Habari Mseto

Shirika la Posta kufanyiwa mageuzi ili kuendana na teknolojia ya kisasa

October 10th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI imetangaza mpango wa kulifanyia mageuzi shirika la Posta Kenya ili kuoanisha huduma zake na ukuaji wa teknolojia nchini.

Kulingana na Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano (ICT) Bw Joe Mucheru, baadhi ya mikakati hiyo ni kuunganishwa kwa huduma za utumaji na upokeaji barua, ambapo zitakuwa zikiendeshwa kwa mfumo wa teknolojia.

Waziri alisema kuwa kulingana na mpango huo, anayetuma ama anayepokea barua atakuwa na uwezo wa kutumia namba yake ya simu kama anwani yake.

“Huu ni mpango ambao tayari unaendeshwa katika nchi zilizostawi kiuchumi kama Amerika, Japan na Uingereza, ambapo wateja wamekuwa wakitumia namba za simu kama anwani zao kutuma ama kupokea barua bila matatizo yoyote,” akasema Bw Mucheru.

Alitoa kauli hiyo Jumatano kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Bi Julia Anyango jijini Nairobi, katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Huduma za Posta Duniani.

Kutuma na kupokea pesa

Kwenye mpango huo, serikali pia inapanga kuliwezesha shirika hilo kuanza kutoa huduma za fedha kwa njia ya simu, ambapo wateja watakuwa na uwezo wa kutuma ama kupokea pesa kwa mfumo wa dijitali.

Tayari, majaribio hayo yameanza katika kaunti tano, zikiwemo Vihiga, Kitui, Kisumu, Uasin Gishu na Mombasa. Ikiwa utafaulu, mpango huo utasambazwa katika kaunti zote 47.

“Tunachukua hatua hii ikizingatiwa kuwa mfumo wa utumaji fedha sasa unaendeshwa kwa njia ya teknolojia. Hatua hii ni kuwawezesha wateja wetu, hasa walio katika maeneo ya mashambani kunufaika kwa huduma hizo,” akasema.

Wakati huohuo shirika lilitangaza wanafunzi watano walioibuka bora kwenye shindano la kuandika barua mwaka huu.