Habari

Shirika la reli lasema utupaji holela wa taka huziba mitaro na kusababisha mafuriko

December 6th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKA la Reli la Kenya limelaumu wakazi wanaoishi karibu na reli za garimoshi kwa hatua yake ya kuondoa huduma za usafiri jijini Nairobi hapo Alhamisi kutokana na mafuriko.

Katika taarifa kutoka kwa kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw Jamhuri Mainga anasema kuwa shirika hilo lilifutilia mbali safari za kutoka kituo kikuu cha Nairobi hadi vituo vya Kikuyu, Ruiru, Embakasi, na Syokimau kwa sababu kuzibwa kwa mitaro ya majitaka kulisababisha mafuriko, ambayo hayangewezesha usafiri.

“Sehemu kadhaa za reli zetu za treni zilikuwa majini kwa sababu ya mafuriko yalizifanya zisipitike,” anasema.

“Tulilazimika kufutilia mbali safari za treni kwa sababu tulihofia usalama wa wateja wetu,” aliongeza na kuhakikishia watumiaji wa treni kuwa wafanyakazi wake wanashughulika kutatua tatizo hili ili huduma zirejelewe.

“Tunaangalia hali ilivyo na tutatoa taarifa za mara kwa mara kufahamisha wateteja wetu,” anasema.

Bw Mainga anasema kuwa katika mpango mkubwa wa shirika hilo, vituo 10 vipya vinaendelea kukarabatiwa. Vituo hivyo ni Ruiru, Kahawa, Githurai, Kikuyu katika kaunti ya Kiambu; Mwiki, Dandora, Donholm, Pipeline, Embakasi Village katika kaunti ya Nairobi; na Athi River katika kaunti ya Machakos.

Treni inayohudumu barabara ya Ruiru-Nairobi hubeba abiria kutoka maeneo ya Kahawa, Githurai, Mwiki, Maili Saba, Dandora, Mtindwa na Makadara. Ile ya Embakasi Village-Nairobi inatumiwa na wakazi wa Aviation, Tai Mall, Avenue Park, Quarry, Donholm, Pipeline na Makadara.

Treni hizi mbili pamoja na ile ya Syokimau-Nairobi inayosimama Imara na Makadara, ziliathiriwa vibaya na mafuruko katika kituo cha Makadara, ambacho hakikuwa kinapitika kwa sababu mafuriko.

Mafuriko pia yalishuhudiwa katika vituo vya Maili Saba katika mtaa wa Dandora na Mukuru Kwa Njenga.

Garimoshi la ruti ya Kikuyu-Nairobi kupitia vituo vya Thogoto, Dagoretti Station, Lenana, Satellite, Kibera, Gatwekera, Mashomoni na Laini Saba pia halikuhudumia wateja wake kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa kote nchini.

Treni hizi nne huhudumia karibu wateja 9,000 kila siku. Zote huhudumu asubuhi na jioni isipokuwa wikendi. Maelfu ya watumiaji wa treni wamelazimika kutembea kwa miguu ama kuabiri magari ya umma, ambayo yalitumia kukosekana kwa treni kuongeza nauli.