Shirika la PrimRose laokoa walevi Gatundu Kaskazini

Shirika la PrimRose laokoa walevi Gatundu Kaskazini

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kawira eneo la Gatundu Kaskazini, wanalalamikia jinsi pombe haramu imefanya vijana kushindwa kufanya kazi.

Mjane mmoja Bi Felista Wambui anasema ya kwamba familia yake ya watoto 14 ni mzigo kwake na tayari vijana wake watatu wametekwa nyara na pombe haramu.

Alieleza kuwa baada ya mume wake kuaga dunia miaka michache iliyopita, aliachwa na familia kubwa ambayo hawezi kuisimamia ipasavyo.

“Tayari mimi ni mjane ambaye amelemewa na mzigo wa familia. Vijana wangu wengine ni walevi ambapo hakuna kazi yoyote wanayojishughulisha nayo,” alifafanua mjane huyo na kuongeza maisha yamenifikisha ukingoni hata sijui nifanyeje.

Alidai kuwa mtoto wake wa kiume kwa jina la utani ‘Komero’, amelemewa na pombe ambapo kutoka asubuhi hadi jioni yeye uraibu wake ni kulewa chakari

Hivi majuzi kijana wake mwingine alibomoa paa la nyumba na kuuza mabati hayo ili apate angalau hela ya kupata ‘kinywaji’.

“Kwa sasa anaishi kwa nyumba ambayo imebomolewa paa upande fulani. Jambo hilo limenikera na hata kukasirisha wanakijiji wa eneo hili,” alifafanua Bi Wambui.

Hata hivyo, shirika moja lisilo la kiserikali la Primrose Rehab and Wellness, limejitolea kuhifadhi kijana mmoja wa mama huyo ili aweze kupewa mwongozo jinsi ya kurekebisha maisha yake.

Bw Joseph Kamau ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo alisema walichukua hatua hiyo ya dharura baada ya jambo hilo kuangaziwa katika kituo cha redio cha Inooro wiki moja iliyopita.

“Sisi kama shirika la kurekebisha tabia tuliona ni vyema tuingilie kati ili kuokoa maisha ya kijana huyo ambaye alionekana kuathirika kutokana na unywaji wa pombe haramu,” alieleza Bw Kamau.

Alisema watakuwa naye katika kituo hicho kwa muda wa miezi mitatu mfululizo ili kukagua mienendo yake huku akipokea mawaidha na matibabu.

Alieleza pia kuwa shirika hilo linatetea watu walioathirika kutokana na ulevi, dawa za kulevya na waliozamia kwenye mchezo wa kamari.

Hivi majuzi wakazi wa kijiji hicho walitaka serikali kuingilia kati jambo hilo kwa sababu vijana wengi wameshindwa kuoa na wengine wameasi familia zao.

Ilidaiwa pia hakuna boma la kujivunia kwa sababu vijana wengi hawapatikani nyumbani, kutekeleza majukumu yao.

Wakazi wa eneo hilo wamepongeza hatua iliyochukuliwa na shirika hilo la Primrose Rehab and Wellness, huku wakitaka lifanye juhudi kuwapokea vijana zaidi ili kuwarekebisha tabia na kuwapa mwongozo wa kimaisha.

You can share this post!

Nyundo ya West Ham United yazamisha Chelsea ligini

Bei ghali ya chakula cha mifugo yatishia kuzima jitihada za...

T L