Kimataifa

Shirika la ndege la Uingereza lasitisha safari za nchini China hofu kuhusu Corona ikitanda

January 29th, 2020 1 min read

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

SHIRIKA la Ndege la Uingereza – British Airways – limesitisha safari zote kutoka na kuingia nchini China wakati huu ambapo virusi vya Homa ya China vinaenea kwa kasi.

Hatua ya shirika inajiri baada ya Afisi ya Uingereza kuhusu Masuala ya Kigeni kushauri raia wa nchi hiyo kutozuru taifa hilo.

Shirika hilo la ndege zake hufanya safari hadi Shanghai na Beijing kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Hearthrow. Hatua hiyo imejiri wakati ambapo Serikali ya Uingereza imekamilisha mipango ya kuwaondoa raia wake kutoka mji wa Wuhan na mkoa wa karibu wa Hubei.

Virusi hivyo vya coronavirus vinavyosababisha homa hiyo tayari vimesababisha vifo vya watu 130 nchini China pekee na watu 16 katika mataifa mengine.

Tangu Jumatatu wiki hii mamia ya raia wa kigeni wamekuwa wakihamishwa kutoka jiji la Wuhan ambalo ugonjwa huo hatari ulianza.