanatukumbusha kuhusu ndege wa angani ambao hawajali watakachokila lakini Mungu huhakikisha wanapata chakula na pia hawalimi na kuvuna shambani lakini ni wema kutuliko,” alisema Mchungaji Maina.

Wakati wa ushauri huo wasichana wapatao 15 waliokoka na kukubali kuifuata njia ya kumtumainia Mungu na kutubu kwa kusema watamfuata bila kulegea.

Mshauri wa kisaikolojia Dkt Susan Gitau ambaye ndiye mkurugenzi wa Chuo cha Africana College of Professionals mjini Thika na pia mhadhiri katika Chuo cha Nazarene jijini Nairobi, aliwahimiza wasichana hao kujiamini na kujikubali ili kuondoa dhana mbaya kuwa wametelekezwa.

“Ni vyema kwanza kumweka Mungu Muumba mbele ili kuweza kutuongoza kufanya yote mazuri tunayotarajia kutekeleza. Mimi nitoapo ushauri kwanza huwahimiza wateja wangu kumweka Mungu mbele kwanza kwa sababu yeye ndiye mweza yote,” alisema Dkt Gitau.

Aliwashauri wasichana hao kujisahili kwanza na kuwa wazi wanapojieleza ili matatizo yao yaweze kutatuliwa kwa ushauri unaostahili.

Alipendekeza kuwe na mikutano ya kila mara ya maombi ili kuwakuza wasichana hao kiroho na kisaikolojia huku pia akiwataka vijana wengine walioathirika kimaisha wajitokeze wazi ili wapewe ushauri utakaowaponya ili kujiondoa kwa masaibu yao.